Dodoma. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, leo Ijumaa Februari 13, 2026, amefanya mazungumzo na Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda, nyumbani kwake jijini Dodoma, kwa lengo la kubadilishana uzoefu na kupata ushauri kuhusu ujenzi na uimarishaji wa uhusiano katika jamii.
Mazungumzo hayo yamekuja kufuatia kuanzishwa kwa Kitengo cha Uhusiano na Rais, Samia Suluhu Hassan, kinacholenga kuimarisha mshikamano wa kitaifa na kuweka mwelekeo mmoja katika sekta za kidini, kiraia na nyinginezo.
Akizungumza baada ya kikao hicho leo, Sangu amesema tayari wizara yake imeanza mchakato wa kukutana na viongozi wa dini mbalimbali wakiwamo wa The Council of Pentecostal Churches of Tanzania (CPCT), Baraza la Waislam Tanzania (Bakwata) pamoja na Kanisa la Waadventista wa Sabato, kwa lengo la kujenga maelewano na kuimarisha ushirikiano.
Sangu amempongeza Pinda kwa mchango wake katika kuasisiwa kwa Kamati ya Kitaifa ya Maridhiano na Amani ya Viongozi wa Dini, akieleza kuwa uzoefu wake katika kushughulikia masuala ya migogoro ya kijamii ni hazina muhimu kwa maendeleo ya sekta ya mahusiano nchini.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Deus Sangu, amefanya mazungumzo na Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda, nyumbani kwake jijini Dodoma leo Ijumaa Februari 13, 2026
Kwa upande wake, Pinda amesema mahusiano ni mchakato unaohitaji kujengwa kwa misingi ya mazungumzo ya wazi na uelewano wa dhati. Amesisitiza umuhimu wa jamii kuwa na kauli na mwelekeo mmoja ili kudumisha amani, umoja na mshikamano wa Taifa.
Aidha, amempongeza Sangu kwa kuaminiwa na Rais Samia kusimamia Sekta ya Mahusiano na kumtaka kuendeleza ushirikiano mzuri na wananchi pamoja na wadau wote wa maendeleo.
“Mahusiano ni msingi muhimu katika ujenzi wa maendeleo ya Taifa letu,” amesisitiza Pinda.