Usimkatie tamaa mtoto mtukutu, fanya haya

Katika safari ya malezi karibu kila mzazi hukutana na changamoto ya kulea mtoto anayejulikana kama ‘mtukutu.’

Huyu ni mtoto anayependa ukaidi, anayeonekana kutosikiliza maelekezo, anayejibu bila hofu au anayevuka mipaka ya malezi inayotarajiwa na family au majirani na watu wengine.

Mara nyingi mtoto wa aina hii huibua hisia za hasira, fedheha au kukata tamaa kwa mzazi, hasa pale tabia hizo zinapojirudia hadharani au shuleni.

Hata hivyo, ni muhimu kwa mzazi kufahamu kuwa utukutu si tabia ya kuzaliwa nayo, bali ni ishara ya jambo fulani linalomsumbua mtoto.

Katika jamii zetu, mtoto mtukutu hupewa taswira hasi mapema. Maneno kama hana adabu, hana akili au hatokuja kuwa lolote, hutamkwa hadharani bila kujali athari zake. Kauli hizi humuumiza mtoto kisaikolojia na kumjengea dhana kuwa yeye si wa maana. Kadiri anavyoamini kuwa hawezi kubadilika, ndivyo anavyozidi kuonyesha tabia ile ile, kama njia ya kujilinda au kuonyesha maumivu yake kwa vitendo.

Wataalamu wa malezi wanaeleza kuwa kwa watoto wengi, utukutu ni lugha ya hisia. Mtoto anaweza kuwa na hasira, wivu, hofu au upweke, lakini hana uwezo wa kuyawekea hisia hayo katika maneno.

Badala yake, hujitokeza kwa kupiga kelele, kugombana, kuvunja vitu au kukaidi maelekezo. Ndiyo maana adhabu kali peke yake haimalizi tatizo, bali huongeza ukuta kati ya mzazi na mtoto.

Hatua ya kwanza kwa mzazi ni kubadili mtazamo. Badala ya kuangalia tabia tu, bali aangalie sababu iliyo nyuma ya tabia.

Mtoto anapofanya kosa, mzazi jaribu kuzungumza naye kwa utulivu na kumsikiliza. Kusikiliza hakumaanishi kuhalalisha kosa, bali ni kumpa mtoto nafasi ya kujieleza na kujisikia kuthaminiwa. Mtoto anayesikilizwa huwa tayari zaidi kubadilika kuliko anayehukumiwa kila wakati.

Pili, nidhamu ijengwe juu ya upendo na uthabiti. Nidhamu si kipigo, matusi wala vitisho. Ni mchakato wa kumfundisha mtoto kutambua mipaka na kuwajibika kwa matendo yake.

Hivyo mzazi anapaswa kuweka misimamo inayoeleweka sambamba na kitu kama masharti kwake ya wazi na yanayo eleweka, pamoja na matokeo yake.

Masharti hayo yaelekezwe kwa haki na bila upendeleo, ili mtoto ajifunze kuwa kila tendo lina athari chanya na hasi.

Lakini mzazi pia anapaswa kuwa kielelezo bora. Mtoto huiga zaidi anachokiona kuliko anachoambiwa. Mzazi anayependa kupandwa na hasira, kupiga kelele au kudharau wengine, humfundisha mtoto tabia hizo bila kujua.

Ikiwa mzazi anatamani mtoto wake awe mpole, mvumilivu na mwenye heshima, ni lazima aanze kuonyesha sifa hizo katika maisha ya kila siku.

Kwa sababu mzazi anapaswa kutambua na kuendeleza vipaji vya mtoto wake. Watoto wengi wanaoitwa watukutu huwa na nguvu nyingi, ubunifu na ujasiri mkubwa.

Wengine ni viongozi kwa asili, wachunguzi au wapenda kuuliza maswali mengi. Badala ya kuzima sifa hizi kwa lawama, mzazi azielekeze kwenye michezo, sanaa, masomo au shughuli za kijamii zitakazomsaidia mtoto kutumia nguvu zake kwa njia chanya.

Na asisisite kutafuta msaada pale inapobidi. Kuna wakati utukutu wa mtoto unaweza kuwa dalili ya changamoto kubwa zaidi kama msongo wa mawazo, matatizo ya kujifunza au changamoto za kihisia.

Kuzungumza na mwalimu, mshauri wa nasaha au mtaalamu wa saikolojia ya watoto si dalili ya kushindwa, bali ni ishara ya mzazi anayejali mustakabali wa mtoto wake.

Kwa sababu mzazi anapaswa kumbuka kuwa mtoto mtukutu anahitaji upendo mara dufu. Anahitaji mzazi anayemwamini, anayemwelekeza na anayempa matumaini. Kukata tamaa ni rahisi, lakini kulea kwa subira, hekima na huruma ndiko kunakojenga taifa lenye watu wazima wanaojiamini na kuwajibika. Mtoto akipewa mazingira sahihi leo, kesho anaweza kuwa kiongozi bora anayejivunia malezi aliyopata.