Zanzibar iko tayari kuikaribisha Yanga New Amaan Complex

Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF) limekamilisha maandalizi yote ya kuikaribisha timu ya Yanga SC katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, wakati itakapocheza mechi yake ya mwisho ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya JS Kabylie, Jumapili, Februari 15, 2026.

Yanga inaingia katika mchezo huo ikiwa inahitaji kufunga mabao zaidi ya moja ili kuongeza nafasi ya kufuzu hatua inayofuata. Mbali na kushinda, timu hiyo pia inasubiri matokeo ya mechi nyingine ya Kundi D kati ya AS FAR Rabat na Al Ahly, ambapo AS FAR wanahitaji sare tu kufuzu moja kwa moja.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari wa ZFF, Mohamed Kabwanga, amesema Zanzibar kama wenyeji wako tayari kwa asilimia 100 kuhakikisha kila kitu kinakwenda kwa usahihi.

“Yanga ni wageni lakini ukija hapa sisi ndio wenyeji na tumejiandaa kikamilifu. Kama Shirikisho, tupo tayari kuwapa ushirikiano mkubwa. Tunafahamu ni mechi kubwa barani Afrika na jukumu letu ni kuhakikisha kile wanachokusudia kupata ushindi kinatimia,” amesema Kabwanga.

Ameongeza kuwa maandalizi hayahusishi tu usalama, bali pia kuhakikisha miundombinu ya uwanja na huduma zote muhimu ziko katika kiwango cha hali ya juu. “Uwanja kama unavyouona, kijani kimekolea na kipo tayari kwa mechi. Tunaamini kila kilichopangwa kitaenda sawa.”

Mbali na maandalizi ya mechi hiyo, ZFF imejivunia mafanikio ya Uwanja wa New Amaan Complex msimu huu, uliotumika na klabu tatu za Tanzania Bara, Singida United, Yanga na Azam FC katika mashindano ya kimataifa.

“Tumeandika historia kubwa msimu huu kwa New Amaan kutumika na timu tatu. Tunajivunia hilo, na timu zote zilizotumia uwanja huu zimefanikiwa kupata matokeo mazuri. Hakika tutaukumbuka mwaka huu,” amesema Kabwanga.