Dar es Salaam. Tanzania inatarajia kufanya maonyesho ya tatu ya kimataifa ya mifugo Julai mwaka huu, hatua inayotarajiwa kuchochea mapinduzi ya biashara kwa wafugaji wa ndani na nje ya nchi.
Maonyesho hayo, yatakayohusisha mataifa ya Tanzania, Kenya na Namibia, yanafanyika chini ya udhamini wa Benki ya NMB, iliyoyadhamini kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka huu hadi 2028.
Katika udhamini huo wa maonyesho hayo ya Tri-Nations Livestock Expo 2026–2028 yanayoandaliwa na Mbogo Ranches Limited, NMB imetoa Sh300 milioni.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini wa mkataba wa udhamini leo, Ijumaa, Februari 13, 2026, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Fabian Madele, amesema hatua hiyo itaharakisha mageuzi katika sekta ya mifugo.
Amesema maonyesho hayo yatafanyika Juni 19 hadi 21, 2026, Ubena Zomozi mkoani Pwani, na kwamba yanalenga kuimarisha ubora wa mifugo kikanda kupitia biashara, ubunifu na ushirikiano.
“Wakati akituapisha, Rais alisisitiza mabadiliko ya haraka na makubwa katika sekta hii. Ushirikiano huu kati ya Serikali na sekta binafsi ni kielelezo cha utekelezaji wa maono hayo,” amesema.
Amesema NMB ilianza kwa udhamini wa Sh30 milioni kwa mwaka katika maonyesho yaliyopita, lakini sasa imeongeza nguvu kwa dau la Sh300 milioni, ishara ya dhamira ya dhati katika kukuza sekta hiyo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Kilimo Biashara wa NMB, Nsolo Mlozi, amesema benki hiyo imeamua kuwekeza kimkakati baada ya kushuhudia mafanikio ya maonyesho ya miaka ya 2024 na 2025.
“Mkataba huu ni uwekezaji wa kimkakati unaolenga kuboresha maisha ya Watanzania wanaojishughulisha na mnyororo wa thamani wa kilimo, ikiwemo ufugaji na uvuvi.
“Hadi mwaka 2025, NMB ilikopesha zaidi ya Sh100 bilioni kwenye sekta hii,” amesema, akisisitiza maonyesho hayo ni jukwaa muhimu la kuwakutanisha wafugaji, wawekezaji, wataalamu na taasisi za kifedha.
Amesema maonyesho hayo yatatoa fursa za elimu ya ufugaji bora, bima ya mifugo, mikopo na upatikanaji wa masoko ya kitaifa na kimataifa.
“Tukiwa wadhamini wakuu, tunawaahidi wateja wetu kwamba tutarahisisha upatikanaji wa mikopo kwa washiriki wa maonyesho haya. Mfugaji ajikite kwenye uzalishaji, masuala ya fedha na bima atuachie sisi,” amesema Mlozi.
Amesema kupitia huduma ya matawi yanayotembea, benki hiyo itahakikisha washiriki na wanunuzi wanapata huduma zote za kifedha papo hapo wakati wa maonyesho na minada mingine ya mifugo nchini.
Mkurugenzi wa Mbogo Ranches, Naweed Bulla, amesema lengo la Tri-Nations Livestock Expo ni kujenga mfumo imara wa biashara ya mifugo unaovuka mipaka ya nchi.
“Tunataka kuona wafugaji wa Tanzania wakifanya biashara Kenya na Namibia kwa urahisi. Mwaka huu tunaanza na nchi tatu, lakini mwakani tunapanua wigo kwa kushirikisha pia Zimbabwe, Botswana na Zambia,” amesema.
Amesema maonyesho hayo yataanza rasmi Juni 19 kwa ufunguzi wa viongozi wa kitaifa na kikanda, Juni 20 kutakuwa na semina maalumu za mafunzo kwa wafugaji kuhusu kanuni za ufugaji bora, elimu ya fedha na bima, huku Juni 21 ikiwa ni siku ya mnada wa mifugo na burudani mbalimbali.
Katika ubunifu mpya, maonyesho ya mwaka huu pia yatawahusisha wafugaji wa kuku na kuanzisha shindano la ‘Queen of Agriculture’ kwa mara ya kwanza, hatua inayolenga kuvutia vijana na wanawake zaidi katika sekta hiyo.