Madiwani wakumbushwa kutambua kaya maskini, bima ya afya

Kishapu. Katika juhudi za kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za afya bila vikwazo vya kifedha, Suala la bima ya afya kwa wote limeendelea kuwa ajenda muhimu kitaifa, wadau wakitaka kila usawa wa huduma kwa wote.

Akizungumza leo Ijumaa, Februari 13, 2026 katika baraza la madiwani, Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Kishapu, Emmanuel Johnson amewataka madiwani kushiriki kikamilifu katika masuala ya kijamii ikiwamo kuhamasisha uandikishaji wa watoto wa shule ya awali na kidato cha kwanza, pamoja na uhamasishaji wa bima ya afya kwa wote.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Emmanuel Johnson katika kikao cha baraza la madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu cha kilichopitisha bajeti ya Sh. 54.3 bilioni kwa mwaka wa fedha 2026/2027.



“Madiwani mnatakiwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii ikiwa ni pamoja na utambuzi wa kaya zisizo na uwezo ili ziweze kunufaika na mpango wa kugharamiwa na Serikali katika bima ya afya kwa wote sambasamba na uandikishaji wa watoto elimu ya awali na kidato cha kwanza” amesema Johnson.

Mwenyekiti wa Halmashauri, Josephat Limbe amewapongeza madiwani kwa kujadili kwa kina mapendekezo bajeti kuanzia ngazi ya kamati za kudumu hadi vikao vya vyama vya siasa kabla ya kuidhinishwa rasmi na baraza, huku akisisitiza kuwa usimamizi madhubuti wa mapato ya ndani.

“Nawasihi madiwani kushiriki kikamilifu katika kusimamia ukusanyaji wa mapato ndani ya kata zenu ili kufanikisha utekelezaji wa shughuli zote za halmashauri na miradi ya maendeleo” ameongeza Limbe.

Hata hivyo, Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga limepitisha bajeti ya Sh54 bilioni  kwa mwaka wa fedha 2026/27 kati ya fedha hizo, Sh2.8 bilioni zimetengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo.

Katika picha ni madiwani wakiwa katika kikao cha baraza Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu cha kilichopitisha bajeti ya Sh. 54.3 bilioni kwa mwaka wa fedha 2026/2027.



Katibu Tawala wa Wilaya ya Kishapu, Fatma Mohammed amewapongeza madiwani kwa kupitisha bajeti hiyo na kushauri halmashauri kuendelea kubuni na kuimarisha vyanzo vipya vya mapato ili kuongeza uwezo wa kifedha wa wilaya.

“Kupitishwa kwa hii ya bajeti hiyo kunatarajiwa kuimarisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, kuboresha huduma za kijamii na kuendeleza miundombinu, hatua ambayo inalenga kuinua ustawi wa wananchi wa wilaya ya Kishapu katika mwaka wa fedha ujao” amesema Fatma.