Dar es Salaam. Wakati takwimu zikionesha asilimia 70 ya mapato ya kodi nchini kukusanywa katika Jiji la Dar es Salaam, utafiti mpya umeonya kuwa utegemezi mkubwa wa mkoa mmoja si endelevu na unaweza kuathiri azma ya Tanzania kufikia uchumi wa dola trilioni moja ifikapo mwaka 2050.
Utafiti huo unapendekeza kufanyika kwa mageuzi ya kina yatakayohamasisha urasimishaji wa biashara katika mikoa mingine ili kuongeza mchango wake kwenye mapato ya ndani ya Serikali.
Kwa mujibu wa wachambuzi, mikoa mingi ina fursa kubwa za kiuchumi ambazo bado hazijatumika ipasavyo, huku biashara nyingi zikiendelea kufanya kazi nje ya mfumo rasmi wa kodi.
Matokeo ya uchambuzi huo yamezinduliwa leo Ijumaa, Februari 13, 2026 katika kongamano la utafiti wa masuala ya kodi nchini, lililowakutanisha watunga sera, wasomi na wadau wa maendeleo kujadili uhamasishaji wa mapato ya ndani na vipaumbele vya mageuzi.
Utafiti huo umefanywa na Tanzania Investment and Consultant Group Limited (TICGL) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti, Sera na Uchumi (Repoa).
Ripoti imebainisha kuwa zaidi ya Sh20 trilioni za mapato ya kodi yanayoweza kukusanywa katika mikoa mingine hayakusanywi kikamilifu kila mwaka, hali inayozua maswali iwapo mfumo wa sasa wa kodi unaakisi kwa usahihi maeneo halisi ambako shughuli za kiuchumi zinafanyika.
Akiwasilisha matokeo muhimu ya utafiti, mtafiti wa TICGL, Amran Bhuzohera, amesema mfumo wa kodi nchini bado umejikita zaidi katika ukanda wa kati, hasa kutokana na kampuni nyingi kusajiliwa na kuwasilisha marejesho yao kupitia ofisi kuu zilizopo Dar es Salaam.
Amesema utafiti huo ulichambua mzunguko wa fedha, mienendo ya uzalishaji kikanda na takwimu za ukusanyaji kodi ili kubaini kama utendaji wa kodi unaendana na uhalisia wa shughuli za kiuchumi kote nchini.
“Ripoti inaonesha kuwa mikoa mingine ina uwezo mkubwa wa kuzalisha mapato ya kodi iwapo shughuli za sekta binafsi zitarasimishwa. Kwa sasa, biashara nyingi zinafanya kazi nje ya mfumo rasmi, hivyo sehemu kubwa ya mapato inapotea. Kuitegemea mkoa mmoja si endelevu, hasa tunapoelekea kwenye uchumi wa dola trilioni moja. Mageuzi yanahitajika kwa haraka,” amesema.
Ingawa ripoti inaonesha tofauti za kikanda, imebainisha kuwa utendaji wa jumla wa uchumi bado ni mzuri.
Pato la Taifa liliongezeka kutoka Sh189 trilioni hadi Sh235 trilioni mwaka 2025, huku ukuaji halisi wa uchumi ukifikia asilimia 6.0. Katika kipindi hicho, uwiano wa kodi kwa Pato la Taifa (tax-to-GDP ratio) uliongezeka kutoka asilimia 11.5 hadi 13.3.
Hata hivyo, watafiti wanasema takwimu hizo za jumla zinaficha changamoto za kimuundo katika usimamizi wa kodi.
Mapato yanayotokana na sekta ya madini katika Mwanza na Shinyanga, kilimo katika Mbeya, utalii katika Arusha, pamoja na biashara katika miji ya kati, mara nyingi huripotiwa na kutozwa kodi Dar es Salaam badala ya katika maeneo halisi ambako shughuli hizo zinafanyika.
Utafiti pia umeangazia ukubwa wa sekta isiyo rasmi, ambapo mwaka 2025, takribani asilimia 45 ya Pato la Taifa, sawa na Sh105.7 trilioni, ilitokana na shughuli zilizo nje ya mfumo rasmi.
Hali hiyo inakadiriwa kusababisha upungufu wa mapato ya kodi wa Sh14.1 trilioni kwa mwaka, sawa na karibu asilimia 45 ya mapato yote ya kodi.
Licha ya mageuzi ya kidijitali yaliyolenga kupanua wigo wa walipakodi, ni kati ya asilimia 5 hadi 7 tu ya miamala ya sekta isiyo rasmi inayokamatwa katika mfumo wa kodi kwa sasa.
Kwa mujibu wa ripoti, miamala ya fedha kwa njia ya simu ilifikia Sh223.4 trilioni mwaka 2025, karibu asilimia 95 ya Pato la Taifa la mwaka huo, ikiashiria kasi ya ukuaji wa shughuli za kifedha za kidijitali.
Hata hivyo, watafiti wanasema sehemu ndogo tu ya mtiririko huo wa fedha imeunganishwa ipasavyo katika mifumo ya usimamizi wa kodi.
Akizungumza katika kongamano hilo, Mtafiti Mkuu wa Repoa, Dk Jamal Msami, amesisitiza umuhimu wa kuendeleza mageuzi yatakayoimarisha usimamizi wa kodi, kuongeza usawa na kuimarisha utii wa walipakodi.
Naye mtafiti wa Repoa, Ahmed Amani, amehimiza nchi kuongeza uwiano wa kodi kwa Pato la Taifa kutoka kiwango cha sasa cha asilimia 13, akitaja Namibia na Mozambique kama mifano ya nchi za Afrika zilizofanikiwa kuongeza mapato ya ndani kupitia mageuzi endelevu ya mfumo wa kodi.