Upepo ulivyobadilika Chaumma, kwafukuta | Mwananchi

Dar es Salaam. Baada ya miezi kadhaa ya ukwasi wa ghafla, Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), kinadaiwa kuangukia katika hali ya ukata, migongano ya wanachama na viongozi huku maswali lukuki yakikosa majibu.

Mabadiliko hayo ya hali ya uchumi wa chama hicho, yamesababisha baadhi ya wanachama wake, wadai taarifa ya mapato na matumizi, kujua kiasi kilichotumika na kilichobakia baada ya shughuli za uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Kwa mujibu wa wanachama, kila inapotakiwa taarifa ya mapato na matumizi ya chama hicho, kumekuwa na kigugumizi kutoka kwa viongozi wao, jambo linaloibua wasiwasi na mgawanyiko miongoni mwa wanachama.

Katikati ya madai hayo, uongozi wa chama hicho, unasema hakuna chama kinachotoa taarifa ya mapato na matumizi yake kwa mwanachama mmoja mmoja akiwa nyumbani na anayedai hajapewa taarifa hiyo, aseme ni mjumbe wa kikao gani.

Uongozi huo, umekana kuwepo mgongano na ukimya ndani ya chama hicho, ukisema kuna shughuli za usiku na mchana zinazoendelea kupambania uhai na ustawi wa chama hicho.

Yote hayo yanayoibuka sasa, yanatokana na kumbukumbu za kishindo kilichooneshwa na Chaumma kabla na wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka 2025, ikifanya ziara kwa helikopta na kukodi kumbi za gharama katika matukio yake.

Katika kipindi hicho, Chaumma iliyokuwa ikifanya mikutano yake ya kitaifa katika kumbi ndogo, ikageuka na kufanyia katika hoteli na kumbi za gharama, huku ziara zake zikihusisha msafara wa magari na chopa, hali iliyoibua maswali ni wapi imepata utajiri huo wa ghafla.

Wimbi hilo la ukwasi wa Chaumma, liliambatana na kuvuna maelfu ya wanachama waliohama Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), na kupokewa kwa kishindo katika kumbi za gharama.

Ukwasi na idadi ya wanachama, ilikilazimu chama hata kuhamisha makao makuu ya ofisi hiyo kutoka Mwananyamala na sasa ipo Kinondoni Biafra jijini Dar es Salaam.

Sintofahamu na maswali lukuki, yanaibuka sasa baada ya ukimya wa chama hicho tangu ulipomalizika uchaguzi huo uliofanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025 huku  viongozi wake, wakisikika kwa nadra.

Katika uchaguzi huo, Chaumma iliiambulia mbunge mmoja, Agnesta Kaiza wa Segerea Dar es Salaam na wabunge wawili wa viti maalumu, Devotha Minja na Sigrada Mligo.

Kigugumizi mapato na matumizi

Mmoja wa wanachama na kiongozi wa chama hicho aliyeomba hifadhi ya jina lake kwa kuwa si msemaji, amesema mgongano uliopo unatokana na kutopatikana jibu kuhusu zilikotoka fedha zilizokuwa zinatumika wakati wa uchaguzi.

Amesema wanachama mara kadhaa wamekuwa wakiomba taarifa ya mapato na matumizi ya chama hicho kujua kiasi kilichotumika na kilichobaki, lakini uongozi unapata kigugumizi kutoa jawabu.

“Kwa sasa kila mmoja anahoji mapato na matumizi ya fedha wakati wa uchaguzi. Wanataka kujua kiasi gani kiliingizwa na kilichobaki, jambo ambalo kumekuwa na kigugumizi kutoka kwa viongozi,” amesema.

Amesema hoja ya taarifa ya mapato na matumizi, inatokana na kukithiri kwa ukata ndani ya chama hicho kwa sasa, kiasi cha kushindwa kufanya shughuli mbalimbali, ilhali chama kilikuwa na fedha nyingi wakati wa uchaguzi.

“Hakuna shughuli za chama zinazoendelea kwa kuwa, kwa sasa hakuna umoja wala fedha. Kungekuwa na umoja tungechangishana ili tufanye shughuli za chama, lakini kila mtu yuko kivyake,” amesema.

