Mbeya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa, amemuagiza Kamanda wa Polisi, Benjamin Kuzaga, kuelekeza nguvu katika kukabiliana na matukio ya ubakaji, ulawiti na ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto.
Malisa ametoa agizo hilo leo, Jumamosi, Februari 14, 2026, baada ya kukagua gwaride na kukabidhi tuzo kwa askari 15 waliofanya vizuri katika nyanja mbalimbali, hususan kudhibiti ubakaji na ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto, katika maadhimisho ya Siku ya Familia ya Polisi (Police Family).
“RPC, mkaongeze nguvu kudhibiti matukio ya ubakaji, ambayo sasa mengine yanahusisha wazazi na walezi, kundi ambalo linalalamikiwa ikiwemo unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya watoto,” amesema.
Malisa amesema jamii inapaswa kuhakikisha watoto wanalindwa na kupata haki za msingi na kuwa salama wawapo majumbani, sambamba na kuonya jamii kuacha usiri ili kulisaidia Jeshi la Polisi kutekeleza majukumu yake.
“Hapo kuna mambo mawili, changamoto ya ukatili wa kijinsia na ubakaji ambao hufanyika katika ngazi ya familia au watu wa karibu, lakini imeenda mbali zaidi mpaka kwa walezi,” amesema.
Kufuatia changamoto hiyo, Malisa amewataka walezi shuleni na nyumba za ibada kubeba jukumu la kuleta watoto katika mazingira salama na kusisitiza uhamasishaji wa kampeni ya “Mtoto wa mwenzio ni wako” uwe endelevu ili kuikumbusha jamii.
“Wana Mbeya, sisi ni wasomi, waelewa na tunatambua mambo mengi, tutumie fursa hiyo kulinda jamii kwa kuweka msisitizo kuhakikisha watoto wako salama, si kwa kusikia, bali kwa kufanya kwa vitendo, na si kuwa na imani tu kwamba familia zipo salama,” amesema.
Katika hatua nyingine, Malisa ameonesha kusikitishwa na usiri wa taarifa za matukio hayo na kwamba mambo mengi yanamalizwa kimila kijamii, kifamilia na kiukoo, hali inayopelekea jamii kutokupata msaada wa Serikali katika kumaliza jambo hilo.
“Nasisitiza kuwepo kwa uwazi wa utoaji wa taarifa sahihi kwa wakati kwa lengo la kuliwezesha Jeshi la Polisi kufanya kazi yake kwa weledi katika kukabiliana na matukio hayo,” amesema.
Ameongeza, “Rai yangu mwaka 2026, twendeni tukaongeze juhudi kwenye hilo, mwaka jana tulikutana na changamoto, lakini kulikuwa na utulivu. Utulivu huo uendelee ili kuvutia wawekezaji,” amesema.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga, amesema wamepokea maelekezo ya mkuu wa mkoa katika kuhakikisha wanakabiliana na matukio ya ukatili wa kijinsia, ubakaji, ulawiti na vipigo.
“Tuombe jamii kutoa ushirikiano wa kufichua watu wanaojihusisha na matukio hayo, lakini pia tuonye tabia ya baadhi ya wananchi kufanya siri na kumalizana kwenye ngazi za familia,” amesema.
Kuzaga ametaja moja ya changamoto ya makosa kujirudia ni kutokana na usiri wa matukio hayo kwenye familia, jambo linalohitaji ushirikiano, ili kuwezesha Jeshi la Polisi kutekeleza majukumu, na kubainisha mwaka 2026 wameweka mikakati kabambe ya kutokomeza.
“Lakini mwaka 2025, Dawati la Jinsia la Polisi limefanya kazi kuhakikisha wanazuia ukatili kwa kuwafikia wananchi na kupokea taarifa nyingi, jambo ambalo limefanikisha baadhi ya watuhumiwa kukamatwa na kuchukuliwa hatua,” amesema.
Kuhusu utoaji wa zawadi kwa askari wake, Kuzaga amesema kuwa lengo ni kuthamini utendaji wao wa kazi walioonesha mwaka 2025, ili kuwa chachu kwa wale walio suasua kudhibiti uhalifu.
Mmoja wa Polisi aliyepata tuzo na motisha kutoka Dawati la Jinsia Wilaya ya Rungwe mkoani hapa, Sajenti Twitike Mwakalebela, amesema asilimia kubwa ya kesi wanazopokea na kufanyia kazi ni ubakaji, ulawiti na shambulio la mwili.