Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Patrice Motsepe amefichua kuwa alitamani mechi ya marudiano ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya Simba na RS Berkane, Mei 25, 2025 ichezwe katika Uwanja wa Benjamin Mkapa na sio New Amaan Complex, Zanzibar.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo Februari 13, 2026 jijini Dar es Salaam, Motsepe amesema kuwa hali ya uwanja haikuruhusu jambo lililopelekea mechi ichezwe Zanzibar.
“Mwaka jana nilitamani sana Simba SC wacheze fainali yao Benjamin Mkapa kwa sababu mimi natamani kuona uwanja umejaa.
“Ripoti zilivyokuja na kusema kuwa uwanja hauko tayari nilisema fanyieni kazi fainali ifanyike hapo lakini mpaka mwisho ilishindikana,” amesema Motsepe.
Katika mchezo huo wa fainali, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1 na RS Berkane kutwaa ubingwa kwa ushindi wa jumla ya wa mabao 3-1.
Mchezo wa kwanza baina ya timu hizo uliochezwa Berkane, Morocco, wenyeji RS Berkane waliibuka na ushindi wa mabao 2-0.