RAIS wa Yanga, Hersi Said amesema mchakato wa ujenzi wa uwanja wa klabu hiyo utakaojengwa Jangwani umefikia hatua nzuri baada ya kupokea mchoro wa kwanza wa mradi huo.
Akizungumza mjini Zanzibar katika mwendelezo wa vikao vya Kamati ya Utendaji ya Yanga, Hersi amesema tayari klabu imepata mshirikw katika utekelezaji wa mradi huo, akibainisha mahitaji mahsusi ya uwanja wanaoutaka.
“Mradi wa uwanja ambao utajengwa kwenye ardhi ya Jangwani, mita 250, tayari tumetangaza wa kushirikiana naye na tumemwandikia nini hasa tunataka kwenye uwanja huo,” amesema Hersi.
Amongeza kuwa kampuni ya GSM imewahakikishia upatikanaji wa fedha kwa ajili ya kuanza hatua ya kwanza ya majengo, huku akisisitiza kuwa ndani ya wiki moja watakutana tena kamati ya utendaji kujua imefika wapi.
“Dhamira ni kukusanya fedha kwa ajili ya kuanza utekelezaji. Ndani ya wiki moja tunatarajia hatua ya kwanza ya majengo iwe imekamilika kwenye maandalizi yake,” amesema.
Hersi amesema kupokewa kwa mchoro wa kwanza ni ishara kuwa ndoto ya muda mrefu ya Wanayanga sasa inakwenda kutimia, kwani mradi huo haujawahi kukamilika tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo 1935.
“Leo tumepokea mchoro wa kwanza. Hii inakwenda kuwa historia. Mradi huu haujawahi kukamilika tangu kuanzishwa kwa Yanga. Sasa tunaenda kuujenga uwanja wa kihistoria na kutimiza ndoto ya Wanayanga,” amesema kwa msisitizo.
Amebainisha kuwa baada ya kupatikana kwa mchoro kamili, mkataba utaainisha majukumu ya kila upande, huku wiki ijayo wakitarajia kujadili gharama za mradi kwenye hatua ya pili.
Kuhusu ushiriki wa mdhamini, Kampuni ya GSM, Hersi amesema hadi sasa hawajasaini mkataba rasmi wa ujenzi, lakini kampuni hiyo imeshinda zabuni ya kutekeleza mradi huo na imewahakikishia kuwa fedha zipo tayari kwa kuanza kazi pindi taratibu zitakapokamilika.
“Hatujasaini mkataba na GSM, lakini yeye ameshinda tenda ya ujenzi. Ametuhakikishia kuwa pesa ipo na kila kitu kikikamilika, mradi utaanza mara moja,” amesema.
“Mkataba utaainisha majukumu. Baada ya kikao cha leo, ndani ya wiki moja mambo yawe yamekalilika, na wiki inayofuata tutakaa kuzungumzia gharama za mradi kwenye hatua ya pili,” amesema.
Wiki mbili zilizopita, Yanga ilitangaza kuwa GSM ndiyo mshindi wa zabuni ya ujenzi wa uwanja huo.