Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba ameziagiza kamati za ulinzi na usalama nchini kudumisha maelewano na amani kwa kuwachukulia hatua wanaovunja sheria.
Mwigulu amesema hayo leo Ijumaa, Februari 12, 2026 katika ziara yake mkoani Tanga alipozungumza na viongozi na wananchi waliojitokeza katika uzinduzi wa mradi wa umeme Kijiji cha Mkata Wilaya ya Handeni mkoani humo.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwigulu amesema wanaovunja sheria za nchi hawapaswi kuonewa huruma ili kuepusha madhara ya uvunjifu wa amani wanayoweza kusababisha katika jamii kutokana na uhalifu wao.
“Nawaagiza kamati zote za usalama, msiwe na huruma na wavunja sheria. Lazima watu waheshimu na wafuate sheria, hatuwezi kuruhusu watu wachache watumie nafasi zao kuumiza wengine na Serikali hatutalifumbia macho hilo,” ameagiza.
Maagizo hayo ya Waziri Mkuu yamekuja baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa wananchi na viongozi wa mkoa huo waliodai kuwa katika Kijiji cha Mkata na maeneo mengine ya mkoa huo kumekuwa na migogoro ya wakulima na wafugaji inayohusisha maeneo ya kilimo na malisho.
Migogoro hiyo imedaiwa kuwa imeendelea kujirudia hali inayosababisha mapigano na hata vifo katika maeneo kadhaa, hivyo kutishia hali ya amani na usalama katika eneo hilo.
Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Mradi wa kupooza umeme uliopo Mkata mkoani Tanga ambao una uwezo wa 2X60MVA 132/33kV, pamoja na ujenzi wa njia za kusambaza umeme msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa kilomita 45 kutoka kituo cha Mkata kwenda kijiji cha Kwamsisi .
Akizungumzia migogoro hiyo, Waziri Mkuu huyo amewataka wananchi kudumisha udugu na maelewano miongoni mwao bila kubaguana huku akiwataka viongozi kutoingia kwenye mkumbo wa kutoa adhabu kwa jamii nzima pale mtu mmoja anapofanya kosa kutoka katika jamii hiyo.
“Akifanya kosa mtu tusishughulike na jamii nzima, tushughulike naye binafsi maana anataka kutupeleka pabaya. Mkulima asimuone mfugaji kuwa adui na mfugaji asimuone mkulima kuwa adui, tusiruhusu huu ufa tutaharibu, hapana,” amesisitiza.
Mwigulu ameweka mkazo kuwa Mtanzania yeyote ana haki ya kuishi popote anapopataka ndani ya nchi yake ilimradi tu afuate sheria huku akiweka wazi kuwa idadi ya watu inaendelea kuongezeka huku ardhi haiongezeki akiisihi jamii kubadili mtazamo na kuanza kuzalisha kwa tija katika eneo dogo.
Akizungumzia ujenzi wa miradi baada ya kupokea malalamiko na maelezo ya wananchi na viongozi wakiwamo wabunge wa mkoa huo, Mwigulu ameagiza ujenzi wa Shule ya Msingi Imani iliyopo Mkata wilayani Handeni uanze mapema mwezi ujao huku akiwaagiza makandarasi wote nchini kuhakikisha miradi inayojengwa inaendana na thamani ya fedha inayotolewa na serikali.
“Kwa miradi yote ya maji, umeme na mingine inayoendelea nitoe rai kwa makandarasi, fedha zote zinazotolewa zilingane na kazi inayofanyika na kwenye hili hatuna mzaha lazima tuone thamani ya fedha kwenye miradi. Wakandarasi wote mpate huu ujumbe sawasawa,” ameagiza.
Mbali na miradi ya maji na umeme inayoendelea kujengwa maeneo mbalimbali nchini, Mwigulu amesema katika siku 100 za Rais Samia Suluhu Hassan, ajira za ualimu 7000 na za watumishi wa sekta ya afya 5000 zimetolewa huku bika ya afya kwa wote ikianza kutekelezwa kwa makundi maalumu.
Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu ameambatana na viongozi mbalimbali wakiwamo mawaziri, wabunge na viongozi wa mamlaka mbalimbali za kitaifa na za Mkoa wa Tanga. Miongoni mwao ni Waziri wa Maji Jumaa Aweso ambaye amesema mradi mkubwa wa maji uliosuasua kwa miaka mingi unaotarajiwa kumaliza tatizo la maji katika mkoa wa Tanga, umefikia asilimia 75.
Kuhusu mgogoro wa wakulima na wafugaji uliodaiwa kutokana na mahitaji ya kilimo na malisho, mawaziri wa Wizara za Kilimo, Mifugo na Tamisemi wameeleza mikakati ya pamoja wanayoichukua ili kumaliza tofauti hizo na kujenga maelewano na usalama kwa jamii hizo.
Waziri wa Mifugo, Dk Bashiru Ali amesema wataalamu wa wizara hizo wanaendelea na mazungumzo ya kiushirikiano katika kutafuta suluhisho la dharura huku wakitafuta utatuzi wa kudumu wa malalamiko hayo ambayo yameibuliwa na viongozi wa eneo hilo wakiwemo wabunge.
“Rais Samia akiwa Mvomero mkoani Morogoro aliagiza mkakati wa ‘tupendane’ unaolenga kuwaleta pamoja wakulima na wafugaji, hivyo tuumie mkakati huu kuwaweka pamoja wazalishaji hawa muhimu,” amesema Ali.
Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo amewanyooshea kidole wafugaji wenye tabia ya kuhamahama kutafuta malisho huku wakivamia ardhi za wakulima na kusababisha migogoro akitoa wito kwa viongozi wa Serikali za vijiji na kata kusimama katika nafasi zao ili kumaliza migogoro hiyo.
Akitolea maelezo ukarabati wa Shule ya Msingi Imani iliyopo Kijiji cha Mkata baada ya kupokea malalamiko juu ya uchakavu wa madarasa na nyumba ya walimu unaoikabili, Waziri wa Tamisemi, Riziki Shemdoe ameahidi ujenzi wa madarasa manne akitaja vyanzo vya fedha kuwa vitatolewa na halmashauri na serikali kuu.
“Ninamuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni apeleke Sh50 milioni ajenge madarasa mawili na Katibu Mkuu wa Wizara alete milioni 50 za madarasa mawili ili tuweze kujenga madarasa manne tumalize tatizo la shule hii iliyopo Mkata magharibi,” ameagiza.