Dar es Salaam. Katika siasa za Tanzania, miongoni mwa majina yanayoibua hisia kali ni la John Heche, makamu mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Akiwa mmoja wa wanasiasa vijana waliokulia katika harakati za upinzani, safari yake imegubikwa na misukosuko, misimamo mikali na mapambano yasiyoisha.
Katika mahojiano maalumu na Mwananchi yaliyofanyika Februari 10, 2026, nyumbani kwake jijini Dar es Salaam, Heche amezungumzia masuala mbalimbali ya kisiasa na maisha binafsi.
Heche anaeleza maumivu aliyopitia kisiasa, kuanzia vitisho, kesi za mara kwa mara, na namna changamoto hizo zilivyomjenga.
Anafichua hofu ya familia, gharama za kisiasa alizozilipa binafsi, na misimamo yake iliyomfanya asirudi nyuma.
“Familia yangu imeumizwa sana ili kunikomesha mimi kisiasa, mdogo wangu wa damu kabisa, Suguta, aliuawa kama sehemu ya kunikomoa,” anasimulia Heche kwa sauti ya ujasiri yenye maumivu.
Akielezea tukio hilo, Heche anasema miaka minane iliyopita mdogo wake huyo aliuawa kwa kuchomwa na singe akiwa amefungwa pingu.
“Ilipangwa wakamtupe, aliyefanya hivyo akakamatwa, baadaye akaachiwa, yupo huru,” anasema Heche kwa huzuni.
Hilo ni moja kati ya mengi, Heche anaeleza pia namna nyumba ya mama yake ilivyobomolewa.
“Nikiwa diwani wa kata ya Tarime mjini, ndipo nyumba ya mama yangu ilibomolewa, vitu vyetu vikatupwa nje. Wakati huo ndipo tumetoka kufiwa na baba.
“Hizi siasa za Chadema, siasa za nchi hii, nina maumivu makubwa nazo, hata hivyo, namshukuru Mungu ninachofanya ni sahihi na siwezi kurudi nyuma, japo tuna maumivu makubwa katika struggle za nchi hii,” anasema.
Anasema siasa za mageuzi ya Tanzania zina maumivu kwa watu wengi, akibainisha kwamba hata wasiokuwa Chadema wanajikuta kwenye maumivu hayo.
“Kuna watu wamepigwa risasi nyumbani kwao, si Chadema, lakini ni sababu za siasa. Kuna wengine ndugu zao wamepotea na si hata wana Chadema, haya ni mambo ambayo hayakutakiwa yawe hivyo. Siasa siyo vita,” anasema.
Misimamo ya familia ilivyomjenga
Heche ni miongoni mwa wanasiasa wanaotajwa kuwa na misimamo, ambayo anasema ilimjenga.
Akitolea mfano namna alivyokamatwa na ikasemekana ametekwa, kabla ya ndugu zake kuonesha msimamo wa kulitaka Jeshi la Polisi liseme wapi alipo ndugu yao. Anasema familia yao ilijengwa kwa upendo.
“Baba yangu alikuwa na wanawake wanane, sisi tumezaliwa kwa baba watoto 60, lakini wote tumeishi kwa upendo, baba alitulea hivyo,” anasema.
Anasema baba yao, aliyekuwa na uchumi wa mifugo, alipenda haki, hakupenda uongo, hivyo amekulia katika maisha hayo tangu utoto wake.
Huku akitabasamu, Heche anasema, “Zamani sikuwa namuelewa kabisa baba katika kusema ukweli, nilipokuwa mtu mzima nimegundua ukweli ni kitu kizuri. Hii misimamo, kupenda haki na kuzungumza ukweli ni malezi yangu ya tangu utoto.”
Anasema malezi hayo ndiyo yapo hadi kwenye familia yao, hivyo mtu asitegemee anaweza kumuumiza ikaisha hivyo.
“Ndiyo sababu huwa nasema tusijenge chuki, inajenga visasi,” anasema Heche.
Akisimulia kukamatwa kwake hivi karibuni na kupelekwa Kituo cha Polisi Mtumba, Dodoma, huku ndugu zake wakionesha msimamo, anasema, “Nilipokamatwa nilikuwa kwenye hatua ngumu ya njaa, nilikaa siku mbili na nusu bila kula nikiwa mahabusu. Ndipo wale walionikamata wakaona nisije kuwafia mikononi ndipo wakaeleza wananishikilia.
“Wakati ule mama yangu alitoka tu India, akashuka uwanja wa ndege Dar es Salaam na kwenda Central (Kituo Kikuu cha Polisi) kutaka kujua nini kinaendelea. Ndugu zangu, Watanzania na wana Chadema walipambana, bila wao, nafikiri leo hii ingekuwa inazungumzwa historia nyingine juu yangu,” anasema.
Alama anayotamani kuiacha
Katika harakati zote za kisiasa, Heche anasema anatamani akiondoka kwenye siasa aache alama ya kuona Chadema imeshinda kwa haki na kuongoza dola.
“Kushinda ni jambo moja, lakini si kuishia tu kushinda bali na kubadilisha maisha ya watu. Tawala nyingi huwa zinapambana kuingia madarakani, nyingi zikiishaingia zinajisahau.
“Ambacho nakitaka ni kuhakikisha tumeshinda kwa haki, tumebadili maisha ya watu. Hiyo itaanza kujengwa katika ngazi za familia. Ipo hivi, familia yoyote yenye malezi mazuri huwa inashangilia haki, zipo ambazo zimejengwa kifisadi, hata ndugu yao akiiba zinashangilia. Tunataka tutoke huko,” anasema.
