Serikali yatoa vitabu vya mkondo wa amali

Dar es Salaam. Serikali imetoa vitabu vya 18,354 masomo ya elimu ya amali  kwa shule zote za sekondari za umma na binafsi nchini, hatua inayolenga kuongeza ufanisi katika ufundishaji na ujifunzaji sambamba na kuwawezesha wanafunzi kujipatia ujuzi utakaowasaidia kujiajiri au kuajiriwa baada ya kuhitimu masomo yao.

Akizungumza leo Februari 13, 2026 wakati wa hafla ya ugawaji wa vitabu hivyo kwa wakuu wa shule Tanzania Bara, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dk Aneth Komba amesema hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mtalaa ulioboreshwa ulioanza mwaka 2024.

Amesema mtalaa huo umegawanyika katika mikondo miwili ambayo ni mkondo wa amali na mkondo wa jumla, huku mkondo wa amali ukiwa na lengo la kujenga ujuzi wa vitendo kwa mwanafunzi ili kumwandaa kukabiliana na soko la ajira.

“Serikali imedhamiria kuhakikisha mwanafunzi hapati tu maarifa ya darasani, bali pia anapata ujuzi wa moja kwa moja unaomwezesha kujitegemea,” amesema Dk Komba.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Dk Aneth Komba akizungumza na wakuu wa shule wakati wa kukabidhi vitabu vya mkondo wa amali kwa shule za sekondari.



Mbali na ugawaji wa vitabu, Dk Komba amesema TET pia imetoa mafunzo kwa wakuu wa shule kuhusu maboresho ya mtalaa, hususan katika mkondo wa amali, pamoja na matumizi ya maktaba mtandao ambako vitabu vyote vinapatikana kwa njia ya kidijitali.

Meneja Uchapaji na Usambazaji wa Vitabu wa TET, Emmanuel Stanslaus, amewataka walimu kutumia vitabu hivyo kwa umakini na kwa kuzingatia miongozo iliyotolewa ili kuhakikisha vinatoa matokeo chanya kwa wanafunzi kulingana na fani wanazosoma.

“Vitabu hivi ni nyenzo muhimu. Ni wajibu wa walimu kuhakikisha vinatumika ipasavyo ili kuongeza tija katika ujifunzaji,” amesema.

Mkuu wa Shule ya Ufundi Nzega na Makamu Mwenyekiti wa Wakuu wa Shule Tanzania Bara, Mwanakombo Martin, amesema upatikanaji wa vitabu hivyo bila malipo utapunguza changamoto ya uhaba wa vitabu na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa mtalaa ulioboreshwa.

Amesema hatua hiyo pia itaweka usawa kati ya shule za Serikali na binafsi katika utoaji wa elimu ya amali.

Baadhi ya wakuu wa shule walioshiriki halfa ya kupokea vitabu vya amali vilivyotolewa na Taasisi ya Elimu Tanzania (TET).



Mkuu wa Shule ya Ufundi ya Wavulana Bwiru mkoani Mwanza, Thomas Werema, amesema Elimu ya Amali inaelekea kuwa mkombozi kwa vijana wengi nchini kwa kuwa inawapa uwezo wa kujiajiri, kuajiriwa au hata kuanzisha ajira kwa wengine.

“Bila vitabu na walimu waliopata mafunzo, mtalaa bora hauwezi kuleta matokeo yaliyokusudiwa. Huu ni mwanzo mzuri, kinachofuata ni ufuatiliaji wa utekelezaji wake,” amesema.