Mwanachama huyo amesema hata fedha zilizotolewa kwa ajili ya kusaidia kampeni kwa wagombea ubunge, hawakupewa kama wanavyostahili.

“Walikuwa wanaangalia hadhi ya mgombea, kama ana jina kubwa, anapewa Sh milioni 10 hadi 15, lakini akiwa sio maarufu anapewa hata Sh milioni 5. Hii ilisababisha manung’uniko,” amesema.

Alipotafutwa kuzungumzia hilo, Naibu Katibu Mkuu wa Chaumma Bara, Benson Kigaila amesema hakuna chama kinachotoa taarifa ya mapato na matumizi yake kwa mwanachama mmoja mmoja akiwa nyumbani na kwamba anayedai hajapewa taarifa hiyo, aseme ni mjumbe wa kikao gani.

“Kuna chama kinachotoa taarifa ya mapato na matumizi kwa kila mwanachama mmoja mmoja akiwa nyumbani? Huyo anayesema ni mwanachama aseme anashiriki kikao gani, ameomba hiyo taarifa katika kikao kipi?

“Anataka taarifa za fedha yeye amechangia kiasi gani kwa chama. Huyo mwanachama aliyekwambia alikuwa chama gani kabla? Nilishavuka kujadili mambo madogo madogo, kuniuliza mambo ya watu wajinga ambao hawana shughuli za kufanya,” amesema Kigaila.

Mwananchi ilimtafuta Makamu Mwenyekiti wa Chaumma Bara, Devotha Minja ambaye amesema chama hicho kina idara ya fedha na ndiyo yenye mamlaka ya kuzungumza kuhusu mapato na matumizi.

“Sio kila mtu anaweza kuongea au kupewa taarifa ya mapato na matumizi, idara ipo kwa ajili ya masuala ya fedha yenyewe inaweza kutoa taarifa lakini sio kwa kila mtu,” amesema.

Mei 2025, katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Kigaila alivyoulizwa Chaumma wanapata wapi fedha hadi kuwapata jeuri ya kurusha chopa amesema:“Chadema tulikuwa tunarusha chopa hatukuwahi kuulizwa fedha tunatoa wapi? Tumehamisha chama tumeleta Chaumma tukirusha chopa unatuuliza tunarusha fedha tumetoa wapi.”

Amesema wanajua kuzisaka fedha na wale waliokuwa wanawasaidia wakiwa Chadema ndiyo hao hao wanawasaidia wakiwa Chaumma.

Kada mwingine ambaye pia ana wadhifa ndani ya Chaumma, amedai kila mtu yupo kivyake ndani ya chama hicho, si kama ilivyokuwa awali.

“Ukiwaona viongozi utaona kama vile wapo pamoja, lakini ni danganya toto si uhalisia wa mambo yalivyo ndani. Kwa kifupi kuna mpasuko wa kutoelewana viongozi kwa viongozi pamoja na wanachama,” amesema.

“Hatuoni ‘future’ ya chama zaidi ya viongozi wanatuhumiana tu, hakuna kitu kinachoendelea tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu, hakuna shughuli za chama. Ni kama vile chama kinakwenda kufika mwisho,” amesema mmoja wa viongozi wa chama hicho.

Amesema kuna mgogoro unaendelea chini kwa chini siku si nyingi utaibuka hadharani, kwa kuwa waliohamia chama hicho kutoka Chadema, wengi wamejitenga na Chaumma wanafanya mambo yao binafsi.

“Baadhi ya wale waliokuwa Chadema na kuhamia Chaumma kila mtu sasa hivi yupo ‘busy’ na mambo yake hajishughulishi na mambo ya chama maana hawaoni mwelekeo. Siku chache zijazo mtaanza kuwasikia baadhi yao wakitangaza mustakabali wao kisiasa,” amesema.

