Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikiendelea kusukuma mbele lengo lake la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034, sekta binafsi imeanza kujitokeza kwa kasi kwa kuoanisha juhudi zake na ajenda ya maendeleo ya taifa.
Kampeni mpya kati ya TotalEnergies na Hisensse imezinduliwa leo Jumamosi, Februari 14, 2024, umeashiria namna kampuni binafsi zinavyoweza kushirikiana kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi, juhudi inayopewa kipaumbele na Rais Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo jijini Dar es Salaam, Meneja Masoko wa TotalEnergies, Caroline Kakwezi, amesema mpango huo uliopewa jina la “Gesi TotalEnergies, Jiko Hisensse” umebuniwa mahsusi kuunga mkono msukumo wa Serikali wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.
“Leo tunafuraha kushirikiana na Hisensse kuzindua kampeni hii kubwa itakayodumu hadi Aprili 7, ikiwa na lengo la wazi la kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia,” amesema.
“Kama mnavyojua, mkakati wa taifa unalenga kuhakikisha ifikapo 2034, asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi. TotalEnergies na Hisensse tumeungana kuhakikisha tunawafikia wananchi majumbani mwao na kuwaonesha umuhimu wa matumizi ya nishati safi kwa kuwapatia majiko ya kisasa sambamba na suluhisho la gesi safi.”
Kupitia kampeni hiyo, wateja watakaonunua majiko maalumu ya Hisensse kwa bei ya punguzo watapatiwa mtungi wa gesi wa TotalEnergies bure, ukiwa na vifaa vyote muhimu vya matumizi.
Kwa upande wa Hisensse, kampeni hiyo si tu mkakati wa kukuza biashara, bali pia ni sehemu ya uwajibikaji wa kijamii wa kampuni hiyo. Ofisa Mauzo na Masoko wa Hisensse, Oscar Edgar, amesema mpango huo umeundwa kwa kuzingatia ramani ya taifa ya nishati safi.
“Kama wafanyabiashara wa vifaa vya umeme vya nyumbani na maofisini pamoja na suluhisho za nishati, tuliona ni muhimu kuoanisha juhudi zetu na lengo la Serikali la 2034 la nishati safi,” amesema.
“Tunaamini kwa kuleta bidhaa hizi pamoja, tutawanufaisha kwa kiasi kikubwa Watanzania huku tukisisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia salama na safi za kupikia.”
Wafanyakazi wa TotalEnergies na Hisensse wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya uzinduzi wa kampeni ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia jijini Dar es Salaam.
Mkakati wa Tanzania wa nishati safi ya kupikia umepata msukumo mpya chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kusisitiza nishati safi kama kipaumbele cha afya ya umma na uhifadhi wa mazingira.
Mwaka 2024, Serikali ya Tanzania ilizindua Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034), unaolenga kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa — vyanzo vya nishati vinavyotumiwa na idadi kubwa ya kaya.
Kwa mujibu wa takwimu rasmi, matumizi ya nishati asilia kama kuni na mkaa yanachangia kwa kiasi kikubwa ukataji miti na uchafuzi wa hewa ndani ya nyumba, huku wanawake na watoto wakibeba mzigo mkubwa wa athari za kiafya zinazotokana na kuvuta moshi.
Kupitia uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi, Serikali inalenga kupunguza uharibifu wa mazingira sambamba na kuboresha afya za watu.
Mtaalamu wa nishati, Dk. Deus Ngaruko wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), amesema ushirikiano kama wa TotalEnergies na Hisensse unaonesha jinsi nguvu ya soko inavyoweza kuharakisha utekelezaji wa sera.
“Serikali inaweza kuweka malengo na kuandaa mifumo wezeshi, lakini sekta binafsi ndiyo inayosukuma usambazaji na upokeaji wa teknolojia kwa kiwango kikubwa.
“Pale kampuni zinapobuni ofa zinazopunguza vikwazo vya kuanza kutumia nishati safi, kama kutoa mitungi ya gesi bure au punguzo la bei ya vifaa, zinawafanya wananchi wa kipato cha kati na cha chini waweze kumudu nishati safi.”
Ameongeza kuwa kuoanisha kampeni hiyo na siku ya wapendanao, Kwaresma na Ramadhani ni mbinu inayolenga tabia za msimu za watumiaji.
“Kuunganisha nishati safi na upendo kwa familia kunabadilisha mtazamo, si tu chaguo la kiteknolojia, bali pia ni kitendo cha uwajibikaji na kujali,” amesema.
Wazo hilo linaungwa mkono na mchambuzi wa sera za mazingira, Neema Mwambene, akisema hatua kama hizi zinaonesha kukomaa kwa mazingira ya biashara nchini, ambapo faida na maslahi ya umma vinaanza kukutana.
“Hapo awali kampeni nyingi za kampuni zililenga zaidi kuongeza mauzo. Sasa tunaona kampuni zikirejea wazi mikakati ya taifa na kuoanisha ujumbe wao na vipaumbele vya Serikali. Huu ni mwelekeo chanya.”
Hata hivyo, amesisitiza kuwa mafanikio ya muda mrefu yatategemea uthabiti.
“Ofa za muda mfupi zinasaidia, lakini muhimu zaidi ni upatikanaji wa bei nafuu kwa muda mrefu, minyororo imara ya usambazaji na elimu kwa watumiaji. Kampuni zikidumu katika dhamira hii hata baada ya kampeni, zinaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kufikiwa kwa lengo la 2034.”