Unamkumbuka Pantev? Sikia alichosema! | Mwanaspoti

KOCHA Dimitar Pantev ameibuka na kuvunja ukimya  kufuatia kurejea nchini Botswana, akisema uamuzi wake wa kujiunga na Klabu ya Jwaneng Galaxy ni sehemu ya kujitathmini na kujipanga upya baada ya kipindi kifupi na chenye mafunzo mengi akiwa na Simba.

Pantev ametambulishwa rasmi na Jwaneng Galaxy kuelekea msimu ujao wa mashindano, hatua inayotajwa na wengi kama mwanzo mpya kwake baada ya kuachana na wekundu hao wa Msimbazi.

Kupitia taarifa rasmi za klabu hiyo ya Botswana, uongozi umeweka wazi dhamira ya kuimarisha benchi la ufundi na kuongeza ushindani wa timu katika mashindano ya ndani na kimataifa.

Akizungumza na Mwanaspoti baada ya utambulisho wake, Pantev amesema kurejea Botswana sio hatua ya kurudi nyuma, bali ni fursa ya kuendelea kujenga alichokianza awali katika soka la nchi hiyo.

“Ninaifahamu vizuri ligi ya Botswana na mazingira yake. Nimerudi nikiwa na uzoefu zaidi na njaa ya mafanikio,” amesema kocha huyo raia wa Bulgaria.

Ndani ya mwaka jana, 2025, rekodi zinaonyesha Pantev amefundisha timu mbili tofauti. Alianza na Gaborone United Januari 23 ambako alidumu kwa miezi minane (siku 254), kabla ya kutua Simba SC alikodumu kwa miezi miwili (siku 61).

Kipindi chake Simba hakikuwa kirefu kama alivyotarajia lakini amesema kilikuwa cha kujifunza mengi. “Simba ni klabu kubwa yenye presha ya matokeo ya haraka. Nimejifunza namna ya kushughulikia matarajio makubwa ya mashabiki na uongozi,” alieleza.

Pantev aliondoka Simba ikiwa ni siku mbili kabla ya mechi dhidi ya Mbeya City katika Ligi Kuu Bara  huku kukiwa na pambano jingine zito la Mzizima Dabi dhidi ya Azam lililokuwa linatarajiwa kufanyika Desemba 7, 2025. Hata hivyo, alieleza kuwa maamuzi katika soka wakati mwingine hayangoji ratiba.

Amesema licha ya mambo kutokwenda kama alivyotaka, bado anaiheshimu Simba na mashabiki wake. “Tulikuwa na mpango wa muda mrefu lakini soka lina maamuzi ya papo kwa papo. Nawashukuru kwa nafasi ambayo walinipa,” amesema.

Pantev amechukua mikoba ya Sean Connor ambaye mkataba umefikia tamati. Uongozi wa klabu hiyo umemshukuru Connor kwa mchango na mafanikio aliyoyapata huku ukimtakia kila la heri katika hatua zinazofuata za taaluma yake.