KWA wale wanaoamini katika Mungu siku zote huwa hakuna jambo gumu lisilotatulika. Wengi wao huwa wanaamini katika miujiza. Na miujiza kwa wenye imani na Mungu huwa ni suala jepesi. Na hapo kwa lugha ya Malkia husema “In God We Trust”.
Na huenda hivi ndivyo mashabiki wa soka nchini, hususani wale wa Yanga na Azam FC watakuwa wakiomba kimya kimya ili Mungu atende miujiza yake kwa timu hizo wakati pazia la hatua ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika likifungwa wikiendi hii.
Ndio, leo Jumamosi na kesho Jumapili ni wikiendi ngumu na iliyoshikilia hatma ya timu hizo mbili za Tanzania katika nafasi ya kukata tiketi ya kwenda ya robo fainali ya michuano hiyo, kila moja ikiwa kundi na viwanja tofauti, ili kulinusuru taifa kupata pigo la kupoteza timu nne michuanoni.
Wikiendi hii zinapigwa mechi za kukamilisha makundi ya michuano hiyo ili kupata timu 16 kwa kila michuano kutinga robo fainali, huku Tanzania ikizitegemea Yanga na Azam baada ya wawakilishi wengine, Simba na Singida Black Stars kuishiwa pawa mapema japo nazo zitakamilisha ratiba zao.
Wawakilishi hao wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika, Yanga, Simba, Azam FC na Singida BS zote wikiendi hii zinatupa karata za mwisho za makundi kwenye viwanja tofauti tofauti.
Hata hivyo, Simba inayoshiriki Ligi ya Mabingwa na Singida iliyopo Kombe la Shirikisho, haziwezi kusonga mbele hata iweje kutokana na pointi ilizonazo na macho ya na masikio ya wadau wa soka nchini ynaelekezwa katika mechi Yanga visiwani Zanzibar na ile ya Azam itakayochezwa Morocco.
Yanga itakuwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex kesho Jumapili kuikaribisha JS Kabylie ya Algeria inayoburuza mkiani ktika Kundi B na wawakilishi hao wa Tanzania, ikihitaji ushindi wa zaidi ya mabao 2-0, huku ikiiombea AS FAR Rabat ya Morocco ipoteze kwa Al Ahly ya Misri.
Kwa upande wa Azam FC ina kibarua kigumu cha kuhitaji ushindi pia kesho Jumapili au sare ya aina yoyote ugenini dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco, huku ikiiombea AS Maniema Union ya DR Congo ipoteze mbele ya Nairobi United kutokea Kenya.
Na hapo ndipo mashabiki wa klabu hizo mbili kila moja kwa imani yake watatumia muda uliosalia kabla ya timu hizo kushuka uwanjani ili ifanyike miujiza na kupenya katika tundu la sindano kuendelea kupeperusha bendera ya taifa katika michuano hiyo mikubwa kwa ngazi za klabu.
Baada ya wiki iliyopita Yanga kupoteza ugenini bao 1-0, dhidi ya AS FAR Rabat ya Morocco, kwa sasa matumaini pekee ya mabingwa hao wa Tanzania ni kushinda mechi ya kesho, huku ikiomba pia dua mbaya kwa Wamorocco wapoteze mbele ya Al Ahly.
Yanga imejiwekea mazingira magumu ya kusonga hatua ya robo fainali, ila ikiwa itashinda kwa zaidi ya mabao 3-0, huku kwa upande wa FAR Rabat itakayokuwa ugenini ikachapwa na Al Ahly, basi kikosi hicho kitakata tiketi hiyo rasmi ya kibabe.
Katika kundi hilo la B, Al Ahly ina pointi zake tisa, ikifuatiwa na AS FAR Rabat yenye nane, huku Yanga yenye tano ikiwa itaifunga JS Kabylie yenye pointi tatu, itafikisha pointi nane, lakini uwiano wa mabao unaweza kuiangusha zikilingana.
Iko hivi, Yanga ilishinda mechi ya kwanza nyumbani kwa bao 1-0, kisha ugenini ikaenda ikachapwa pia 1-0, hivyo, ushindi pekee kwa JS Kabylie hautatosha, isipokuwa itategemea na matokeo ya AS FAR Rabat inayohitaji sare tu mbele ya Al Ahly.
Moja ya jambo ambalo mashabiki wa Yanga hawataki lijirudie, ni kuona tena kikosi hicho kinashindwa kupenya hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, kama ilivyotokea msimu uliopita wa 2024-2025, katika mazingira yanayofanana na sasa.
Msimu uliopita, Yanga ilihitaji ushindi wa aina yoyote katika mechi ya mwisho ya makundi ili ifuzu hatua ya robo fainali ingawa, ilitoka suluhu (0-0) dhidi ya MC Alger ya Algeria, hivyo, kushuhudia ikimaliza ya tatu kundi A na pointi nane.
