KAMATI YA MIUNDOMBINU YASISITIZA UBIA KATI YA SERIKALI NA SEKTA BINAFSI UJENZI WA BARABARA

:::::::::::::::

Kamati ya Kudumu ya Bunge ye Miundombinu imeitaka Wizara ya Ujenzi kuharakisha utekelezaji wa mipango ya ushirikishaji wa ubia kati ya Sekta binafsi na Serikali (PPP) katika miundombinu ya ujenzi wa barabara nchini ili kurahisisha huduma za usafirishaji na usafirishaji. 

Kamati imesisitiza umuhimu wa kufanya haraka utekelezaji huo ili iende sambamba na maboresho yaliyofanywa na Serikali katika miundombinu ya Bandari nchini ambapo hivi sasa shehena za mizigo imeongezeka kuliko awali na hivyo kusababisha wasafirishaji kutumia muda mrefu katika barabara zilizopo.

Hayo yameelezwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Abubakar Assenga Bungeni jijini Dodoma wakati wa mafunzo wa uelewa wa mchango wa Sekta ya Ujenzi kwa maendeleo ya Uchumi na ustawi wa maisha ya wananchi kwa wabunge hao uliotolewa na Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC).

“Harakisheni mchakato wa ubia wa kujenga na kupanua barabara zenu ikiwemo barabara kuu ya kutoka Dar es Salaam – Morogoro ambapo wasafirishaji wanakumbana na foleni na hivyo kuwa kero kwao”, amesema Makamu Mwenyekiti.

Aidaha, Assenga ametaka Baraza hilo kuhakikisha wanakamilisha Sheria ya majengo nchini ili kuondokana na ujenzi holela usiofuata tarabu na viwango kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega amesema kuwa Sekta ya Ujenzi ni Sekta ya Pili kwa mchango mkubwa wa kiuchimi nchini hali inayofanya mtandao wa barabara zinazosimamiwa na Wakala wa Barabara (TANROADS) kuwa na thamani inayokadiriwa kufikia Shilingi Trilioni 34.  

Awali wakati akitoa mafunzo hayo kwa wabunge hao, Mtendaji Mkuu wa Baraza la Taifa la Ujenzi (NCC) Dkt. Matiko Nturi ameeleza kuwa Sekta ya Ujenzi ni Sekta Wezeshi kwa Sekta nyingine za kiuchumi na kijamii kwa ajili ya uzalishaji, utoaji ajira, kuchangia pato la Taifa na kukuza maarifa ya ujuzi na Teknolojia.