Mbeya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa amezitaka kampuni za bima kutoa huduma zinazozingatia hali halisi ya maisha na shughuli za kiuchumi za wananchi, ikiwamo kilimo na uchimbaji madini, ili kuwawezesha kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.
Amesema kila mkoa una shughuli zake za uzalishaji, akitolea mfano Mkoa wa Arusha unaotegemea zaidi utalii, huku Mkoa wa Mbeya ukiwa na wananchi wengi wanaoshiriki katika mnyororo wa thamani wa kilimo na baadhi ya maeneo, hususan Chunya, yakijikita katika uchimbaji madini.
Hivyo, amesisitiza kuwa huduma za bima zinapaswa kuendana na mazingira na mahitaji ya wananchi wa eneo husika.
Malisa ametoa kauli hiyo wakati akizungumza kwenye hafla ya uzinduzi wa ofisi ya Strategis Insurance iliyofanyika usiku wa kuamkia leo, Ijumaa Februari 13.
Amesema bima ni nyenzo muhimu katika kulinda ustawi wa maisha ya mwananchi na shughuli zake za kila siku.
Amebainisha kuwa, Serikali tayari imezindua mpango wa bima ya afya kwa wote kama sehemu ya kutambua umuhimu wa huduma hiyo, hivyo uwepo wa taasisi za bima mkoani Mbeya, utasaidia wananchi kuwa na uhakika wa maisha yao ya baadaye.
“Niwapongeze Strategis Insurance kwa kuichagua Mbeya kufungua tawi. Nawashauri mtoe huduma kulingana na shughuli za wananchi.
“Hapa wengi wako katika mnyororo wa kilimo na kule Chunya kuna uchimbaji. Wafikieni na wapewe huduma stahiki,” amesema Malisa.
Ameongeza kuwa ni muhimu hata mkulima mwenye ekari tano za viazi kuwa na bima, ili kuondoa dhana potofu kuhusu huduma hiyo. Amesema katika ukanda wa Nyanda za Juu Kusini, shughuli kubwa ni kilimo, hivyo kuna haja ya kuwalinda wakulima wanaopata hasara, ikiwamo kuunguliwa mazao au mali zao, pamoja na kuwajumuisha wachimbaji wadogo kwa kuwapatia elimu ya bima.
Mkurugenzi Mtendaji wa Strategis Insurance, Jabir Kigoda amesema kampuni hiyo imejipanga kuwafikia wananchi wengi nchini kwa kutoa huduma bora katika maeneo mbalimbali.
Amesema taasisi hiyo itatoa huduma za bima ya moto, wizi, magari, kilimo, afya na biashara, huku ikitambua fursa zilizopo mkoani Mbeya kulingana na shughuli za wananchi wake.
Kigoda amesema kufunguliwa kwa tawi la Mbeya ni sehemu ya mkakati wa kampuni hiyo kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi kwa kuzingatia ubora, uwadilifu na ubunifu. Ameongeza kuwa baada ya kufanikiwa katika mikoa ya Mwanza, Arusha, Zanzibar, Dar es Salaam na Dodoma, sasa wameona umuhimu wa kupanua wigo kwa kuwekeza Mbeya.
“Msingi wetu mkuu ni kuwafikia wananchi wengi zaidi. Tumechagua Mbeya kwa sababu ya fursa zilizopo katika kilimo, uchimbaji na biashara. Tunaamini ushirikiano na wananchi utatuwezesha kutoa huduma kwa ufanisi,” amesema Kigoda.
Mmoja wa washiriki wa hafla hiyo, Khelly Sichone amesema bima ni huduma yenye umuhimu mkubwa katika maisha ya sasa, akisisitiza kuwa kinachohitajika zaidi ni utoaji wa elimu kwa wananchi ili waelewe faida zake.
Amesema licha ya bima kutokuwa na manufaa yanayoonekana mara moja, ni kinga muhimu kwa wajasiriamali, wakulima na wasafirishaji wanapokumbwa na majanga.
Ametoa mfano kuwa bado wamiliki wengi wa vyombo vya moto kama bajaji na bodaboda hawana bima, hali inayowaweka hatarini wanapopatwa na ajali.
Ameongeza kuwa zipo pia bima za mifugo, nyumba na kilimo, hivyo kampuni zinapaswa kuongeza juhudi za kutoa elimu kwa umma.
Jeremiah Msemwa, amesema bima ni huduma muhimu inayopaswa kupatikana kwa kila mwananchi kwa kuwa shughuli zozote za kiuchumi zinaweza kukumbwa na majanga na kusababisha hasara.
Amesema hata mizigo inayosafirishwa inahitaji bima kutokana na changamoto zilizopo katika biashara, hivyo kuna haja ya kuendesha kampeni za uhamasishaji ili wananchi wengi zaidi waweze kuilinda mitaji na usalama wao kupitia huduma za bima.