Otieno apewa dk 90 Prisons,  Mgunda azitaka tatu Sokoine 

BAADA ya kusota kwa muda mrefu kwa matokeo mabaya, Tanzania Prisons imeapa kuangusha mbuyu kwa kuwazima Namungo ili kurejesha ari na furaha kwa mashabiki wa timu hiyo.

Prisons inatarajia kushuka uwanjani kesho kuwakaribisha wapinzani hao mchezo utakaopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, huku ukiwa maalumu ‘kumuaga’ Kocha Mkuu wa timu hiyo, Zedekiah Otieno, raia wa Kenya.

Otieno aliyetambulishwa mapema msimu huu kuiongoza timu hiyo inayomilikiwa na Jeshi la Magereza, amekutana na upepo mbaya baada ya kusimamia michezo 12 akishinda miwili, sare tatu na kupoteza saba na kuwa nafasi ya 15 kwa pointi tisa.

Habari za ndani ilizopata Mwanaspoti ni kuwa Kocha huyo asiye na maneno mengi baada ya kupewa michezo mitatu nyuma ikiwa ni kipimo amepoteza miwili dhidi ya Mtibwa Sugar 2-1 na Coastal Union 4-0 na sare dhidi ya Mashujaa.

Kufuatia matokeo hayo, imeelezwa kuwa vigogo walikaa vikao vya mara kwa mara na kuamua kumpa ‘byeybye’ Kocha huyo ambapo, kesho itakuwa mchezo wake wa mwisho kubaki kikosini humo, huku uongozi ukiendelea kumtafuta mbadala wa kumalizia Ligi.

Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Innocent Mwangonde amesema kwa sasa hawaangalii mechi zilizopita na badala yake akili na nguvu zote zipo kwenye mchezo dhidi ya Namungo kuhakikisha wanakufa naye Sokoine.

“Tumeandaa kisaikolojia wachezaji, mpira una matokeo yake ya kuumiza na kufurahisha, kwa sasa hatufikirii yaliyopita badala yake kazi moja tu ni kufa na Namungo waache pointi tatu, hii ni zamu yetu kushinda,” amesema Mwangonde.

Kwa upande wake, Emanuel Martin amesema wamepitia mambo magumu zaidi na sasa kazi iliyobaki ni kupigania nembo ya Prisons kuhakikisha wanashinda mechi zilizobaki wakianza na Namungo.

“Kama ni mtoto kukosea akasahihishwa na mzazi na sisi tumegundua tulipokosea na tumejifunza kwa makocha wetu, tunaahidi kesho kushinda mechi hiyo ili kurudi upya mchezoni,” amesema Martin.

Kocha Mkuu wa Namungo, Juma Mgunda amesema mchezo huo ni muhimu sana kwao na wanatambua ugumu utakaokuwapo kwakuwa wapinzani hawapo sehemu nzuri hivyo presha yake wanaifahamu.

“Hatutawadharau, huu ni mchezo muhimu kama ilivyo mechi nyingine tunaijua presha ilivyo kwetu na kwao vilevile, tunahitaji ushindi baada ya kupoteza mechi yetu iliyopita kupunguza maumivu,” amesema Mgunda.