JKT, Coastal yajirudia baada ya miaka sita

SARE ya kufungana bao 1-1 kati JKT Tanzania na Coastal Union katika mechi ya Ligi Kuu iliyopigwa juzi kwenye Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo Mbweni ni ya kwanza timu hizo baada ya kupita miaka sita.

Kabla ya mechi hiyo, mara ya mwisho kwa timu hizo kutoka sare ya kufungana bao 1-1, ilikuwa ni Februari 4, 2020, wakati huo kikosi hicho cha maafande wa JKT Tanzania kikiwa uwanja wa nyumbani, kama ilivyotokea pia kwenye pambano la juzi.

Katika mechi hiyo ya Februari 4, 2020, JKT ilitangulia kupata bao la kwanza lililofungwa na aliyekuwa mshambuliaji nyota wa kikosi hicho, Adam Adam dakika ya 50, huku Ayoub Lyanga akiifungia Coastal Union dakika ya 61, kwa mkwaju wa penalti.

Tangu Februari 4, 2020, mechi iliyojirudia ya sare ya bao 1-1 ni ya Februari 13, 2026, ambapo JKT ilipata bao la dakika ya nne kwa penalti ya Valentino Mashaka, huku Shiza Kichuya aliyeichezea maafande akiisawazishia Coastal dakika ya 12.

Kuanzia mechi ya Februari 4, 2020, timu hizo zimekutana mara tisa katika Ligi Kuu Bara, ambapo JKT imeshinda mara nne, Coastal ikishinda mara tatu na sare mara mbili ambazo ni ya suluhu (0-0), Mei 25, 2024 na ya bao 1-1, Februari 13, 2026.

Mechi ya JKT ilikuwa ya 16 msimu huu ingawa ni ya tisa nyumbani ikishinda tatu, sare nne na kuchapwa miwili ambayo ni mabao 2-1 dhidi ya Simba, Novemba 8, 2025; kisha 1-0 mbele ya Dodoma Jiji, Januari 30, 2026.

Kwa upande wa Coastal mechi hiyo na JKT ilikuwa ni ya nane kucheza ugenini msimu huu, ambapo kati hizo, kikosi hicho cha Wagosi wa Kaya kimeshinda mmoja katika ushindi wake wa 4-1 dhidi ya Prisons, sare mitatu na kuchapwa minne.