Lissu alivyombana shahidi fiche wa Jamhuri, akana kutishiwa maisha

Dar es Salaam. Shahidi wa tano wa Jamhuri katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amesema hajawahi kutoa taarifa polisi kuhusu kutishiwa maisha, wala hajawahi kupokea vitisho vyovyote vinavyohusiana na ushahidi wake.

Shahidi huyo ni mmoja wa mashahidi fiche wa Jamhuri waliowekewa ulinzi wa Mahakama na wasiopaswa kuonekana au kutambulika hadharani.

Hutoa ushahidi wakiwa ndani ya kizimba maalumu ambamo hawaonekani kwa wasikilizaji wala kwa mshtakiwa, isipokuwa kwa majaji pekee.

Akitambulishwa kwa jina la P6 (24), shahidi huyo alikana kutishiwa maisha wakati wa maswali ya dodoso yaliyoulizwa na mshtakiwa Lissu, anayejiwakilisha mwenyewe katika kesi hiyo.

Awali, upande wa Jamhuri uliomba mashahidi raia kupewa ulinzi kwa mujibu wa Kanuni za Ulinzi wa Mashahidi za mwaka 2025, zilizotungwa na Jaji Mkuu chini ya kifungu cha 194 cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA), ukieleza kuwa, mashahidi hao walikuwa wakitishiwa maisha.

Katika uamuzi uliotolewa Agosti 4, 2025 na Jaji Hussein Mtembwa, Mahakama ilielekeza kuwa majina ya mashahidi hao yasitajwe, pamoja na anuani zao au taarifa zozote zitakazoweza kuwatambulisha wao, familia zao au watu wao wa karibu.

Pia, ilizuia usambazaji wa maelezo au nyaraka zozote zinazowahusu bila idhini ya Mahakama na kuagiza watumie majina bandia wakati wote wa usikilizwaji wa kesi.

Kesi hiyo inasikilizwa katika Mahakama Kuu, Masjala Ndogo Dar es Salaam, mbele ya jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Iringa, Dunstan Ndunguru, akishirikiana na James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde. Hivi sasa shauri hilo liko katika hatua ya usikilizwaji wa ushahidi wa upande wa mashtaka.

Akitoa ushahidi wake leo Ijumaa Februari 13, 2026, shahidi huyo akiongozwa na Wakili wa Serikali, Cuthbert Mbilingi ameeleza kuwa, yeye ni mkazi wa Songea na hufanya kazi ya usafirishaji kwa kutumia bodaboda.

Amedai kuwa,  mwaka 2024 alianza kufuatilia siasa za Chadema kwa kuhudhuria mikutano mbalimbali na mwaka 2025 akaamua kueleza nia ya kujiunga rasmi na chama hicho.

Amedai kuwa,  alimfuata aliyekuwa Katibu wa Vijana wa Wilaya ya Songea na baadaye Mwenyekiti wa Vijana wa wilaya hiyo, Chiza (Esau), kumweleza dhamira yake ya kuwa mwanachama.

Amedai kuwa,  Chiza alimwahidi kumsaidia kupata kadi ya uanachama na baadaye akawa akimshirikisha katika shughuli mbalimbali za chama, ikiwamo kuandaa mikutano.

Shahidi huyo amedai kuwa, Aprili 4, 2025, akiwa anatumia simu yake, aliingia kwenye chaneli ya Jambo TV na kusikiliza hotuba ya Mwenyekiti wa Chadema akihutubia wafuasi.

Amedai kuwa, katika hotuba hiyo alimsikia Lissu akisema: “Bila mabadiliko hakuna uchaguzi, hivyo tunaenda kukinukisha, tunakwenda kuvuruga uchaguzi.”

Pia alimsikia akisema. “yeyote ambaye atataka kwenda na  sisi tutakwenda naye ambaye hatataka tutamuacha…”

Kama kuna mtu ambaye anatarajia kugombea udiwani, ubunge, asahau, hata mimi mwenyekiti kuhusu kugombea urais hilo sahau. Bila mabadiliko hakuna uchaguzi. Watasema tunafanya uasi, ni kweli utakuwa ni uasi bila mabadiliko hakuna uchaguzi.”

Amedai kuwa, maneno yake yalimwingia moyoni na yalimshawishi akatamani kuwa miongoni mwa watu ambao watashiriki ajenda ya kuzuia uchaguzi, bila mabadiliko, kwa kukinukisha, yaani kufanya vurugu au kuharibu uchaguzi.

Amedai kuwa, alimfuata mwenyekiti wa vijana, wakati huo Chiza aliyekuwa Songea, alimweleza nia yake ya kuwa miongoni mwa vijana watakaoshiriki kukinusha kabla ya mabadiliko ya uchaguzi.

Shahidi huyo alidai kuwa, Chiza alimsifia kwa uamuzi mzuri na wa kishujaa na akampongeza, akisema vijana kama yeye ndio vijana wanaotakiwa kulikomboa Taifa.

Amedai kuwa, alimuahidi kuwa chochote kitakachokuwa kinaendelea kuhusu harakati hizo za kukinukisha atamshirikisha kwenye kundi lililoitwa Siasa Yetu Update, lililojadili mipango ya kudai mabadiliko kabla ya uchaguzi.

Baada ya kuhitimisha ushahidi wake huo mkuu shahidi huyo, Lissu alimhoji maswali mbalimbali ya dodoso. Sehemu ya mahojiano hayo yalikuwa kama ifuatavyo:

Lissu: Shahidi sasa naomba unijibu maswali kama nitakavyokuuliza siyo kilichomo kichwani mwako, kama hujui unasema sijui siyo kupotezeana muda. Wewe ni mwanamume kwelikweli maana naweza kusema mwanamume kumbe ni dada, umenielewa?

