Mido Barberian aona mwanga Championship

KIUNGO wa Barberian FC, Muhsin Mlaga, amesema licha ya mwenendo usioridhisha kwa timu hiyo katika Ligi ya Championship hadi sasa msimu huu, ila bado wana nafasi ya kurekebisha changamoto mbalimbali, ikiwemo za kutumia vyema nafasi kufunga.

Nyota huyo anayemudu kucheza kiungo wa ukabaji na ushambuliaji aliyehusishwa kutua Simba katika dirisha dogo la Januari 2026, amesema kikosi hicho kinakosa balansi nzuri katika eneo la kujilinda na kushambulia, jambo linalowagharimu zaidi.

“Ushindani ni mkubwa sana hasa raundi hii ya pili lakini tutaendelea kupambana kwa kushirikiana na wachezaji wenzangu, lengo ni kuhakikisha tunaepuka janga la kuishusha timu daraja, naamini mechi 12, zitatuongezea motisha,” amesema Mlaga.

Nyota huyo kabla ya kutua Barberian, aliichezea pia Ndanda, huku akianzia katika kituo cha Michezo cha Kapteni (Captain Sports Centre), ambacho ni cha aliyekuwa kocha na mchezaji wa Majimaji, Yanga, Mtibwa Sugar na KenGold, Omary Kapilima.

Barberian iliyokuwa ikifahamika kwa jina la Kiluvya United, inashika nafasi ya 16, katika msimamo na pointi tisa, baada ya timu hiyo kushinda mechi moja tu, sare sita na kupoteza 11, kati ya 18, iliyocheza, ikifunga mabao 10 na kuruhusu 29.