390 wakutwa na matatizo ya nyonga Mbeya, 14 wapandikizwa viungo bandia

Mbeya. Watu 600 waliofanyiwa uchunguzi wa matatizo ya nyonga, magoti na mgongo 390 wamekutwa na ugonjwa huo huku 14 wakifanyiwa upasuaji na kupandikizwa viungo bandia.

Hatua hiyo imekuja baada ya kuwepo kwa Kambi ya Madaktari Bingwa kutoka Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) kwa kushirikiana na Hosptali ya Rufaa Kanda ya Mbeya (MZRH) huku ikielezwa asilimia kubwa ni wazee kuanzia umri wa miaka 60.

Daktari Bingwa wa upasuaji wa wagonjwa wa ajali, tiba za mifupa hosptali ya kanda, Dk Baraka Mponda ameiambia Mwananchi leo Jumamosi Februari 14, 2026 wakati akitoa takwimu za wagonjwa waliobainika baada ya kufanyiwa uchunguzi katika kambi hiyo.

“Tangu kambi ilianza Februari 2, 2026 tumewafanyia uchunguzi watu 600, kati ya hao 390, wamebainika na matatizo huku 14 wamefanyiwa upasuaji na kupandikizwa viungo bandia,” amesema.

Dk Mponda amesema idadi kubwa ya wagonjwa walibainika hali zao haziwezi kupata matibabu ya sindano na dawa zaidi ya kufanyiwa upasuaji wakiwepo wazee wenye umri kuanzia miaka 60.

“Tatizo la nyonga na magoti linatokana na viashiria mbalimbali ikiwamo ajali, umri mkubwa na mifupa kusagika, tunashauri jamii kupima afya wanaposikia dalili za maumivu ya miguu au mifupa kufuatia wengi wao kufika hospitali wakiwa na hali mbaya,”amesema.

Kwa upande wake, daktari bingwa wa upasuaji wa mifupa na majeraha na mbobezi kubadilisha nyonga na magoti, Profesa Billy Haonga ametaja moja vichocheo vya kupata matatizo hayo ni pamoja na matumizi holela ya dawa bila kupata ushauri wa daktari.

Haonga ambaye pia ni Profesa Mshiriki wa Chuo Kikuu cha Afya cha Muhimbili, ameitaka jamii hususani wazee kufanya vipimo mara kwa mara na kubainisha hiyo ni kambi ya pili ya kwanza ilifanyika Oktoba 2025a kabla ya uchaguzi mkuu.

Katika hatua nyingine ametaja makundi ambayo yako kwenye hatari ya kupata changamoto hiyo ni pamoja na wachezaji wa mpira, wenye uono hafifu, na umri mkubwa.

Aidha ametaja miongoni mwa dalili ni kushindwa kuchuchumaa,magoti kupata maumivu makali huku waathirika wakubwa wakiwa ni wanawake.

Mnufaika wa kambi hiyo, Emmanuel Mwakyeja (70), Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kirutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Konde Matema Wilaya ya Kyela, amesema alipata ajali Oktoba 23, 2025 na  kuvunjika mguu wa kushoto uliosababisha kupata ulemavu kutokana na nyonga kuharibika.

“Tatizo lilikuwa kubwa sehemu ya nyonga, lakini nashukuru Serikali na uongozi wa hosptali ya kanda kwani imerejesha matumaini baada ya kupata matibabu ya kina na kufanyiwa upasuaji na sasa maendeleo yangu mazuri,” amesema.