Dk Kijaji awatwisha mzigo Bodi TFS, ataka watalii milioni nane

Dodoma. Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wametekeleza uamuzi ya kamati ya mawaziri wanane kwa kutatua migogoro 423 kati ya 438 inayotajwa kuwa ni asilimia asilimia 96 ya migogoro iliyobainishwa.

Kauli hiyo imetolewa leo Ijumaa Februari 13,2026 na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji wakati wa kuzindua Bodi ya Ushauri ya TFS.

Amesema mamlaka hiyo kwa kushirikiana na taasisi zingine imetekeleza uamuzi ya kamati ya mawaziri wanane iliyoundwa kwa ajili ya kutatua migogoro inayokabili maeneo ya hifadhi yaliyovamiwa na kuanzishwa vijiji au makazi.

Bodi hiyo ya tano itaongozwa na Luteni mstaafu Chiku Gallawa aliyehudumu katika nafasi ya mkuu wa mkoa katika maeneo kadhaa nchini, mbali na maagizo mengine wametakiwa kuwa wabunifu ili kuongeza watalii kufikia  milioni nane.

Hata hivyo, Waziri Dk Kijaji amewatwisha mzigo bodi hiyo kuhakikisha wanawageuza mwelekeo wa sekta ya misitu na nyuki kwa kupunguza kasi ya uharibifu wa misitu na kuongeza mapato ya Taifa kupitia utalii lakini waone kuwa utendaji wao unaendana na kuzingatia kauli mbiu ya ’Kazi na Utu.’

Mawaziri wanane wa kisekta wakiongozwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, wakati huo William Lukuvi walifanya ziara ya mikoa 10 kutoa kuangalia na kutoa maelekezo juu utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi katika vijiji 975 nchini.

Dk Kijaji amesema baada ya utatuzi wa migogoro hiyo, maeneo yaliyobaki kama hifadhi yanapaswa kusimamiwa kikamilifu ili kuzuia uharibifu na uvamizi.

Waziri amesema utafiti unaonesha changamoto kwa kiwango kikubwa zinachangia upotevu wa rasilimali za misitu hekta 372,816 mwaka 2015 hadi hekta 469,420 mwaka 2017 sawa na ongezeko la asilimia 25.9 ya upotevu wa uoto wa ardhi yenye miti nchini.

Waziri ameonya juu ya uzembe wa kusubiri uvamizi ukue ndipo hatua zichukuliwe kwamba siyo sahihi badala yake TFS wanatakiwa kuwa walinzi kwa kuzuia siyo kulinda kwa kuharibu.

”Takwimu tulizonazo zinaonesha kuwa, rasilimali za misitu nchini zinakadiriwa kuwa takribani hekta milioni 48.1 sawa na asilimia 55 ya eneo lote la Tanzania Bara, kati ya eneo hilo, wakala unasimamia rasilimali za misitu zenye ukubwa wa eneo la takribani hekta milioni 12.5 ambazo ni sawa na asilimia 30 ya eneo lote la misitu nchini, kwa hiyo mnayo kazi.”

Amesema kuwa bodi hiyo haina budi kubuni mikakati itakayowezesha wakala kuongeza mashamba ya miti na kusimamia kikamilifu misitu iliyo chini yake ili kuwe na mikakati thabiti ya kukuza uchumi wa viwanda kupitia rasilimali za misitu na nyuki na kushirikiana na wananchi ikiwemo sekta binafsi.

Dk Kijaji aliitaka bodi hiyo kulisimamia na kushauri kwa umakini suala la nyuki kwa kuwa, eneo hilo likitumiwa vizuri wataongeza kipato kwa jamii zinazozunguka misitu na hivyo kupunguza utegemezi kwenye misitu ambao mara  nyingi unapelekea uharibifu.

Mwenyekiti wa bodi hiyo, Luteni mstaafu Gallawa amesema watatekeleza majukumu yao ka weledi na uzalendo lakini kwa kuzingatia ushirikishwaji wa wananchi katika maeneo yote.

Gallawa amesema ni wakati sasa kuwaona wananchi kama sehemu yao na wasiwe wapinzani kwani wakishirikishwa wanaweza kutoa matokeo chanya kwa wakati.

Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi Rasilimali Watu wa wizara hiyo, Bernard Marcelline amesema bodi hiyo yenye wajumbe saba, itahudumu hadi Desemba 4,2028.