Kwa msimu huo, Al Hilal ya Sudan iliongoza kundi A na pointi 10, ikifuatiwa na MC Alger ya Algeria, iliyomaliza ya pili na pointi tisa, wakati Yanga ilikuwa ya tatu na pointi nane, huku TP Mazembe ya DR Congo ikiburuza mkia na pointi tano.
Pia rekodi zinaonyesha katika misimu mitatu mfululizo, Yanga ilipokumbana na timu za Algeria kwa mechi za maamuzi kama hizo, imetoboa mara moja tu dhidi ya CR Belouizdad msimu wa 2023-2024 na kupenya robo, lakini ilichemsha pia mbele ya USM Alger katika fainali ya Shirikisho Afrika kwa kulikosa taji kwa kanuni ya sheria ya bao la ugenini, ukiacha hiyo ya MC Alger.
Hivyo mashabiki wanataka kuona msimu huu wa nne mbele ya JS Kabylie itatoboa ama itaendelea kuwa wanyonge kwa Waarabu kupitia mechi hiyo itakayochezeshwa na Jean Jacques Ndala kutoka DR Congo anayekumbukwa kwa kucheza fainali ya AFCON 2025 kti ya Morocco na Senegal.
Licha ya uwepo wa washambuliaji, Prince Dube na ongezeko la Laurindo Dilson Maria ‘Depu’, aliyejiunga dirisha dogo la Januari 2026, na viungo wanaoweza kutengeneza nafasi akiwemo, Pacome Zouzoua, ila Yanga imekuwa na safu butu eneo hilo.
Katika mechi tano ilizocheza hadi sasa za hatua ya makundi, kikosi hicho kimekuwa hakina balansi nzuri maeneo yote hayo mawili ya kujilinda na kushambulia, kwani timu hiyo imefunga mabao mawili tu na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara nne.
Kushindwa kufunga mabao mengi na kuruhusu pia licha ya uwepo wa mabeki wakiongozwa na nahodha, Bakari Mwamnyeto ndani ya kikosi hicho, unatoa shaka ya timu hiyo kusonga mbele, japo lolote katika mpira wa miguu linawezekana ukijipanga vyema.
Mabosi wa Yanga wakiongozwa na bilionea, Ghalib Said Mohammed ‘GSM’ wamewatia hamasa mastaa wa timu hiyo kw kuwawekea mzigoni zaidi ya Sh 1.2 Bilioni kama watatinga robo fainali licha ya kusikilizia matokeo ya Misri.
GSM amewadaiwa ataibuka kambi ya Yanga kule visiwani kuanzia leo ili kuzungumza na mastaa kabla ya kesho kukaa jukwaani kuwaangalia wakipambana kuisaka tiketi hiyo ya robo, huku kocha Pedro Goncalves akisisitiza timu haitawaangusha mashabiki kwa namna alivyojipanga.
Huenda kocha huyo akafanya mabadiliko kidogo ya kikosi kulinganisha na kile kilichocheza ugenini dhidi ya As Far Rabat na kupoteza kwa bao 1-0, huku ikielezw nyota mpya, Buba Jammeh akitarajiwa kuanza kuonekana uwanjani katika mechi hiyo ya kufa au kupona kwa Yanga.
Mechi hii itakayopigwa leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam saa 1:00 usiku, ni ya heshima kwa Simba, kwani tayari kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Mkuu, Steve Barker, hakiwezi kwenda popote hata kikishinda mabao 10-0.
Simba iliumaliza mwendo tangu raundi ya nne ya hatua ya makundi ilipotoka sare ya mabao 2-2, nyumbani dhidi ya Esperance ya Tunisia, kisha kujitibulia ilipotoka sare nyingine ya 1-1, ugenini wiki iliyopita dhidi ya Petro Atletico ya Angola.
Timu hiyo inayoburuza mkia na pointi mbili kundi D, kwa sasa inasaka ushindi wa kwanza msimu huu nyumbani, kwani katika mechi nne zikiwemo za raundi ya awali na mbili za makundi haijawahi kushinda zaidi ya kutoka sare na nyingine ikichapwa.
Simba ilitoka sare ya 1-1 na Gaborone United ya Botswana raundi ya kwanza, kisha kutoka suluhu na Nsingizini Hotspurs ya Eswatini kabla ya kufungwa 1-0 na Petro Luanda ya Angola hatua ya makundi na kutoka sare ya 2-2 na Esperance ya Tunisia.
