SERIKALI, COSTECH NA CRDB WATENGA BILIONI 4.6 KUWAINUA VIJANA WABUNIFU

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidhi Ameir,

 ::::::::::::::::

 Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa kushirikiana na Benki ya CRDB, imetenga Shilingi bilioni 4.6 kuwawezesha mitaji vijana wabunifu walio tayari kupeleka bidhaa na huduma zao sokoni.

Fedha hizo zinatolewa kupitia Mfuko wa Samia wa Ubiasharishaji Ubunifu uliozinduliwa mwaka 2024, ukiwa na lengo la kubadili mawazo bunifu kuwa biashara zenye tija.

Akizungumza Februari 13, 2026 jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidhi Ameir, amesema Serikali imeielekeza COSTECH kuhakikisha vijana wanapata mitaji ya kukabiliana na ushindani wa soko.

Amesema mfuko huo uko wazi kwa Watanzania wote wenye bunifu zilizo tayari kuingia sokoni lakini wanakosa mtaji.

“Wizara ilitenga Sh. bilioni 2.3 kwa mikopo nafuu kupitia Mfuko wa Samia wa Ubiasharishaji Ubunifu. Kutokana na wingi wa wabunifu, Serikali iliingia makubaliano na Benki ya CRDB iliyochangia Sh. bilioni 2.3, hivyo kufanya mtaji kufikia Sh. bilioni 4.6,” amesema.

Kwa mujibu wa takwimu, wabunifu 3,300 tayari wametambuliwa nchini, huku 300 wakiendelezwa kupitia Mfuko wa Taifa wa Uendelezaji Sayansi na Teknolojia (MTUSATE) unaosimamiwa na COSTECH.

Hata hivyo, Naibu Waziri huyo ameonesha kusikitishwa na kasi ndogo ya uchukuaji wa mikopo hiyo.

Amesema katika miezi 10, vijana saba pekee ndio wamenufaika na kiasi cha Sh. milioni 767 kimetumika kati ya bilioni 4.6 zilizotengwa.

Ametoa wito kwa vijana wenye bunifu kuwasilisha maombi kupitia COSTECH ili kunufaika na fedha hizo, akisema mitaji hiyo itasaidia kuanzisha biashara, kutoa ajira na kukuza uchumi.

Katika hafla hiyo, baadhi ya wanufaika walitambuliwa akiwemo kijana Paul Kitema aliyebuni teknolojia ya utambuzi wa thamani ya asali na mazao ya nyuki, na kufanikiwa kusafirisha nje zaidi ya tani 60 za asali na nta, zilizoingiza zaidi ya Sh. milioni 200 za fedha za kigeni.

George Buchafwe pia ametajwa kwa kuanzisha vituo viwili vya kuchakata chikichi katika Halmashauri za Mlimba mkoani Morogoro na Kibiti mkoani Pwani.

Meneja wa Mfuko wa Uendelezaji Sayansi na Teknolojia, Dkt. Beatrice Lyimo, amesema jukumu la mfuko huo ni kubadili mawazo bunifu kuwa suluhisho la changamoto za jamii kupitia uwezeshaji wa kifedha.

Mkurugenzi wa CRDB Foundation, Tully Esther Mwambapa, amesema changamoto kubwa kwa vijana imekuwa mitaji, akimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha mfuko huo kwa wakati sahihi.

Amesema katika awamu ya kwanza maombi 152 yalipokelewa, 22 yakatimiza vigezo na saba kuchaguliwa na kupatiwa Sh. milioni 667 kulingana na mahitaji ya miradi yao, huku 15 wakiingizwa kwenye mpango wa kujengewa uwezo.


Kwa upande wake, Profesa John Kondoro, Mwenyekiti wa Tume ya COSTECH, amesema ipo haja ya kuongeza hamasa ili vijana wengi zaidi wachangamkie fursa hizo.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt. Amos Nungu, amesema mfuko huo umeanzishwa baada ya utafiti kuonesha kuwa Tanzania ina hazina kubwa ya bunifu, lakini wabunifu wengi hukwama kutokana na ukosefu wa mitaji na uelewa wa kibiashara.

Amesema hadi sasa bunifu 300 zimepita katika mfuko huo na zinaendelea kuunganishwa na wadau ili kuhakikisha zinakuwa endelevu na zenye tija kwa taifa.