Sh45 bilioni zitakavyotumika 2026/27 Simanjiro

Simanjiro. Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, mkoani Manyara, wamepitisha Sh45 bilioni kwa ajili ya rasimu wa mpango wa bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2026/2027.

Ofisa mipango wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Happy Masatu akisoma mpango huo wa makisio ya bajeti leo Jumamosi Februari 14, 2026 amesema umelenga kufanikisha miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwamo ya elimu, afya, kilimo na mifugo.  

Amesema mpango huo wa rasimu ya bajeti ya mwaka wa fedha wa 2026/2027 umeandaliwa kwa kuzingatia sheria, sera, mikakati ya halmashauri na miongozo ya kiserikali.

“Mpango umelenga muongozo wa maandalizi ya mpango wa bajeti ya Serikali kwa mwaka 2026/2027, hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan akifungua Bunge la 13, ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na vipaumbele vya halmashauri,” amesema Masatu.

Amesema mapato ya ndani ya halmashauri hiyo yameongezeka maeneo ya ushuru wa mchanga, mazao ya biashara na chakula, minada, masoko standi ya magari, kodi ya huduma, ushuru, wa trekta na uuzaji wa viwanja. 

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Kaleiya Mollel amesema madiwani washirikiane na watumishi wa halmashauri katika kuteketeza miradi mbalimbali ya maendeleo.

“Watu kule kwenye kata zetu wana matarajio makubwa katika kupata huduma za muhimu kupitia bajeti ya mwaka huu kwenye sekta ya afya, elimu, maji, miundombinu ya barabara na mengineyo,” amesema Mollel.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Dominika Ngaleka amewashukuru madiwani hao kwa kupitisha mpango huo wa bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2026/2027.

“Tunatarajia watumishi wa halmashauri watashirikiana na madiwani wetu ili kuhakikisha utekelezaji wa mpango wa bajeti ya mwaka wa fedha wa 2026/2027 unatekelezeka ipasavyo,” amesema Ngaleka.

Diwani wa Endiamtu, Lucas Zacharia amepongeza bajeti hiyo katika suala la kuendeleza soko la madini, Mirerani Tanzanite City ili kuimarisha biashara ya madini.

Diwani wa Shambarai, Julius Lemboi amepongeza mpango wa bajeti hiyo akisema  itakidhi matarajio ya wana Simanjiro katika miradi mbalimbali ya maendeleo.

Diwani wa Mirerani, Salome Mnyawi, amesema anatarajia kupitia mpango wa bajeti hiyo ya mwaka wa fedha wa 2026/2027 utakamilisha choo cha kituo cha afya Mirerani (Tanzanite) ili kianze kufanya kazi kwa kutoa huduma za afya kwa jamii.

Mkazi wa mji mdogo wa Orkesumet, Elivis John amesema kupitia mpango huo wa bajeti ya mwaka 2026/2027 anatarajia wakazi wa Wilaya ya Simanjiro kuendelea kunufaika katika miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo sekta ya afya, elimu na mengineyo.