Bundi ainyemelea CUF, Msajili awaweka kando kina Lipumba

Dar es Salaam. Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, imebatilisha uchaguzi mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), uliomweka madarakani Profesa Ibrahim Lipumba na viongozi wenzake watano.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Februari 14, 2026 Msaidizi wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza amesema kuanzia Jumatatu ijayo, itatolewa ratiba rasmi ya kuanza mchakato wa kupata uongozi mpya wa chama kwa kipindi cha miaka mitano.

Mbali na Profesa Lipumba wengine walioathirika na uamuzi huo ni Makamu wenyekiti, Mbarouk Seif Salim (Zanzibar), Othman Dunga (Bara), Katibu Mkuu, Husna Mohamed Abdallah, Naibu Katibu Mkuu, Magdalena Sakaya (Bara) na Ali Juma Khamis (Zanzibar).

Sababu ya kubatilishwa kwa uchaguzi huo uliowaweka madarakani ni kuwa, washindi hawakupata zaidi ya nusu ya kura zilizopigwa na wajumbe, kinyume na matakwa ya katiba ya chama, inayohitaji mshindi kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura halali.

Kwa mujibu wa Msajili, mchakato huo ulipaswa kurudiwa.

Hata hivyo, hatua hiyo imekuja kufuatia malalamiko ya wajumbe wa mkutano mkuu wa chama hicho, waliowasilisha pingamizi Desemba 19, 2024, katika Ofisi ya Msajili wakidai kuwapo kwa ukiukwaji wa katiba, kanuni na taratibu za uchaguzi katika mchakato uliofanyika Desemba 18 na 19, 2024 uliomweka madarakani Profesa Lipumba na wenzake.

Wajumbe waliowasilisha malalamiko hayo ni Maftaha Nachuma, Fatuma Athuman, Khamis Khamis Ameir, Ismail Issa Chitutuli, Zuwena Kitatichingi, Liwikula Omari Mohamed, Kassim Mossi Ameir na Ruwaid Abdala Kassim, kupinga mchakato huo kwa madai ya ukiukwaji wa katiba, kanuni na taratibu za uchaguzi katika uchaguzi mkuu wa chama chao uliofanyika Desemba 18 na 19, 2024. 

Katika malalamiko yao, wameeleza kasoro zilizojitokeza ziliathiri uhalali wa matokeo na uteuzi uliofuata, hivyo kufanya uchaguzi mzima kuwa batili.

Wamedai uteuzi wa wagombea, hususan nafasi ya mwenyekiti Taifa, haukuzingatia misingi ya kuepusha mgongano wa masilahi, kwa kuwa baadhi ya wajumbe wa kamati ya utendaji Taifa walikuwa wagombea au walikuwa na masilahi ya moja kwa moja na wagombea.

Pia, wamedai kuwa, zaidi ya theluthi mbili ya wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi Taifa kutoka Zanzibar walisusia uteuzi wa katibu mkuu kwa kutoka nje ya kikao, huku baadhi ya waliobaki wakipigia kura ya kumkataa mteuliwa.

Katika maelezo kwenye barua yao walidai, kanuni za uchaguzi za chama hazitoi fursa ya rufaa kwa mtu ambaye hakuwa mgombea, hata kama ameathiriwa na mchakato huo.

Akizungumza na Mwananchi iliyotaka kujiridhisha kuhusu uamuzi huo Nyahoza ambaye ni Msajili Msaidizi wa Vyama vya Siasa, amekiri ofisini kufikia uamuzi huo, akisema wamejiridhisha pasina shaka madai ya walalamikaji ya hoja na katiba ya chama haikufuatwa.

“Kwa sasa unatambuliwa uongozi uliokuwapo kabla ya uchaguzi huo, ambao utaendelea kuongoza hadi uchaguzi mpya utakapofanyika, kuanzia Jumatatu tutatoa ratiba rasmi ya chama hicho kuanza mchakato wa kuandaa uchaguzi wa kupata viongozi wapya,” amesema.

Alipoulizwa imekuwaje wamechukua muda mrefu kushughulikia madai hayo, Nyahoza amesema Ofisi ya Msajili huchunguza malalamiko yanapowasilishwa na kuchukua hatua pale inapobainika taratibu hazikuzingatiwa.

“Kuchelewa kutangaza uamuzi kulitokana na uchunguzi wa kina uliofanyika kabla ya kufikia hitimisho hilo,” amesema Nyahoza.

Baadhi ya wahusika wa upande wa walioathirika na uamuzi huo, akiwamo Dunga walikiri kuona barua hiyo ya Msajili, ingawa katika maelezo yake alidai hakuna mtu aliyewahi kulalamikia ushindi wake.

“Pia, sijawahi kuitwa na Ofisi ya Msajili kuelezwa malalamiko dhidi yangu wala kusikilizwa. Kwa kweli, sijatendewa haki na sikutegemea ofisi inayoongozwa na mtu mwenye taaluma ya uanazuoni inayoheshimika ifanye makosa ya kiufundi kama hayo,” amesema.

Amesema anachojua rufaa zilizokatwa na wajumbe hao zilikuwa zinahusu nafasi ya uenyekiti, lakini si makamu mwenyekiti jambo analodai haki haijazingatiwa katika kushughulikia jambo hilo.

Amesema kwa kuwa bado yupo nje ya Dar es Salaam, hawezi kutoa uamuzi wowote kwa sasa; hata hivyo, wiki ijayo anatarajiwa kuwasili Dar es Salaam, atatoa uamuzi wake kuhusu hatua iliyochukuliwa na Ofisi ya Msajili.

Mwananchi pia ilipata fursa ya kuongea na Maftaha miongoni mwa waliowasilisha malalamiko kwa Msajili, alisema ameiona barua hiyo na kuthibitisha ni kweli uchaguzi husika haukuzingatia matakwa ya katiba yao pamoja na kanuni zake.

“Barua yake nimeiona na imejibu kile tulichokuwa tunakilalamikia. Katiba na taratibu katika uchaguzi ule zilikiukwa kwa masilahi binafsi. Kwa kweli hatukufurahishwa na yaliyotokea,” amesema Maftaha.

Amesema kukiukwa kwa katiba na kanuni zake ndiko kulikomfanya aondoke katika chama hicho na kujiunga na ACT-Wazalendo.

Amesema ndani ya CUF kulikuwa na uchu wa madaraka badala ya kufuata misingi na taratibu walizojiwekea.

“Kwa sasa nipo katika maisha mapya ndani ya ACT-Wazalendo, sina wasiwasi wowote. Hata hivyo, nakuthibitishia tulipeleka malalamiko hayo tukiwa wajumbe wengi kuhusu uchaguzi huo ambao kwa kweli, ulikuwa batili,” amesema.