KOCHA Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ ameanza kwa kishindo kazi ya kuinoa Mashujaa ya Kigoma baada ya juzi usiku kuizima Mtibwa Sugar ikiwa uwanja wake wa nyumbani wa Jamhuri Dodoma kwa mabao 3-1, huku akiweka bayana anapambana kupata wa kumsaidia kikosini.
Julio aliyetambulishwa katika ya wiki hii na maafande hao wa Mashujaa walioandika rekodi ya aina yake ya kucheza mechi sita mfululizo za Ligi Kuu Bara ikiwa ugenini, juzi aliiongoza timu hio kupata ushindi wa kwanza mnono msimu huu kupitia mabao ya Hassan Haji ‘Cheda’, Jaffar KIbaya na Abdul Bakari, huku Fredrick Magata akiifungia Mibwa bao la kufutia machozi.
Matokeo ya juzi yameifanya Mashujaa kuchupa kutoka nafasi ya 10 hadi ya nane ikifikisha pointi 17 baada ya mechi 15, ikishinda mechi nne, sare tano na kupoteza sita, huku ikifunga mabao manane na kufungwa 15 ikiwa imekamalisha duru la kwanza la Ligi hiyo inaoongozwa na JKT Tanzania.
Kabla ya mechi hiyo, Julio ambaye ni nyota na beki wa zamani wa kimataifa wa CDA, Simba na Taifa Stars, aliwahi pia kuzinoa timu hizo sambamba na Coastal Union, Mwadui na KMC, alisema alikuwa anapambana kutafuta mtu wa kusaidiana naye.
Akizungumza na Mwanaspoti, Julio alisema kazi kubwa aliyonayo kwa sasa ni kuhakikisha kikosi hicho kinarudisha makali yake na jambo la kwanza ataanza nalo ni kuwajenga wachezaji kisaikolojia.
Alisema, ameiangalia timu kwa ukaribu mkubwa na amegundua yapo maeneo baadhi ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi kwa haraka ili kukiokoa kikosi hicho.
“Kazi ya kwanza ninayotaka kuanza nayo Mashujaa ni kuwajenga kisaikolojia wachezaji wangu na ninaamini tunaweza kubadilika na kurudi kutafuta ushindi kwa haraka.
“Nimeangalia timu inavyocheza najua wapi pa kuanzia ili tuweze kuiokoa timu na matokeo mabaya, nitatumia uzoefu wangu wote kuhakikisha Mashujaa inafanya makubwa sawa na jina lilivyo.”
Julio ni miongoni mwa makocha wazawa wakongwe wenye uzoefu wa kufundisha timu mbalimbali ikiwemo Simba na timu ya Taifa ‘Stars’, lakini ana rekodi ya kutokudumu nazo muda mrefu.