Tanga/Dar. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, amemuagiza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kuhakikisha ifikapo mwisho wa mwezi huu, fedha za ujenzi wa madarasa katika Shule ya Msingi Imani, Mkata Magharibi, ziwe zimefika.
Ametoa agizo hilo leo Ijumaa, Februari 13, 2026, akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Tanga alikoweka jiwe la msingi na kukagua kituo cha kupoza umeme cha Mkata.
Awali, Mwenyekiti wa Kijiji cha Mkata Magharibi, Mussa Ngana, aliwasilisha ombi la kusaidiwa kutokana na uchakavu wa madarasa matatu ya shule hiyo, ambayo kwa sasa hayatumiki.
“Muandikie kabisa katibu mkuu kwamba mwisho wa mwezi fedha iwe imefika. Mkurugenzi anasikia na mkuu wa mkoa pia. Fedha itoke popote pale, wakate safari na matumizi yasiyo ya lazima, kila mtu anywe chai nyumbani kwake, fedha hiyo ije tutengeneze kizazi cha kesho hapa,” amesema Dk Mwigulu.
Kwa mujibu wa Ngana, Shule ya Msingi Imani ina zaidi ya wanafunzi 1,000, lakini inatumia madarasa manne pekee, huku matatu yakiwa yamezuiwa kutumika baada ya mhandisi kubaini yamechakaa. Pia, nyumba ya mwalimu haifai kutumika kutokana na hali yake.
“Nimechoka kujibu hoja za wananchi kwa sababu ya kikomo cha mamlaka yangu. Ziara yako itakuwa msaada mkubwa katika kutatua changamoto hii,” amesema Ngana.
Akijibu hoja hiyo, Waziri wa Tamisemi, Profesa Riziki Shemdoe, amesema ameshamuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Handeni Vijijini kupeleka Sh50 milioni kwa ajili ya ujenzi wa madarasa mawili katika shule hiyo.
Aidha, amesema amemuelekeza Katibu Mkuu wa wizara hiyo kupeleka Sh50 milioni nyingine ili kuongeza madarasa mawili zaidi.
“Miaka miwili iliyopita tulitoa fedha zilizokamilisha ujenzi wa shule mpya ya Julius Nyerere yenye madarasa 14. Tayari wanafunzi 670 wanasoma katika shule hiyo,” amesema Profesa Shemdoe.
Hata hivyo, ripoti za ukaguzi na taarifa za mamlaka za Serikali zinaonesha kuwa changamoto ya miundombinu katika shule za umma nchini bado ni kubwa, hususan katika maeneo ya vijijini.
Shule nyingi za msingi na sekondari zinakabiliwa na uchakavu wa madarasa, vyoo na nyumba za walimu, huku ongezeko la wanafunzi likizidi kasi ya ujenzi wa miundombinu.
Hali hiyo imekuwa ikisababisha msongamano darasani na uhaba wa huduma muhimu, zikiwamo za vyoo na makazi ya walimu.
Wadau wa elimu waliozungumza na Mwananchi wamesema licha ya jitihada zinazofanywa na Serikali, bado kuna uhitaji mkubwa wa uwekezaji katika miundombinu ya elimu, ili kuboresha mazingira ya ujifunzaji na kuongeza ubora wa elimu nchini.
Ili kukabiliana na changamoto hiyo, wanasema Serikali inapaswa kuongeza bajeti ya maendeleo katika sekta ya elimu, kuboresha mifumo ya manunuzi na usimamizi wa miradi, pamoja na kuhakikisha uwazi katika matumizi ya fedha za umma.
Dk Wilberforce Meena amesema kilichofanywa na kiongozi huyo ni mwendelezo wa vitendo vinavyofanywa na wanasiasa wanapokwenda kwa wananchi.
Amesema Serikali ina mfumo wa utendaji kazi unaohusisha mipango na upangaji wa bajeti kuhusu shughuli husika, hivyo kwa kiongozi kuelekeza wizara itekeleze ujenzi ndani ya wiki mbili inaonesha wazi ni siasa.
