Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Patrice Motsepe amezihakikishia nchi za Tanzania, Kenya na Uganda kuwa zitaandaa Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 kama ilivyopangwa.
Motsepe ametoa uhakika huo leo, Ijumaa, Februari 13, 2027 wakati akitoa mrejesho wa Kikao cha Kamati ya Utendaji ya CAF kilichoketi Dar es Salaam.
Motsepe amesema hakuna kitakachobadilika na jambo la msingi ni nchi hizo kuhakikisha zinafanya maandalizi ya uhakika.
“Nina imani kupitiliza kwamba mashindano yatafanikiwa. Tunatakiwa kuamini kwetu wenyewe Waafrika na watu wetu.
“Siku zote kumekuwa na shauku sisi Waafrika kuonyesha watu wetu kuwa tunaweza kuandaa AFCON kwa mafanikio. Siku zote tunatakiwa kutuma meseji kwa watu wetu wote Afrika kwamba tunaamini kwa uwezo kufanikiwa na kufanya mazuri duniani kwa vile tuna uwezo.
“Ninasisitiza kuwa nina imani kubwa kwamba tutafanya kazi na kamati yetu ya utendaji. Kutakuwa na taarifa kwenye vyombo vya habari kwamba viwanja haviko tayari, meneo ya kuchezea hayako tayari lakini tutatatua hayo matatizo,” amesema Motsepe.
Motsepe amewashukuru Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Rais wa Kenya, William Ruto na Rais wa Uganda, Yoweri Museveni pamoja na raia wa nchi hizo kwa juhudi kubwa wanazoendelea kuzifanya kuhakikisha fainali hizo za mwakani zinafanyika kwa ukamilifu.
“Tunahitaji viwanja 24 vya kisasa vya mazoezi na viwanja sita vya mechi. Kwa nchi hizo kukutana pamoja, ukiondoa suala la mpira, watu wetu wanapata ajira. Uwekezaji na kuinua hali ya maisha ya watu.
“Miundombinu yote hiyo itatumiwa na klabu, timu za taifa hivyo viwanja vyote vitatumika baada ya mashindano kumalizika,” amesema Motsepe.