Hata hivyo, yanayoelezwa na wanachama hao, yaliwahi kuzungumzwa na Patrick Assenga, kada wa Chaumma aliyetoka Chadema, akisema yuko mbioni kurudi Chadema kwa kuwa, chama chake cha sasa kimepoteza mwelekeo.

“Siku chache zijazo nitatangaza rasmi uamuzi wangu wa kurudi nyumbani Chadema kuendeleza mapambano. Kwa umri wangu siwezi kustaafu siasa,” alisema Assenga.

 “Unakuta kinashiriki vikao vya vyama vya mkakati, lakini unaona kabisa kimepoteza mwelekeo. Badala ya kushughulika na chama tawala, inajihusisha zaidi na vyama vingine vya siasa.”

Alisema Chaumma imepoteza hewa ya oksijeni na kilichobaki ni kifo, akieleza kuwa chama cha siasa kinategemea watu na kinapaswa kuonesha ukaribu na wananchi, hasa wanapopitia shida.

Hata kada mwingine wa Chaumma aliyewahi kuzungumza na Mwananchi, Henry Kileo alisema kwa sasa hajihusishi na masuala ya siasa na amejiingiza katika shughuli za biashara ili kurejesha hasara aliyopata katika uchaguzi.

“Nimekaa mbali na siasa, sijui chochote. Niko na biashara zangu tangu tumalize uchaguzi. Mambo yanayoendelea siyajui, sijaongea na wanachama, na siingii katika majukwaa kabisa,” alisema.

Alipoulizwa kama yuko tayari kurudi Chaumma, alisema: “Nikiwa tayari nitajua cha kufanya, lakini kwa sasa niko bize na shughuli zangu. Ndiyo maana sifuatilii kinachoendelea.”

Akijibu hilo, Kigaila amehoji wamegongania wapi, mgongano ukoje, unamhusisha nani na nani?

“Mimi sijui kuhusu mgongano wowote, anayesema kuna mgongano wa nani na nani, mgongano ukoje, wamegongania wapi? Wasilete maneno maneno,” amesema.

Kuhusu ukimya na kukosekana mipango ya baadaye ndani ya chama hicho, Kigaila amehoji ni nani anayepanga mipango kati ya mwanachama wa kawaida na viongozi.

Kigaila alisema kama anayelalamikia kutokuwepo kwa mipango ni mwanachama wa kawaida, anajuaje ilhali yeye si sehemu ya wapanga mipango ya chama.

Amehoji, anayedai Chaumma haina mipango ya baadaye, anaijua mipango ya chama gani kingine nchini.

“Anayesema hakuna mipango anajua mipango inapangwa na nani? Mipango inapangwa na viongozi, yeye mwanachama wa kawaida anajuaje.

“Sisi tunafanya kazi ya kujenga chama, wanaoandika katika mitandao waache waandike kwa sababu kalamu na mabando ni yao,” amesema.

Devotha ambaye ni mbunge wa viti maalumu, amesema viongozi wa chama hicho wanapambana usiku na mchana kuhakikisha chama kinasonga na hilo wamefanikiwa.

Amesema yapo mambo yanayohitaji vikao kama mkutano mkuu na vingine vinavyohusisha uwakilishi wa wanachama wote, bado havikufanyika baada ya uchaguzi.

Hata hivyo, amesema kilichosababisha visifanyike ni tukio la Oktoba 29 na 30, lililoleta mshtuko kwa Taifa na chama hicho kilipata msukosuko pia.

“Chama ni kama kilichanganyikiwa na hii ni karibu kila mtu nchini. Kama kuna watu wanalalamika vikao vilikaliwa wazungumze kwenye vikao,” amesema Devotha.

Amesema hivi karibuni, Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi alikuwa na kikao na vyama vyote na Mwenyekiti wa Chaumma, Hashimu Rungwe maarufu Mzee wa Ubwabwa na Katibu Mkuu wake, Salum Mwalimu walihudhuria.

“Sasa unasemaje chama kimedhoofika wakati kinashiriki vikao, kinafanya shughuli ndogondogo. Naona kuna wanataka kutupiga kuturudisha nyuma, lakini hata kwa udogo na uchache wetu tutasonga,” amesema.