“Kuna tabia ya viongozi kutoa matamko ambayo wanaamini yataamsha shangwe kwa wananchi, lakini utekelezaji wake unakuwa mgumu. Unaposema wabane fedha zao hata za chai, je ni shule ngapi nchini zina hali kama ya shule hiyo? Vipi zote zikijitokeza kwa pamoja bado Tamisemi itakuwa na uwezo wa kuzijenga?” amehoji.
Hata hivyo, ameshauri Serikali iongeze bajeti ya ujenzi wa miundombinu ya shule na kusisitiza fedha zinazotengwa zitumike vizuri.
Kwa upande wake, mtaalamu wa sera za elimu, Joseph Mshana, amesema tatizo hilo lipo kwa muda mrefu na sasa linahitaji suluhisho la kimfumo badala ya uamuzi wa kushtukiza.
Amesema ili kuepuka kauli zinazoonekana za kisiasa, Serikali inapaswa kuweka wazi takwimu za mahitaji halisi ya miundombinu ya elimu nchini na kuainisha mpango wa utekelezaji kwa awamu.
“Ni kweli kuna shule nyingi zina hali mbaya ya madarasa, mabweni na vyoo, lakini suluhisho si kutoa maagizo ya ghafla, bali kuongeza mgawo wa bajeti kwa sekta ya elimu na kuhakikisha fedha hizo zinatumika kama ilivyokusudiwa,” amesema.
Naye Mwalimu Mkuu mstaafu, Peter Luhanga, amesema mara nyingi viongozi wanapofika shuleni hukutana na uhalisia unaogusa hisia, lakini utekelezaji wa uamuzi huo unapaswa kuongozwa na taratibu za utawala wa umma.
Amesema hoja ya msingi si muda uliotajwa na kiongozi, bali ni namna ya kujenga mfumo imara wa kushughulikia changamoto za miundombinu.
Aidha, ameitaka Serikali kuimarisha ushirikiano kati ya Tamisemi na halmashauri ili miradi ya ujenzi na ukarabati wa shule iwe na uratibu mzuri bila kuathiri mipango mingine ya maendeleo.
Agizo la kukatwa mishahara
Katika hatua nyingine, Dk Mwigulu, ameagiza baadhi ya watumishi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kukatwa fedha kwenye mishahara yao ili kufidia hasara iliyotokana na mifuko 1,262 ya saruji kuganda katika mradi wa ujenzi wa Chuo cha Veta wilayani Handeni.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, watumishi hao ni wale waliokuwa na jukumu la kusimamia ujenzi wa chuo hicho.
“Wananchi wa Handeni wanasubiri Veta. Waliotakiwa kujenga wameiacha saruji ikaganda na kila siku wako ofisini, kila mwezi wanalipwa mishahara kwa kodi za wananchi wanaosubiri jengo,” amesema.
Amesema uzembe wa aina hiyo hauwezi kuvumiliwa, akieleza kuwa awali alidhani tatizo hilo linawahusu watumishi wa halmashauri, lakini baadaye alibaini kuwa usimamizi ulikuwa unafanywa kutoka wizarani.
Aidha, amemuagiza Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia kuchukulia hatua watumishi wote waliohusika na uzembe huo.
“Hii saruji iliyoganda wasimsumbue Rais Samia Suluhu Hassan kutafuta fedha. Wakatwe kwenye mishahara yao ili saruji irudishwe hapa,” amesema Dk Mwigulu.
Amesisitiza kuwa fedha za umma zinatokana na kodi za wananchi wanaojinyima ili miradi ya maendeleo ikamilike, hivyo uzembe unaosababisha upotevu wa rasilimali haukubaliki. Pia ameagiza apewe orodha ya watumishi wote waliohusika.
Takukuru kuchunguza jengo la mama na mtoto
Wakati huohuo, Waziri Mkuu ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchunguza ujenzi wa jengo la mama na mtoto katika kituo cha afya Sindeni wilayani Handeni, linalodaiwa kujengwa chini ya viwango.
