Viongozi wa migodi midogo wapewa mafunzo ya baruti

Musoma. Wafanyakazi 75  wa migodi ya wachimbaji wadogo mkoani Mara wamepewa mafunzo ya usalama kazini ikiwamo matumizi sahihi ya baruti ili kuepuka majanga na ajali  zinazoweza kutokea kutokana na matumizi yasiyo sahihi  sambamba na mazingira yasiyo salama katika maeneo yao ya kazi.

Mafunzo hayo ya awamu ya kwanza yamehusisha walipuaji, wakurugenzi, wakaguzi  na mameneja wa migodi hiyo midogo kutoka wilaya za Musoma, Butiama na Bunda mkoani Mara.

Mafunzo hayo yametolewa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mikakati ya Serikali katika kuboresha mazingira ya kazi kwa wachimbaji wadogo ili waweze kufanya shughuli zao kwa tija zaidi.

Akizungumza leo Jumamosi,  Februari 14, 2026 mjini Musoma wakati wa kuhitimisha mafunzo hayo ya siku tano, Mkufunzi kutoka Taasisi ya Rasilimali Madini Dodoma (MRI),  Salum Mkango amesema  mafunzo hayo yametolewa baada ya kubainika kuwepo kwa matumizi yasiyo sahihi ya baruti wakati wa ulipuaji jambo ambalo linahatarisha maisha ya wafanyakazi wa migodi hiyo.

“Mbali na matumizi ya baruti kwenye uliapuaji tumebaini pia usafirishaji wa baruti haufanyiki kwa njia salama na hata utunzaji wake pia sio salama kwani wapo wachimbaji ambao wanalala na baruti kwenye nyumba moja tena zile nyumba za kule migodini,” amesema

Amesema mazingira yasiyo salama ni moja ya sababu za kutokea ajali katika migodi hiyo huku akitolea mfano tukio la wachimbaji sita kufariki na wengine 11 kujeruhiwa baada ya kufukiwa na kifusi katika mgodi wa dhahabu katika Kijiji cha Mwakitolyo mkoani Shinyanga Mei 2025.

Amesema mafunzo kama hayo yatatolewa kwa awamu tofauti lengo likiwa ni kuwafikia wachimbaji wadogo nchini kote hatua ambayo itasaidia kupunguza ama kumaliza kabisa ajali zinazotokea migodini kutokana na uendeshaji wa shughuli katika maeneo hayo kwa njia zisizokuwa za kitaalamu.

Mhandisi kutoka Ofisi ya Ofisa Madini Mkoa wa Mara, Wilson Bankobeza amesema mafunzo hayo yatasaidia katika kuongeza ujuzi hasa katika ukaguzi kabla na baada ya kazi katika migodi ili iwe salama.

“Mazingira salama yana matokeo chanya katika kufanya kazi kwa tija na hii itasaidia hata kuongeza kipato cha wachimbaji na pato la Serikali litokanalo na uchimbaji hasa wa wachimbaji wadogo,” amesema.

Amesema Serikali imedhamiria kuboresha mazingira ya wachimbaji wadogo katika nyanja zote huku suala la usalama mahali pa kazi likiwa ni kipaumbele.

Amesema sekta ya madini ni miongoni mwa sekta zinazotoa fursa ya ajira, hivyo usalama wa wachimbaji ni jambo muhimu ikiwa ni pamoja na suala zima la utunzaji wa mazingira ili uchimbaji uweze kuwa endelevu na kwa faida kizazi cha sasa na kijacho.

Bankobeza amesema ofisi yake itahakikisha mafunzo kama hayo yanawafikia walipuaji, wakurugenzi, wakaguzi  na mameneja wa migodi midogo yote iliyopo mkoani Mara, kwa sasa wapo kwenye maandalizi ya kuwafikia katika wilaya za Tarime, Serengeti na Rorya.

Baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wameshukuru kwa kupata fursa hiyo  huku wakitoa wito kwa Serikali kuhakikisha mafunzo yanakuwa endelevu.

Lawi Kishosha amesema suala la utunzaji wa mazingira katika migodi mingi halikuwa kipaumbele lakini baada ya mafunzo hayo wameelewa uhusiano uliopo kati ya mazingira na shughuli za uchimbaji, hivyo kuahidi kuwa mabalozi wa mazingira katika maeneo yao ya kazi.

“Haya mafunzo ni muhimu sana na kumbe tulitakiwa twende chuo Dodoma tena kwa gharama zetu lakini Serikali imetusaidia ,naiomba Serikali iendelee kuwafikia wachimbaji wengi zaidi ili wapate elimu hii ili kuboresha shughuli zetu migodini,” amesema

Denis Magabe amesema kabla ya mafunzo walikuwa wanafanya kazi kwa mazoea lakini hivi sasa watafanya kazi kitaaluma na kwa uhakika zaidi.

“Ingawa kwangu hatujawahi kupata ajali kwenye mgodi wetu lakini baada ya mafunzo nimegundua tulikuwa kwenye hatari kubwa, hivyo kupitia haya mafunzo tunakwenda kuboresha shughuli zetu kwa kuzifanya kitaalamu zaidi,” amesema.