Boli la Gomez lashtua mastaa Simba

MSHAMBULIAJI wa Simba, Seleman Mwalimu ‘Gomez’ sio chaguo la kwanza la washambuliaji wa kikosi cha timu hiyo, lakini kiwango anachokionyesha kimewastajabisha mastaa waliofichua sababu inayosababisha nyota huyo aliyepo kwa mkopo kutokea Wydad Casablanca asiwe panga pangua.

Gomez ambaye msimu uliopita alikuwa akiitumikia Fountain Gate kwa mkopo kutokea Singida Black Stars iliyomuuza katika dirisha dogo la msimu huo kwa Wydad kabla ya Simba kumrejesha msimu huu, hadi sasa amefunga mabao matatu katika Ligi Kuu, likiwamo la juzi dhidi ya KMC walipoilaza 2-0.

Hata hivyo, licha ya kutokuwa kikosi cha kwanza, lakini Gomez amekuwa na mwendelezo mzuri ambao umemfanya mshambuliaji wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Emmanuel Gabriel ‘Batgol’ kusema: “Mwalimu ana uwezo wa kucheza namba zote za mbele kwa maana ya kulia, kushoto na kati, ana mwendo na nguvu, hivyo namuona anastahili kuaminiwa kwa faida ya huduma yake katika timu.

“Kwa nini haanzi kikosi cha kwanza hilo ni suala la makocha wenyewe. Pia viongozi wakiona ni mchezaji mzuri wanaweza wakahoji. Ukiona kunakuwa kimya hilo pia ni tatizo lingine na kinachombeba ni CV yake ya kucheza Wydad Casablanca,” alisema Gabriel.

“Nilichokiona Simba viongozi hawana uvumilivu na wachezaji vijana. Wanawasajili wengi wakicheza msimu wa kwanza wanawaacha. Pia hawajawaruhusu wachezaji kuambiana ukweli, mfano alikuwa Fabrice Ngoma kabla ya kuondoka alionekana moja ya video akimsema kipa Moussa Camara kutokana na makosa yake, Simba ikamuondoa.

“Hadi sasa sijaona namba sita wa Simba aliye imara kama alivyokuwa Ngoma ambaye angekuwepo wangetengeneza pacha nzuri sana na Shomari Kapombe. Pia katika kusajili wasiondoe wachezaji kwa mkupuo na kusajili upya kila wakati, hilo halileta afya pia mchezaji mzawa akionyesha kiwango wakiheshimu.

“Jambo la mwisho ninaloliona viongozi wa Simba wasipoacha migogoro ya ndani kwa ndani timu itapotea katika ramani ya ushindani, hicho ni kitu kibaya hiyo ni klabu iliyo na mashabiki wengi wanaoumia, tukiwaambia ukweli wanatuona tuna njaa.”

Kiungo wa zamani wa Simba na Taifa Stars, Shabaan Kisiga alisema: “Mwalimu ni mchezaji mzuri sana azidi kuongeza umakini na bidii bila kukata tamaa, kocha ndiye mwenye maamuzi ya mwisho, huenda kwa sasa anampa programu ya kutomchezesha dakika 90 siku akimuona anafiti ataanza tu na bado ana umri wa kucheza muda mrefu.”

Naye staa wa zamani wa Simba, Azam FC na Stars, Ramadhan Chombo ‘Redondo’ alisema: “Mwalimu ana talenti kubwa, kwanza yeye mwenyewe anapaswa kupambana bila kukata tamaa, kuanza ama kutoanza kikosi cha kwanza kocha ndiye mwenye uamuzi, ila huduma yake itaifaa Simba endapo wakimwamini na kumjengea kujiamini.”