Amesema miongoni mwa kasoro zilizobainika ni uwekaji wa milango 34 isiyokidhi viwango vinavyotakiwa.
“Katika ujenzi ule, milango 34 ipo chini ya viwango. Haya ni mazoea ya kubandika vitu na kuondoka,” amesema.
Amesema amepokea taarifa zinazoonesha kuwepo kwa matatizo katika utekelezaji wa baadhi ya miradi Handeni, hivyo ameitaka Takukuru kufanya uchunguzi na kuchukua hatua za kisheria kwa wote watakaobainika kuhusika.
“Kama mtagundua milango iliwekwa chini ya kiwango kwa lengo la kuiba fedha, hatua zichukuliwe. Haiwezekani Sh300 milioni zikatoka halafu wakaweka milango isiyokidhi viwango,” amesema huku akimtaka Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batlida Burian, kufuatilia kwa karibu.
Wito wa amani, uzalishaji wenye tija
Pia, Dk Mwigulu amewaomba wananchi kudumisha udugu na maelewano, akisisitiza kuwa makosa ya mtu mmoja yasichukuliwe kama ya jamii nzima.
“Akifanya kosa mtu, tushughulike naye binafsi. Mkulima asimuone mfugaji kuwa adui na mfugaji asimuone mkulima kuwa adui. Tusiruhusu ufa,” amesisitiza. Amesema kila Mtanzania ana haki ya kuishi popote nchini kwa kuzingatia sheria, huku akibainisha kuwa idadi ya watu inaongezeka wakati ardhi haiongezeki, hivyo kuna haja ya kubadili mtazamo na kuanza kuzalisha kwa tija hata katika maeneo madogo.
Miradi ya maendeleo na ajira
Akizungumzia utekelezaji wa miradi baada ya kupokea malalamiko ya wananchi na viongozi wakiwamo wabunge wa mkoa huo, Dk Mwigulu ameagiza ujenzi wa Shule ya Msingi Imani iliyopo Mkata kuanza mapema mwezi ujao.
Pia amewataka makandarasi wote nchini kuhakikisha miradi ya maji, umeme na mingine inatekelezwa kwa kuzingatia thamani ya fedha inayotolewa na Serikali.
“Hatuna mzaha katika kuona thamani ya fedha kwenye miradi. Fedha zinazotolewa zilingane na kazi inayofanyika,” ameagiza.
Amesema katika siku 100 za Rais Samia madarakani, ajira 7,000 za walimu na 5,000 za watumishi wa sekta ya afya zimetolewa, huku bima ya afya kwa wote ikianza kutekelezwa kwa makundi maalumu.
Katika ziara hiyo, Waziri Mkuu ameambatana na mawaziri, wabunge na viongozi wa kitaifa na mkoa wa Tanga.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amesema mradi mkubwa wa maji uliokuwa umesuasua kwa miaka mingi na unaotarajiwa kumaliza tatizo la maji mkoani Tanga umefikia asilimia 75 ya utekelezaji.
Kuhusu migogoro kati ya wakulima na wafugaji, mawaziri wa sekta za Kilimo, Mifugo na Tamisemi wamesema wanaendelea na mikakati ya pamoja ya kuimarisha maelewano.
Waziri wa Mifugo, Dk Bashiru Ally, amesema wataalamu wanaendelea na mazungumzo ya kutafuta suluhisho la dharura na la kudumu, akirejea agizo la Rais Samia la mkakati wa ‘tupendane’ unaolenga kuwaleta pamoja wakulima na wafugaji.
Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo, amewataka viongozi wa vijiji na kata kusimama imara kukabiliana na vitendo vya baadhi ya wafugaji wanaohamahama na kuvamia ardhi za wakulima, hali inayochochea migogoro.
Naye Waziri wa Tamisemi, Adolfu Ndunguru, ameahidi ujenzi wa madarasa manne katika Shule ya Msingi Imani, akieleza kuwa Sh50 milioni zitatolewa na Halmashauri ya Wilaya ya Handeni na Sh50 milioni nyingine kutoka Serikali Kuu ili kukamilisha madarasa hayo.