Anasema katika maisha yake ya kisiasa, hususani akiwa kijana, ametembelea nchi mbalimbali na kutolea mifano namna baadhi ya nchi watu wamejengwa kwa misingi ya kufuata haki na wajibu.
“Mfano mdogo tu, niliwahi kuwa Uingereza, nikachukua teksi saa 7 usiku, kwenye taa tuko wenyewe, lakini yule dereva hakuvunja sheria, alisimama kusubiri taa zimruhusu.
“Hata China tu, raia wamejengwa kwa misingi hiyo, nenda Japan ukifanya kosa unajinyonga mwenyewe. Inatakiwa tufike huko, ukiwa fisadi hata familia yako ikukatae. Tunatakiwa tujenge nchi ya hivyo,” anasema.
Huenda wengi hawafahamu kama Heche kabla ya kuingia kwenye siasa alikuwa mwalimu wa moja ya shule huko Tarime.
Anasema ualimu ni kazi ‘special’, japo kuna taswira imetengenezwa watu kuidharau taaluma hiyo, ambayo ndiyo inatengeneza ufahamu wa mtoto.
“Kama siyo siasa ningekuwa mwalimu, lakini pia nilipenda kuwa mwanasheria nitetee haki za watu. Niliwahi kuwa mwalimu, niliondoka huko kwa kuwa kwenye maisha yangu sipendi kuonewa.
“Historia yangu hadi kuacha ualimu ipo hivi, nilikuwa mwalimu pekee ninayefundisha kiingereza shule nzima, DC (Mkuu wa Wilaya) ya Serengeti wakati huo akataka kunionea, nikaondoka kwenye ualimu,” anasema.
Anasema nje ya ualimu na siasa pengine angekuwa mwanasheria, yote hiyo ni katika kupigania haki za watu au kuwatoa watu katika hatua moja kwenda nyingine kwa kuwapa ufahamu na maarifa.
Familia inavyotamani aache siasa
Heche anasema kama binadamu wengine naye kuna mazingira huwa yanamlazimisha kuishi kwa hofu kutokana na mazingira ya kisiasa yalivyo.
“Kutokana na aina ya siasa za nchi yetu, katika familia yangu siyo wote wanapenda niwe huku, mama yangu anatamani niache siasa hata kesho.
“Japo ananiunga mkono, ananiombea, lakini ni mtu ambaye anahisi kwenye siasa wakati wowote naweza kuumia, kupata tatizo, lakini hayo ndiyo maisha yangu. Natimiza wajibu wangu, kitakachotokea namwachia Mungu,” anasema.
Anasema hajawahi kujutia kuwa mwanasiasa wala kuwa Chadema, hiyo ni nafasi ya utumishi, ambayo japo wakati mwingine haina shukrani, kwani unaweza kufanya vizuri wengine wakatokea tu na kukutukana.
“Kuna watu wanafikiri labda mimi siogopi au sipendi kuishi, lakini binadamu yoyote anapenda kuishi. Mimi nimeona Tundu Lissu (mwenyekiti wa Chadema) akipigwa risasi, nimeona watu wanapotea, wengine wanashikiliwa magerezani bila makosa.
“Nimeona wengine familia zao zinaumizwa, hivyo na mimi ninazo hizo hisia za hofu za kuumizwa, lakini nimeamua kuzipuuza kwa sababu kitu ninachokifanya ni sahihi. Ujasiri siyo kuwa na hofu, ni kuizidi hofu,” anasema.
Anasema kuna nyakati anapokea taarifa za kutakiwa kuwa makini, akiambiwa kuna watu wanamfuatilia, lakini ameamua kuishinda hofu hiyo.
“Mimi ni mtu ninayependa kukaa na watu, napenda niende uwanjani nikaangalie mpira, nina marafiki hadi huko CCM, lakini kwa mazingira tuliyopo yanakulazimu ubaki nyumbani, ukihofia kuumizwa. Haya ni maisha mabaya kabisa, ndiyo maana tunapigania tuyabadilishe. Upinzani siyo chuki, mbishane kwa hoja, unikosoe nikukosoe,” anasema.
Anasema yeye ni mtu anayependa mijadala, misuguano, na kuna wakati huwa anaongea kwa hisia, watu wanafikiri anapenda ugomvi.
“Sipendi ugomvi kabisa, mimi ni mtu ninayependa kusema kitu kilivyo, na huwa sina tatizo na mtu binafsi, ila nina tatizo na tunavyoongozwa na wanaokuwa madarakani,” anasema.
Anasema anapenda kuambiwa ukweli na amewajenga wasaidizi wake kumwambia ukweli bila kumuogopa.
“Nikiwa mbunge, kuna wakati hadi katibu wangu nilikuwa nabishana naye mno, mimi ukishanishinda na ‘fact’ mezani sina tatizo. Ni mtu wa demokrasia ya kweli, sioni tatizo kukosolewa na kuomba msamaha kama nimekosea,” anasema, akiweka wazi matamanio yake ya kutaka kuona Serikali ikimuachia huru Tundu Lissu.
“Wamuachie Tundu Lissu na wafungulie chama chetu, na uonevu na utekaji ukomeshwe,” anasisitiza Heche.
Anasema huwa hapendi kuona mtu amehongwa pesa ili aseme uongo bila kujali anayemnenea uongo anaumizwa kiasi gani na familia ya huyo mtu inaumizwa kiasi gani.
Anashauri Watanzania wakiona mtu yoyote anaumizwa wasikae kimya na kuishia kupiga picha, kwani leo ni huyo, kesho ni wewe.