LIGI ya Championship inayotoa timu za kupanda Ligi Kuu kwa sasa imefikia patamu wakati raundi ya 18 ikitarajiwa kupigwa leo Jumamosi kwa mechi tatu kwenye viwanja mbalimbali na nyingine zikiendelea kesho Jumapili, huku ushindani ukipamba moto kwa kila timu kujiwekea mazingira bora.
Kwenye Uwanja wa Mkwakwani Tanga, African Sports inayoburuza mkiani na pointi nane, baada ya kuchapwa mabao 4-1 na B19 FC, itakuwa na kibarua kigumu cha kupambana na Gunners FC, iliyotoka kuichapa Songea United bao 1-0.
Timu hii ya mjini Tanga ambayo hufahamika kwa jina la utani la ‘Wanakimanumanu’, inakabiliwa na kibarua cha kupambana kurejea tena Ligi Kuu, baada ya kikosi hicho kushuka daraja msimu wa 2015-2016, kilipomaliza nafasi ya 15 na pointi 26.
Katika msimu huo, ulikuwa ni rekodi pia kwa soka la Tanzania kushuhudia Mkoa wa Tanga ukishusha timu tatu daraja, ambapo mbali na African Sports, ila nyingine zilizoshuka zilikuwa ni Mgambo JKT na Coastal Union ambayo kwa sasa iko Ligi Kuu.
Msimu huo, Mgambo JKT ilimaliza nafasi ya 14 na pointi 28, ikishinda mechi sita, sare 10 na kupoteza 14, ikifunga mabao 24 na kuruhusu 36, huku Coastal ikiburuza mkiani na pointi 22, baada ya kushinda mechi tano, sare saba na kupoteza 18.
Gunners inayoshiriki Ligi ya Championship kwa mara ya kwanza msimu huu, imeshinda mechi zote mbili za duru la pili ilizocheza hadi sasa, ikianza kwa kuifunga KenGold mabao 2-1 kisha kuichapa pia Songea United bao 1-0 wiki iliyopita.
Timu hiyo yenye benchi jipya la ufundi chini ya Kocha Mathias Wandiba, inaingia ikiwa na kumbukumbu nzuri pia mara ya mwisho ilipokutana na African Sports, kwani kikosi hicho kilishinda mabao 3-2 kwenye Uwanja wa Jamhuri, jijini Dodoma.
Kwenye Uwanja wa Nyankumbu mjini Geita, vinara wa Ligi hiyo, Geita Gold yenye pointi 43, baada ya kuifunga Transit Camp bao 1-0, itakuwa na kibarua kingine kigumu cha kupambana na Mbeya Kwanza ya Tabora inayoshika nafasi ya tatu na pointi 40.
Geita iliyoshuka kutoka Ligi Kuu Bara msimu wa 2023-2024 na msimu uliopitaa ikiwa Ligi ya Championship ilimaliza nafasi ya nne na pointi 56, chini ya aliyekuwa Kocha Mkuu, Mohamed Muya na kushindwa kupanda Ligi Kuu Bara, baada ya kufeli mechi za ‘play-off’.
Timu hiyo ilicheza ‘play-off’ ya kupanda Ligi Kuu Bara dhidi ya Stand United ‘Chama la Wana’ iliyomaliza nafasi ya tatu na pointi 61 na kushuhudia ikiondoshwa kwa jumla ya mabao 4-2, baada ya sare nyumbani ya 2-2 kisha kuchapwa ugenini 2-0.
Kwa upande wa Mbeya Kwanza inayotumia Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Tabora ikitokea Lindi ilipoweka kambi msimu uliopita, ilishuka daraja msimu wa 2021-2022, ilipomaliza mkiani baada ya kikosi hicho kukusanya jumla ya pointi 25, tu kibindoni.
Mechi hiyo itakayovuta hisia na mvuto kwa mashabiki wengi wa soka kutokana na nafasi za timu hizo mbili, itakuwa ni ya kisasi zaidi kwa kikosi cha Mbeya Kwanza, kwani raundi ya kwanza ilishindwa kutamba ikiwa nyumbani na kuchapwa mabao 2-1.
Mechi ya mwisho leo Jumamosi itapigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha ambapo wenyeji Mbuni iliyotoka kuchapwa mabao 3-1 ugenini na Bigman, itaikaribisha Hausung ya Njombe iliyochapwa pia 2-1 na Polisi Tanzania. Ligi hiyo itaendelea tena kesho Jumapili kwa maafande wa Polisi kuwa kwenye Uwanja wa Ushirika Moshi kucheza dhidi ya Stand United ‘Chama la Wana’, iliyotoka kuchapwa na KenGold mabao 2-0.
Polisi msimu uliopita wa 2024-2025, haukuwa mzuri sana baada ya kumaliza nafasi ya 10 katika Ligi ya Championship ikivuna pointi 33, ikishinda mechi nane, sare tisa na kupoteza 13, ambapo safu ya ushambuliaji ilifunga mabao 44 na kuruhusu 33.
Maafande hao wanapambana kurejea tena Ligi Kuu Bara baada ya kushuka daraja msimu wa 2022-2023, ilipomaliza nafasi ya 15 na pointi 25, kufuatia kushinda mechi sita tu, sare saba na kupoteza 17, ikifunga mabao 25 na kuruhusu 54.
Kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba mkoani Kagera wenyeji Kagera Sugar iliyolazimishwa sare ya bao 1-1 na kikosi cha Barberian, itaikaribisha Bigman yenye kumbukumbu nzuri baada ya mechi ya mwisho kuichapa Mbuni ya Arusha mabao 3-1.
Mechi ya mwisho ya kuhitimisha raundi ya 18, itapigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha kwa wenyeji, TMA iliyochapwa bao 1-0 na Mbeya Kwanza itacheza na B19, iliyotoka kuichapa African Sports ya Tanga mabao 4-1.
Kocha msaidizi wa Bigman, Mohamed Kijuso amesema malengo ya timu hiyo kwa sasa ni kumaliza nafasi nne za juu, licha ya ushindani mkubwa uliopo hasa katika mechi za duru hili la pili la lala salama, ambazo ndizo ngumu kutokana na mahitaji ya kila timu.
“Nafasi ya kumaliza nafasi nne za juu bado ipo kwetu kwa sababu gepu la pointi sio kubwa sana, raundi ya pili huwa ni ngumu kwa kila mechi bila ya kujali mazingira unayocheza, jambo la muhimu ni kucheza kwa umakini sana,” amesema Kijuso.
Timu zinazomaliza nafasi mbili za juu ndizo zinazopanda Ligi Kuu moja kwa moja ile inayosika nafasi ya tatu na nne zitakacheza play-off zenyewe na mshindi atavaana na mshindwa wa mechi za timu za Ligi Kuu kati ya iliyoshika nafasi ya 13 naa 14 ili kuchuana kupanda.
Timu za Ligi Kuu ikifungwa itashuka daraja na kuipisha timu ya Championship kuungana na mbili za awali, lakini timu ya Championshipo ikipoteza itaichia nafasi ya Ligi Kuu kubaki huko kama itakavyokuwa kwa timu hiyo n kujipanga tena kwa msimu ujao. Msimu uliopita Mtibwa Sugar na Mbeya City zilitoboa kurudi Ligi Kuu, huku Fountain Gate ilinusurika kushuka kutoka Ligi Kuu mbele ya Stand United.