Kisha Lissu alimuuliza kama aliandika maelezo polisi, akakubali.

Lissu akaomba aoneshwe nakala akasema kuwa ndio hayo.

Kisha Lissu akamuuliza kama anaweza kutoa mahakamani yawe kielelezo cha upande wa utetezi (mshtakiwa) na shahidi akakubali.

Baada ya upande wa mashtaka kueleza kuwa hauna pingamizi, Mahakama iliyapokea na kuwa kielelezo cha nne cha upande wa utetezi (D4).

Akitumia kielelezo hicho (maelezo ya mshtakiwa) anamuuliza baadhi ya maelezo aliyoyatoa katika ushahidi wake wa mdomo kizimbani ambayo hayamo katika maelezo yake aliyoyaandika Polisi na kumuuliza kama kweli yamo au hayamo katika maelezo hayo ya polisi na shahidi huyo akakiri kuwa hayakuwemo.

Baadhi ya maelezo ambayo shahidi huyo ameyatamka kizimbani, lakini hayamo katika maelezo yake aliyoyaandika polisi ni pamoja na dini yake ni Mkristo.

Lissu amemtaka shahidi huyo asome maelezo yake aliyoyaandika polisi kwa mkono, sehemu iliyoandikwa dini yake shahidi; lakini akajibu hapasomeki, yamefutika, lakini Lissu akadai kuwa katika maelezo hayo yanaeleza yeye ni Muislamu.

Maelezo mengine ni yeye shahidi kuwa na simu aina ya Infinix Smart 8, aliyoitumia kuingia YouTube, na simu yake ilikuwa na bando, kuingia kwenye akaunti ya Jambo TV, maelezo yaliyomo katika hotuba yake (Lissu) kuhusu kuzuia uchaguzi.

Lissu: Kuna huyu mtu umemtaja kama Chiza, kuna mahali unasema alikuwa Katibu wa Vijana Wilaya ya Songea na mahali kwingine unamtaja kama Mwenyekiti wa Vijana Wilaya  ya Songea, sasa kipi ni kipi?

Shahidi: Alianza kuwa katibu kisha akawa mwenyekiti. Wakati ule 2024 alikuwa katibu na mwaka 2025 akawa mwenyekiti.

Lissu: Hebu ngoja nikusomee maelezo yako kuanzia mahali  ilikoandikwa kuwa ilipofika Januari 25, 2025 nilimfuata Katibu wa Vijana Esau Chiza, kwa hiyo 2024 ni katibu na  Januari 2025 ni katibu.

Shahidi: Haya maelezo sikuandika mimi, nilikuwa nahojiwa na polisi ndio wanaandika.

Lissu: Kwa hiyo polisi ndio wamekuuza, pole sana.

Lissu: Baada ya kukutembeza kwenye maelezo yako ya polisi sasa naomba nikuulize maswali mengine. Hebu waeleze waheshimiwa majaji kama kiongozi wa chama kama mimi kuitisha mkutano ni kosa la jinai.

Lissu: Na waeleze waheshimiwa majaji kama kiongozi wa chama kama mimi kusema tutazuia uchaguzi ni kosa la jinai.

Lissu: Na waeleze waheshimiwa majaji kama unafahamu kuwa kuna sheria yoyote katika nchi hii; kusema tutazuia uchaguzi ni kosa.

Shahidi: Huko kwenye sheria mimi sifahamu.

Lissu: Kwani polisi waliokwambia uje useme hapa hawakukueleza kuwa ni kosa?

Lissu: Umeieleza Mahakama kuwa, Aprili 20, 2025  mlikamatwa eneo la DS Kitimoto kwa tuhuma za kupanga maandamano bila kibali, hayo mahojiano yako wapi?

Lissu: Uliwahi kushtakiwa kwa kosa la kupanga maandamano bila kulibali?

Lissu: Kwani hiyo kesi ya tuhuma za kupanga maandamano bila kibali iliishia wapi?

Shahidi: Sifahamu, alikuwa anaifuatilia ndugu yangu.

Lissu: Huyo ndugu yako ni mwanasheria?

Lissu: Hufahamu kwa sababu ni uwongo.

Lissu: Ilikuwaje mtuhumiwa wa kesi ya kupanga maandamano bila kibali ukawa shahidi kwenye kesi ya uhaini ya mwenyekiti wako, kilitokea nini hapo katikati?

Shahidi: Mimi sikumbuki kilitokea nini.

Lissu: Polisi walikwambia ukiwa shahidi kwenye kesi hii watakufutia kesi.

Lissu: Waeleze waheshimiwa majaji kama baada ya Aprili 25, 2025 umewahi kuandika maelezo mengine ya ziada.

Lissu: Waeleze waheshimiwa majaji kama umewahi kutoa taarifa polisi kuwa unatishiwa maisha.

Lissu: Waeleze waheshimiwa majaji kama baada ya Aprili 25, 2025 kuna mwanachama yeyote wa Chadema amewahi kukutishia maisha.

Lissu: Waeleze waheshimiwa majaji kama baada ya Aprili 25, 2025 kuna mwanachama yeyote wa Chadema amewahi kumtishia maisha ndugu yako yeyote.

Lissu anakabiliwa na shtaka moja la uhaini kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, linalotokana na maneno aliyoyatamka kuhusu kusudio la kuzuia kufanyika uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Anadaiwa kuwa, Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania, kwa nia ya uchochezi alishawishi umma kuzuia kufanyia kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Kesi hiyo itandelea Jumatatu.