Dar es Salaam. Vijana wabunifu nchini wametakiwa kujitokeza na kuchangamkia fursa za mitaji na mafunzo zinazotolewa ili waweze kugeuza mawazo yao kuwa biashara endelevu na chanzo cha ajira.
Wito huo umetolewa leo Februari 13, 2026 jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh wakati wa hafla ya kuwatambua wanufaika kupitia mfuko wa Samia wa Ubisharaishaji Ubunifu.
Mfuko huo unaoratibiwa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kupitia Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech) kwa kushirikiana na Benki ya CRDB.
Akizungumza katika hafla hiyo, Wanu amesema Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ilitenga Sh2.3 bilioni kupitia Mfuko wa Samia wa Ubiasharishaji Ubunifu kwa ajili ya kutoa mitaji wezeshi kwa njia ya mikopo nafuu kwa wabunifu wanaofika hatua ya kupeleka sokoni bidhaa au huduma zitokanazo na ubunifu wao.
Amesema baadaye Benki ya CRDB iliwekeza Sh2.3 bilioni katika mfuko huo na kufanya mtaji wa kuwezesha wabunifu kuwa na jumla ya Sh4.6 bilioni.
Hata hivyo, amesema licha ya uwekezaji huo muamko wa vijana kuomba mikopo hiyo hairidhishi.
“Nimesikitishwa na kasi ya uchukuaji wa mikopo hii, katika kipindi cha miezi 10, vijana saba tu ndio wamenufaika na mfuko wa huu wa Samia.
“Hadi sasa ni Sh767 milioni tu zimechukuliwa kati ya Sh4.3 bilioni. Tuna wabunifu wengi, mategemeo yangu ilikuwa pesa zote hizi ziwe zimechukuliwa ndani ya mwaka mmoja,” amesema.
Amesema katika taarifa zote wa watendaji wakuu wa Costech na wa Benki ya CRDB, zimeainisha changamoto kadhaa za utekelezaji wa mpango huo ikiwamo kukosa taarifa sahihi, au bidhaa na huduma zao kukosa sifa mahsusi za kibiashara ili waweze kufanya marejesho.
“Nimefarijika, kwamba mmeanza kufanyia kazi hizi changamoto, hasa kwa kuandaa mafunzo kwa wabunifu ili kuwapa nyenzo na uwezo wa kufikia pesa hizi, kama kuna changamoto za kimfumo, tafuteni ufumbuzi wa haraka ili kuongeza wigo na tija kwa wabunifu wetu,” amesema.
Awali, Wanu amewapongeza wabunifu waliojitokeza kuchangamkia fursa hiyo iliyowawezesha kuendeleza bunifu zao.
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa Costech, Dk Amos Nungu amesema kwa awamu ya kwanza walipokea maombi ya vijana zaidi ya 200 lakini changamoto imekuwa ni ubora na ukamilifu wa nyaraka zinazowasilishwa na waombaji.
Amesema hilo limesababisha wengi kushindwa kufikia hatua ya mwisho ya kupata mkopo.
Amesema kati ya waombaji waliofanikiwa kuvuka hatua za awali, wachache ndio waliokidhi kikamilifu vigezo vya kitaalamu na kibiashara na hivyo kupendekezwa kupata ufadhili.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa lengo la mfuko huo si kugawa fedha tu, bali kuhakikisha fedha zinakwenda kwa wabunifu wenye miradi imara itakayochochea ukuaji wa uchumi na ajira.
Ameongeza kuwa, Costech itaendelea kutoa elimu kwa vijana kuhusu namna sahihi ya kuandaa maandiko ya miradi, kujaza fomu kwa usahihi na kuzingatia vigezo vinavyotangazwa ili kuongeza idadi ya wanaonufaika.
Awali, Tully Ester Mwambapa, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, amesema licha ya vijana wengi kuwa na mawazo makubwa na ubunifu wa hali ya juu, changamoto kubwa imekuwa ni ukosefu wa mitaji ya kuanzisha na kuendeleza miradi yao.
“Wazo bila mtaji linabaki kuwa ndoto. Ubunifu bila uwekezaji hauwezi kuzaa matunda. Ndiyo maana tunaunga mkono juhudi za Serikali za kuweka mifumo madhubuti ya kuwasaidia vijana,” amesema.