Dar es Salaam. Wakati uongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ukiwaelekeza viongozi wake wa ngazi za chini nchi nzima kuanza kutumia ofisi na mali za chama, mawakili wa walalamikaji katika kesi ya mgawanyo wa rasilimali za chama wamesema hatua hiyo ni upotoshaji na kudharau Mahakama.
Chadema kinakabiliwa na kesi ya madai inayohusiana na mgogoro wa madai ya mgawanyo wa rasilimali za chama usio sawa kati ya Bara na Zanzibar iliyofunguliwa na baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Wadhamini kutoka Zanzibar.
Kesi hiyo ya madai namba 8323 ya mwaka 2025 ilifunguliwa na Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema, Said Issa Mohamed na wajumbe wawili wa Bodi ya Wadhamini wa Chadema kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu.
Walalamikiwa katika shauri hilo ni Bodi ya Wadhamini Waliosajiliwa wa Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.
Hivi karibuni, viongozi wa Chadema wametoa maelekezo kwa viongozi wa ngazi za chini wakiwaelekeza kuanza kutumia ofisi na mali za chama hicho kwani zuio lililokuwa limewekwa limekwisha muda wake.
Januari 23, 2026, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Dk Rugemeleza Nshala, katika taarifa yake kwa umma, alisema Chadema ni chama kilichosajiliwa kihalali nchini chenye haki ya kufanya shughuli zake za kisiasa nchini kote, Jeshi la Polisi lazima lifahamu haliko juu ya sheria na halina mamlaka ya kusimamisha au kupoka haki za vyama vya siasa.
Dk Nshala alisema hakuna zuio lolote la Mahakama Kuu juu ya kutenda shughuli za kisiasa kwani amri yake ya Juni 10, 2025 ilikoma Desemba10, 2025. Alisema viongozi, wanachama na wapenzi wa Chadema wana haki ya kukusanyika na kufanya shughuli za siasa na hawatakiwi kuzuiwa kufanya hivyo.
Juzi, Februari 11, 2026, wakati wa kesi ya mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, Naibu katibu Mkuu wa chama hicho, Amani Golugwa alisema viongozi wote wa chama nchi nzima wako huru kutumia ofisi za chama pamoja na mali zao.
Amesisitiza kwamba viongozi waende ofisini kufanya maandalizi ya usafi, nyaraka na mali zote tayari kuzitumia na kwamba watatoa maelekezo hivi karibuni vikao vianze kukaliwa kwenye ofisi zao za chama.
Wakizungumzia suala hilo leo Februari 13, 2026, wakili mwandamizi kutoka kampuni ya Hyperion Legal and Corporate Consultants, Shabaan Marijani amesema amri ya Mahakama inapotolewa inakuwa halali na kuzifunga pande zote husika mpaka amri hiyo itakapotenguliwa na Mahakama yenyewe.
Amesema tafsiri na hoja zilizowasilishwa na wanasheria wa chama na kurudiwa na baadhi ya viongozi wa juu si sahihi, na ama kwa makusudi au vinginevyo yanaelekeza, kuhamasisha na kuchochea upotoshaji umma na kuvunja au/na kudharau amri halali za Mahakama.
“Tunapenda pia kuelimisha umma kuwakumbusha wanasheria na viongozi wa Chadema kuwa; zuio lilitolewa chini ya amri ya hiyo hiyo ya 37 lakini chini ya Kanuni 1(a) na 1(b) ya Sheria ya Mwenendo wa Madai Sura 33 inayobainisha kwamba zuio linalotolewa chini ya Kanuni hii linadumu hadi kesi ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi,” amesema.
Kuhusu hoja ya Dk Nshala kwamba waleta maombi hawakuomba nyongeza ya muda si sahihi kwa kuwa amri yenyewe imejitosheleza kuhusu mipaka au ukomo wa zuio; hivyo wanaona imekua ni hoja iliyopitwa na wakati na jambo lilisilokuwa na manufaa.
“Ni mtazamo wetu kwamba, matamko ya Chadema kama yalivyotolewa na viongozi wa juu wa chama, yapo kinyume na sheria, na yametizamiwa kuhamasisha kuvunja na kudharau amri za mahakama, ikiwa ni mkakati wa kupima uwezo wa vyombo vya dola katika kutimiza utawala wa sheria na utekelezaji wa amri halali za mahakama,” amesema.