SEKTA BINAFSI YAUNGANA NA SERIKALI KUHAMASISHA MATUMIZI YA NISHATI SAFI YA KUPIKIA

KATIKA kuunga mkono juhudi za Serikali za kuhimiza matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia, kampuni za TotalEnergies na Hisense zimeanzisha kampeni maalum ya kuhamasisha wananchi kuachana na nishati zisizo salama na kuhamia teknolojia za kisasa zinazolinda afya na mazingira.

Mpango huo ni sehemu ya utekelezaji wa ajenda ya taifa ya nishati safi inayolenga kufikia mwaka 2034, angalau asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia, hususan gesi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo leo Februari 14, 2026, Meneja Masoko wa TotalEnergies, Caroline Kakwezi, amesema ushirikiano huo unaonyesha dhamira ya sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia upatikanaji wa nishati salama, nafuu na ya kisasa.

Amesema kupitia kampeni hiyo, wananchi wanahamasishwa kutumia gesi ya TotalEnergies sambamba na majiko ya kisasa ya Hisense, hatua inayolenga kuongeza usalama jikoni, kurahisisha matumizi na kuboresha ufanisi wa nishati.

“Kampeni hii itatekelezwa kuanzia sasa hadi Aprili 7, ikiwa ni mchango wetu katika kufanikisha mkakati wa taifa wa nishati safi. Tunatarajia kuona kaya nyingi zaidi zikibadili mfumo wa upishi na kuanza kutumia nishati salama,” alisema.

Katika kipindi cha kampeni, mteja atakayenunua jiko la Hisense katika maduka rasmi atapatiwa bure mtungi wa gesi wa kilo 13 wa TotalEnergies, ili kurahisisha mwanzo wa matumizi ya nishati safi majumbani.

Kwa upande wake, Ofisa Masoko na Mauzo wa Hisense Tanzania, Oscar Kiwuyo, alisema kampeni hiyo inalenga kuongeza upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya kupikia, hasa wakati familia nyingi zinajiandaa na misimu ya Ramadhani na Kwaresima.

Ameeeleza kuwa mbali na mtungi wa gesi wa bure, wateja watanufaika na punguzo la bei kwa baadhi ya majiko ya Hisense, hivyo kupunguza gharama za kuhamia kwenye nishati safi kwa wananchi wa makundi mbalimbali.

“Kupitia ushirikiano huu, tunachangia juhudi za Serikali na jamii kwa ujumla katika kuachana na nishati zisizo salama. Tunaamini ubora wa gesi ya TotalEnergies kama tunavyoamini teknolojia na usalama wa majiko yetu,” alisema.

Ameongeza kuwa majiko ya Hisense yametengenezwa kwa teknolojia inayozingatia matumizi bora ya gesi na umeme, jambo linalopunguza hofu ya wananchi kuhusu gharama za nishati wanapotumia vifaa vya kisasa.

Oscar pia alitoa tahadhari kwa wananchi kujiepusha na bidhaa bandia kwa kununua bidhaa katika maduka rasmi yaliyoidhinishwa, ili kupata bidhaa halisi zenye viwango vya kimataifa na dhamana.