Arusha. Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima amewataka wananchi kufuatilia na kuchangamkia fursa zinazotolewa na Serikali, kwa kuwa uchumi imara wa kaya ni msingi muhimu wa ustawi wa familia na ulinzi wa mtoto.
Waziri Gwajima amesema hayo leo Jumamosi, Februari 14, 2026 jijini Arusha alipotembelea shirika la kulea watoto la SOS, Ngaramtoni kujionea miradi ya uwezeshaji wa ulinzi wa mtoto katika ngazi ya jamii, kukuza malezi na kuongeza fursa za kiuchumi kwa vijana na wanawake.
Waziri Gwajima amesema familia zenye kipato cha uhakika huwa na uwezo mkubwa wa kuwalinda watoto dhidi ya ukatili, migogoro ya kifamilia na changamoto za malezi.
Amesema changamoto nyingi za malezi hujitokeza katika familia zenye hali duni kiuchumi.
Amesema Serikali inaendelea kuboresha mazingira mazuri ya kutengeneza fursa za kiuchumi sambamba na kupunguza vikwazo vya biashara na ujasiriamali ikiwamo kutoa mikopo ili watu wachangamkie kujiiunua kiuchumi.
“Kukosekana kwa shughuli za kiuchumi ndani ya kaya husababisha kuyumba kwa malezi, migogoro ya kifamilia na watoto kujikuta wakijilea wenyewe,” amesema. “Wapo wanaosema hakuna kazi, Serikali inaendelea kutengeneza fursa kila kukicha na kuondoa vikwazo vya kibiashara na kutoa mikopo pia.”
Ameongeza kuwa, ni muhimu jamii ikaacha kulalamikia ajira za kupewa na kutumia muda mwingi kufuatilia taarifa zisizo na tija mitandaoni na badala yake ielekeze nguvu katika kutafuta na kutumia fursa za kujikwamua kiuchumi.
Katika ziara hiyo, Waziri Gwajima alikabidhi pikipiki 15 zenye thamani ya Sh40.5 milioni kwa vijana kutoka halmashauri nne za Mkoa wa Arusha, pamoja na hundi ya Sh17 milioni kwa vikundi vya malezi vilivyo chini ya programu za SOS ili kupanua wigo wa ajira binafsi na kuongeza kipato kwa familia.
Awali, Mkurugenzi wa SOS Children’s Villages Tanzania, Thomas Kipingili alisema shirika hilo linajikita katika kuwahudumia watoto waliopoteza au walio katika hatari ya kupoteza malezi ya familia kwa kuwalea katika mfumo wa kifamilia kwenye vituo vyake.
Alisema pia shirika linawezesha familia kiuchumi ili kuzuia kuvunjika kwa familia, hivyo kupunguza hatari ya watoto kukosa malezi.
“Kwa sasa tunatekeleza pia programu kwa watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani katika mikoa mbalimbali nchini.
“Katika kipindi cha miaka minne, vijana 1,229 wamefikiwa, 1,000 wamepewa mitaji, 450 wamepatiwa malezi mbadala, huku watoto 3,538 na familia 1,221 katika halmashauri za Arusha wakinufaika kupitia mifumo ya Serikali,” alisema Kipingili.
“Hadi sasa shirika limetoa zaidi ya Sh173 milioni kupitia programu za ulinzi wa mtoto, malezi chanya na uwezeshaji wa vijana, ambapo watoto 346 wamenufaika moja kwa moja.”
Mwenyekiti wa Kamati ya Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (Mtakuwwa) katika Kata ya Oltrumet, Huruma Lagris alisema jumla ya matukio 16 ya ukatili yameripotiwa katika eneo hilo, yakiwamo ya kiuchumi, na kwamba hatua zimeanza kuchukuliwa.
Mkazi wa Arumeru, Neema Swai aliiomba Serikali kuhakikisha matukio ya ukatili yanayoripotiwa yanafuatiliwa hadi mwisho ili wahusika wawajibishwe.
“Matukio mengi ya ukatili hufanywa na ndugu wa karibu, ni muhimu watendaji wa Serikali wasichoke kufuatilia kesi hadi adhabu itolewe.
“Wakati mwingine vitisho huwakatisha tamaa waathirika, wanapoona kimya kutoka kwa watendaji, hukata tamaa,” alisema.