Simba iliyofika fainali ya Shirikisho msimu uliopita na kupoteza jumla ya mabao 3-1 mbele ya RS Berkane ya Morocco, ni mwaka 2003 tu, iliishia makundi, ila mara zote ilikuwa ikikwamia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa na Shirikisho Afrika.
Stade Malien ambayo imefuzu hatua ya robo fainali baada ya kufikisha pointi 11, inaingia katika mechi hiyo huku ikiwa na kumbukumbu nzuri, kwani mara ya mwisho ilipocheza dhidi ya Simba ilishinda nyumbani Mali mabao 2-1, Novemba 30, 2025.
Katika kundi hilo D, kwa sasa mechi inayosubiriwa kwa hamu kuona timu itakayoungana na Stade Malien ni kati ya Esperance iliyo nafasi ya pili itakayokuwa nyumbani kucheza dhidi ya Petro Luanda ya Angola, huku miamba hiyo yote ikiwa na pointi sita.
Azam itakuwa na kibarua kigumu kesho Jumapili ugenini huko Morocco ikicheza na Wydad Casablanca, huku kikosi hicho cha matajiri wa Jiji la Dar es Salaam wakisaka rekodi nyingine mpya ya kutinga hatua ya robo fainali kwa mara ya kwanza.
Timu hiyo tayari imeweka rekodi ya kushiriki hatua ya makundi ya michuano ya CAF kwa mara ya kwanza ikiwa kombe hilo la Shirikisho, huku ikipata pointi nyingi ambazo pia haijawahi kutokea klabu yoyote ya Tanzania katika ushiriki wa kwanza.
Azam iipata ushindi wa tatu mfululizo baada ya kuichapa AS Maniema ya DR Congo bao 1-0, wiki iliyopita kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar na kufikisha tisa, ambazo hakuna timu ya Tanzania iliyofikisha iliposhiriki mara ya kwanza.
Ushindi wa mechi ya mwisho wa Azam, umeifanya kundi B kuzidisha utamu, kwani licha ya Wydad Casablanca kufuzu baada ya kufikisha pointi 12, ila kazi kubwa imebakia kwa matajiri hao wa Jiji la Dar es Salaam na AS Maniema Union ya DR Congo.
Kwa sasa katika kundi hilo, inasakwa timu moja ya kuungana na Wydad, kwani AS Maniema Union yenye pointi tisa sawa na za Azam iliyo ya pili, mmoja wapo lazima apatikane mechi za mwisho, huku vibonde, Nairobi United ikiwa haina cha kupoteza.
Ugumu kwa Azam kusonga hatua ya robo fainali, inatakiwa iifunge Wydad katika mechi hiyo ya kesho, huku ikiiombea mabaya AS Maniema Union itakayokuwa nyumbani pale DR Congo ipoteze mbele ya Nairobi United, ambayo haijaonja ladha ya ushindi.
Timu hizo zikitoka pia sare katika mechi za mwisho za hatua ya makundi zitafikisha pointi 10, ingawa AS Maniema itasonga mbele, kwani matokeo ya wao kwa wao yanawabeba, kwa sababu ilishinda DR Congo mabao 2-0, huku Azam ikishinda nyumbani 1-0.
Azam inaingia katika mechi hiyo ikitaka kulipiza kisasi baada ya kuchapwa nyumbani kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar, bao 1-0, la Nordin Amrabat, Novemba 28, 2025, japo haitokuwa rahisi kutokana na ubora wa Waarabu hao.
SINGIDA KUSAKA HESHIMA TU
Wawakilishi wengine wa Kombe la Shirikisho Afrika, Singida Black Stars, itatupa karata yake ya mwisho kesho Jumapili saa 1:00 usiku kwa kucheza dhidi ya Stellenbosch ya Afrika Kusini, huku timu hizo zote zikiwa tayari zimeshaumaliza mwendo.
CR Belouizdad ya Algeria inayonolewa na aliyekuwa Kocha wa Yanga, Sead Ramovic, inaongoza kundi C ikiwa na pointi 12, ikifuatiwa na AS Otoho D’Oyo ya Congo Brazzaville yenye pointi tisa, ambazo timu zote tayari zimefuzu hatua inayofuata.
Kwa upande wa Singida inashika nafasi ya tatu na pointi nne ambazo ni sawa na za Stellenbosch inayoburuza mkiani, hivyo, mechi kati ya timu hizo zote ni ya kusaka heshima, kwani matokeo ya aina yoyote hayawezi pia kuzinufaisha kusonga mbele.
Mechi ya kwanza iliyopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan Zanzibar, Novemba 30, 2025, zilitoka sare ya bao 1-1, huku Singida ikichomoa dakika ya 90+1, kupitia kwa Marouf Tchakei, baada ya Langelihle Phili kuitanguliza Stellenbosch dakika ya 52.