Wanne wafikishwa mahakamani kwa tuhuma za wizi wa ‘Ambulance’

Musoma. Watu wanne wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Musoma mkoani Mara wakidaiwa kuhusika na wizi wa gari la kubeba wagonjwa la Manispaa ya Musoma kisha kulibadilisha na kuwa la biashara ya kubeba watalii.

Washtakiwa hao wamefikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Hadija Masala leo Ijumaa Februari 13,2026 na kusomewa mashtaka matatu likiwamo kosa la uhujumu uchumi.

Washtakiwa hao ni Goodluck Chacha (26) ambaye ni dereva na mkazi wa Tarime mkoani Mara na  Karume Kihedu (26) mkazi wa Arusha.

Gari la wagonjwa la hospitali ya Manispaa ya Musoma kabla halijabadilishwa mwonekano na kuwa la kubeba watalii.



Wengine ni Saidi Ramadhani (39) na Elias Joakim (53)  wote wakazi wa Arusha.

Akisoma mashtaka hayo mahakamani hapo, Wakili wa Serikali, Michael Kayombo amesema washtakiwa wote wanne wanashtakiwa kwa kosa la utakatishaji wa fedha kinyume cha kifungu 12 (d) na 13(a) ya sheria ya udhibiti utakatishaji wa fedha sura namba 423 ambayo inasomwa pamoja na kifungu cha 57(1) na 60(2) cha sheria ya uhujumu uchumi na udhibiti wa uhalifu wa kupanga.

Amesema washtakiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kupokea Sh55 milioni kutoka kwa Alexia  Baraka huku wakijua kuwa  fedha hizo ni zao la uhalifu na kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Kayombo amesema mshtakiwa wa kwanza pia anashtakiwa kwa kosa la wizi kinyume na kifungu cha 258 (1) na 265 (1) ya sheria ya kanuni ya adhabu sura namba 16 marejeo ya 2023.

Washtakiwa wanne wanaodaiwa kuhusika na wizi wa gari la kubeba wagonjwa la Manispaa ya Musoma na kisha kulibadilisha na kuwa gari la biashara ya kubeba watalii wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma. Picha na Beldina Nyakeke



“Wewe Goodluck Chacha Oktoba 25,2025 katika Manispaa ya Musoma eneo la maegesho ya magari lilipo ndani ya manispaa uliiba gari aina ya Toyota Landcruiser lenye namba STM 7830 mali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lenye thamani ya Sh180 milioni,” amesema.

Amesema mshtatiwa huyo wa kwanza pia anashtakiwa kwa tuhuma za kuongoza genge la uhalifu kinyume na aya ya 4(1) (d) ya jedwali la 1 kifungu cha 57(1) na 60 (2) cha sheria ya uhujumu uchumi na udhibiti wa uhalifu wa kupangwa sura namba 200 marejeo ya mwaka 2023.

“Wewe Chacha Oktoba 25, 2025 na Oktoba 27,2025 katika maeneo tofauti ndani ya Manispaa ya Musoma mkoani Mara na Arusha ukiwa sio ofisa wa umma ulihamasisha biashara ya uhalifu kwa nia ya kupata faida kinyume cha sheria,” amesema.

Gari la wagonjwa la hospitali ya Manispaa ya Musoma baada ya kubadilishwa mwonekano.



Kayombo amesema upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika, hivyo kuiomba Mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kesi hiyo kutajwa.

Kufuatia maelezo hayo, hakimu Masala ameahirisha kesi hiyo hadi Februari 26,2026 itakaposomwa.

Awali, hakimu Masala amesema Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, hivyo washtakiwa hawaruhusiwi kujibu chochote.

“Kwa sababu kesi yenu inahusisha makosa mbalimbali likiwamo kosa la uhujumu uchumi, Mahakama hii haina mamlaka ya kuendesha kesi hii hivyo washtakiwa hamtatakiwa kujibu chochote zaidi ya kusikiliza,” amesema.

Baada ya maamuzi hayo washtakiwa kwa pamoja wamerudishwa rumande hadi Februari 26,2026 kesi hiyo itakapokuja mahakamani hapo tena.