Aziz KI aigusa mechi ya Yanga na Waarabu

KIUNGO wa zamani wa Yanga, Stephanie Aziz KI amewatoa hofu mashabiki wa klabu hiyo kwa niaba ya wachezaji wa kikosi hicho, akisema mastaa hao wamemhakikishia kushinda mechi ya kesho Jumapili dhidi ya JS Kabylie ya Algeria, licha ya ugumu uliopo.

Yanga inashuka saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa New Amaan, Zanzibar, kukabiliana na JS Kabylie katika mechi ya mwisho ya Kundi B ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikisaka tiketi ya kucheza robo fainali kwa mara nyingine baada ya msimu uliopita kukwama kwa MC Alger pia ya Algeria.

Akizungumza na Mwanaspoti, Aziz KI amesema presha haipo kwa mashabiki tu hata viongozi kwa na wachezaji kwani lengo ni kuhakikisha wanafuzu hatua inayofuata na siyo kushindwa.

Aziz KI amesema amezungumza na baadhi ya wachezaji wa Yanga na wamemhakikishia kwamba wamekuwa na maandalizi mazuri hivyo hakuna kitakachowakw amisha kupata ushindi nyumbani.

“Nimeongea na baadhi ya wachezaji wa Yanga, wamenihakikishia watafanya kila linalowezekana kuhakikisha Yanga wanapata matokeo yanayohitajika ili wafuzu,” amesema Aziz KI na kuongeza;

“Mashabiki wa Yanga lazima watulie kwani timu yao ilikuwa kundi gumu na bado inaweza kufuzu ikitegemea na matokeo ya Jumapili na wachezaji wa Yanga wanataki kupambania nembo ya timu ili kuendeleza ukubwa wa klabu.”

Aziz Ki amesema amewaambia baadhi ya wachezaji wa timu hiyo mambo ya kuzingatia wanapokwenda kwenye mchezo mgumu wenye presha ndani ya uwanja.

“Wanatakiwa kuendelea kuzungumza kila wakati kuwekana sawa na hawatakiwi kucheza kwa presha, lakini watafute nafasi na wazitumie kwa wakati, kwani hiyo ni mechi ya kuamua.

“Kweli kabisa Yanga inasubiriwa kuamua mchezo tena kwa ushindi mkubwa, lakini tukumbuke hii ni timu kubwa ina wachezaji wenye viwango vikubwa, mambo muhimu yote wakiyatimiza na kumsikiliza kocha basi watafanikiwa,” amesema Aziz.

Aziz tayari ameshajiunga na Ittihad ya Libya iliyomsajiliwa dirisha dogo msimu huu akitokea Wydad ya Morocco ambayo ilimnunua kutoka Yanga mwanzoni mwa msimu.