TWCC: Wanawake tumieni ongezeko la watu nchini kujiinua kiuchumi

Dar es Salaam. Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania ((TWCC) imesema idadi kubwa ya watu nchini ni fursa muhimu ya kiuchumi inayoweza kutumiwa na wanawake na vijana kujikwamua kupitia biashara na uwekezaji.

Akizungumza leo Jumamosi Februari, 14, 2026 katika mkutano wa wanachama unaoenda sambamba na maadhimisho ya miaka 20 ya kuwezesha wanawake, Rais wa TWCC, Mercy Silla, amesema ongezeko la watu linapaswa kuonekana kama soko la uhakika la bidhaa na huduma zinazozalishwa ndani ya nchi.

Amesema kila ongezeko la idadi ya watu linaongeza mahitaji ya chakula, mavazi, elimu, afya na huduma nyingine za kijamii, hali inayofungua milango kwa wafanyabiashara kupanua shughuli zao.

“Tusione idadi ya watu kama mzigo. Huu ni mtaji mkubwa wa soko. Ukizalisha bidhaa bora na huduma zenye viwango, soko lipo,” amesema.

Silla amesema wanawake wanapaswa kujipanga na kujiandaa kuzalisha kwa ubora, kusajili biashara zao na kutumia teknolojia ili kufikia wateja wengi zaidi.

Akizungumzia miaka 20 ya TWCC, Mercy amesema chama hicho kimefanikiwa kuwainua wanawake kwa kuwapa mwanga wa uwekezaji, kuwaunganisha na taasisi za fedha na masoko pamoja na kuwajengea ujasiri wa kuthubutu.

Kupitia hilo wanawake sasa wametambua fursa zilizopo, wamejua wanachotaka na wameanza kuingia katika sekta mbalimbali zikiwamo madini, michezo na sanaa, huku akisisitiza kuwa idadi kubwa ya watu nchini ni soko la uhakika kwa bidhaa na huduma zao.

“Sasa hakuna mtu anayelalamika kuzalisha bidhaa na hana masoko na kila mtu anatambua kuwa masoko yapo huku mitaji ikipatikana maeneo mbalimbali,”

“Huko tuendako tunaamini wanawake na vijana wengi zaidi wanajibidiisha katika biashara hivyo mazingira yanawekwa na fursa zinaoneka huku sisi tukiwasaidia kujiweka tayari ili mwekezaji akija aweze kuridhika na kuona kuwa ni mtu anayeweza kufanya naye biashara,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa TWCC, Mwajuma Hamza amesema pamoja na soko, idadi ya watu pia ni rasilimali ya nguvu kazi inayoweza kuongeza uzalishaji na kukuza ajira.

Amesema vijana wengi wanaweza kushiriki katika mnyororo wa thamani kama wazalishaji, wasambazaji au wabunifu wa bidhaa na huduma mpya, iwapo watapatiwa mafunzo na mitaji.

“Tunachohitaji ni kuwaandaa wanawake na vijana ili waweze kutumia fursa ya soko lililopo. Mazingira ya biashara yanazidi kuboreshwa na taasisi za fedha zipo tayari kusaidia,” amesema.

Aidha, viongozi hao wamesema sekta mbalimbali ikiwamo kilimo, usindikaji wa vyakula, madini, sanaa na huduma za kijamii zina nafasi kubwa ya kunufaika na ongezeko la watu nchini.

Akizungumzia safari ya miaka 20, Mwajuma amesema awali hakukuwa na sauti iliyowaunganisha wanawake wala chombo imara cha kuwakilisha mahitaji yao, hali iliyofanya mchango wao katika uchumi kutotambulika tofauti na sasa.

Tofauti na sasa juhudi zao zinaonekana huku kukiwa na jitihada mbalimbali za kuwakwamua kiuchumi kupitia kuwapa mitaji.

Mbali na hayo yote, Mwajuma amesema changamoto kubwa inayowakumba wanawake ni kutojiamini na mfumo dume ambazo zilifanya washindwe kujiendeleza.

“Lakini sasa mwamko ni mkubwa, wanawake wanashiriki mafunzo, wanachukua mikopo na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi ili kuchangia ujenzi wa taifa,” amesema.

Mkurugenzi wa kampuni ya True Mark:

Agnes Mgongo amesema katika kipindi cha miaka 20 ya TWCC imesaidia kuwapa nguvu ya kuthubutu na kupanua biashara zao.

Amesema licha ya maendeleo yaliyopatikana, bado wanawake wengi wana hofu na huona biashara ni rahisi, wakati inahitaji umakini, muda na ubunifu wa kila siku.

“Kupitia umoja huo tunaweza kufikia malengo makubwa zaidi,” amesema.

Mwandishi wa kitabu Know My Legal, Amne Swedy amesema hatua kubwa imefikiwa katika kuwawezesha wanawake kufikia mitaji na kushiriki katika biashara huku akisisitiza uthubutu kuwa jambo la msingi.

“Bila kuondoa woga, mwanamke hawezi kufanikiwa, mwanamke jiamini na kuchukua hatua katika safari yako ya kiuchumi,” amesema.