Dodoma. Mwenyekiti wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Mary Chatanda amesema jumuiya hiyo itaibeba ajenda ya bima ya afya kwa wote na kuitangaza nchi nzima kuanzia ngazi ya mashina hadi Taifa ili kuwaelimisha wanawake na watu walioko kwenye makundi maalumu kujiunga na bima hiyo.
Amesema hiyo ni mojawapo ya mkakati wa jumuiya hiyo kuunga mkono mafanikio ya siku 100 za Rais Samia Suluhu Hassan kuwepo madarakani ambaye aliahidi kuanza kwa bima ya afya kwa wote na kweli imeanza.
Chatanda ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Februari 14, 2026 kwenye kikao kazi cha UWT ambacho wajumbe wamepewa elimu kuhusu mpango wa bima ya afya kwa wote kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
Amesema kazi ya kutangaza mpango wa bima ya afya kwa wote utafanywa na UWT kwa kushirikiana na wataalamu kutoka NHIF, kuanzia ngazi ya shina hadi Taifa ili kila mwananchi aijue na kujiunga kulingana na sifa yake.
”Kupitia uzinduzi wa mpango wa bima ya afya kwa wote kwa mara ya kwanza nchini kwetu, ikihusisha makundi ya wanawake wajawazito, watoto chini ya miaka mitano, watu wenye ulemavu, wazee kupatiwa huduma za afya bure ,” amesema Chatanda.
Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Chatanda.
Amesema watahakikisha makundi maalumu yaliyotajwa yanatambuliwa na kusajiliwa ili waweze kupata huduma za matibabu bure.
Amesema jumuiya hiyo haitalala mpaka ihakikishe kuwa kila mwanamke nchini amepata uelewa na kujiunga na bima ya afya kwa wote.
Mwakilishi kutoka NHIF, Jackline Tarimo amesema makundi maalumu yameshaanza kuandikishwa kwenye mpango huo kwa kutumia mamlaka za utambuzi.
”Kwa mujibu wa mamlaka za utambuzi hapa nchini tuna asilimia 26.4 ya kaya ambazo hazina uwezo zenye jumla ya watu 3,917,000 ambao watapewa huduma ya bima ya afya kwa wote kwa awamu ya kwanza ambao ndiyo shughuli ya kuwatambua na kuwasajili inaendelea, hawa ni wale ambao hawana uwezo wa kulipia,” amesema Tarimo.
Amesema mpango mwingine ni ule wa kila kaya yenye watu sita kuchangia Sh150,000 kwa mwaka.
Mjumbe wa UWT kutoka Mkoa wa Tanga, Mwantumu Mahiza ameitaka Serikali kuhakikisha inaboresha huduma za afya kwa wananchi kwa kuondoa dosari ndogondogo ambazo huwa zinajitokeza pindi wananchi wanapokwenda kupata huduma hospitalini.
Amesema yapo malalamiko ambayo huwa yanatolewa kwa wananchi kukosa dawa japo wana bima za afya na kuitaka Serikali iboreshe huduma ili huduma zote muhimu zipatikane kuanzia kumwona daktari, vipimo hadi dawa.