Simulizi mapito ya mama anayeendesha bajaji Dar

Dar es Salaam. Kuna wakati maisha yanakufikisha mahali unahisi umefika mwisho, biashara zinaanguka. Madeni yanakaza shingo. Mawazo ya kuzima simu yanazunguka akili, huku usaliti wa uliowaamini ukikuzungusha siku nzima.

Licha ya mambo hayo yote, wapo wapambanaji wa jasho na damu walioamini hata katikati ya giza nene kuna mwanga.

Haya yanaakisi simulizi ya maisha ya Zuwena Mnemo, mzaliwa wa Ifunda, Iringa, aliyekuja Dar es Salaam kutafuta maisha kama maelfu ya watu wengine.

Alifanya kila aina ya biashara ikiwepo uuzaji wa maji ya kufunga maarufu kama ‘maji ya Kandoro’, soda, vocha, nyanya kutoka Iringa na viazi kutoka Njombe. Hata hivyo, mwisho wa siku aliambulia maumivu.

Baada ya biashara kadhaa kuyumba, alijiunga na vikoba akiamini kuwa huo ndio ungekuwa ukombozi wake. Hivyo, alichukua mkopo na kununua bajaji, akamkabidhi kijana mmoja afanyie kazi kwa mkataba kwa makubaliano ya kupeleka hesabu kila siku ili kulipa rejesho la mkopo.

Mwanzoni mambo yalionekana kwenda vizuri na hata akaona mwanga wa maisha yake kupitia biashara ya bajaji aliyokopa.

“Yule kijana alifanya kazi kwa uaminifu miezi miwili au mitatu akiniletea kila siku Sh10,000 kama tulivyokubaliana, baadaye akaanza kunisumbua anakaa haleti pesa nikimtafuta sana ananitumia Sh100,000, halafu anapotea zaidi ya wiki mbili,” anasimulia.

Kadri siku zilivyopita, anasema mawasiliano yakakatika na alipokuwa akimtafuta kupitia kwa mama yake ambaye alikuwa mdhamini wake, naye hakuwa na majibu ya uhakika na kumtaka kutumia njia zake.

Wakati huo, anasema bado alikuwa akiendelea na biashara ya nyanya kati ya Iringa na Dar es Salaam, lakini nayo ikayumba. “Hali ikawa ngumu biashara hakuna, bajaji hailipi, mkopo wa vikoba unamsubiri.”

Zuwena anasema deni likabaki mabegani mwake, bajaji haionekani, Polisi hawatoi msaada wa kuridhisha, watu wanamwambia huenda tayari imeuzwa lakini hakukata tamaa.

Siku moja asubuhi, kama ilivyokuwa desturi yake, Zuwena aliamka mapema saa 11 alfajiri na kuanza tena mzunguko wake wa kuitafuta bajaji yake.

Anasema alishuka Mawasiliano na kuanza kutembea kwa miguu kuelekea Sinza hadi Palestina, macho yake yakichunguza kwa makini kila bajaji nyeusi iliyokuwa ikipita au kuegeshwa pembeni ya barabara.

Hakuwa na hakika kama angeiona, lakini moyo wake ulikataa kukata tamaa. Ghafla, macho yake yakatua kwenye bajaji moja iliyokuwa imeegeshwa eneo la Mugabe, Sinza.

Zuwena Mnemo akizungumza na mwandishi wa gazeti la Mwananchi Devotha Kihwelo.



“Nilisogea na kuitazama kwa makini nikaangalia namba nikasema haiwezekani siku zote nimehangaika hadi nilikuwa navaa nguo kwa kuficha sura ili madereva wenziwe wasinijue na kumpa taarifa,”anasema.

Anasema kwa sekunde chache alibaki amesimama, moyo ukidunda kwa nguvu kwani aliwahi kuambiwa mara nyingi kuwa huenda bajaji hiyo ilishauzwa na kupelekwa mkoani, hivyo hakuamini alichokuwa anakiona kisha bila kuleta taharuki akaisogelea na kuingia ndani, akakaa kimya kana kwamba ni abiria wa kawaida.

“Muda mfupi alikuja kijana tofauti na niliyemkabidhi bajaji nikafunua uso kijana alishtuka na kuniuliza mama umekuja kumtafuta fulani? Nilimjibu hapana nimetoka hospitali nina ndugu yangu amejifungua, hivyo nilikuwa kwenye daladala nilivyoiona hii nikashuka,” anasema.

Kwa kuwa alishaiona bajaji yake alimuuliza kijana kumpeleka Tabata ni kiasi gani na alimtajia Sh15,000 hivyo safari ya kuelekea huko ikaanza huku njiani wakiwa na mazungumzo kadhaa ya dereva wake kutopeleka hesabu.

Baada ya kufika nyumbani alimwambia dereva aiache bajaji kwa sababu ni yake na haikuwa inamlipa, ghafla kijana alikuwa mkali na kufikia hatua ya kumkunja nguo, lakini alipata ujasiri wa kutoa funguo na kumtishia kelele za mwizi.

Baada ya kukumbwa na changamoto za kifamilia na kupoteza mwelekeo wa kibiashara, mwanamke huyu alijikuta hana kazi wala kipato cha uhakika, watoto watatu walikuwa wakimtegemea.

“Nilikuwa sina biashara, sina kazi, bajaji ndiyo imekuja kuwa mkombozi wangu baada ya kusumbuka kwa muda mrefu na kupitia magumu mengi,” anasimulia.

Awali, anasema alinunua bajaji kwa Sh7 milioni, wakati huo alikopa Sh10 milioni, hivyo hakutamani tena kuendelea na bajaji ambayo imempa misukosuko, hivyo aliamua kuiuza kwa fedha ya chini ambayo haikumwezesha kununua bajaji nyingine.

Hata hivyo, anasema kiasi cha fedha alichokuwa nacho ilibidi aongezee kwa kwenda kukopa pesa benki ambayo imemsaidia kupata bajaji mpya ambayo anaitumia kwa sasa.

“Nilikuwa nalipa kila wiki, haikuwa rahisi, lakini nimepambana hadi nimemaliza na sasa naendelea kujivunia kwa kazi yangu,” anasema.

Kabla ya kuingia barabarani, anasema alilazimika kujifunza kuendesha bajaji, alimtafuta mtu wa kumfundisha, akamlipa, akachukua leseni akijua hiyo ndiyo tiketi yake ya kuingia rasmi kwenye maisha mapya.

“Licha ya mwanzo kuwa mgumu kwa kudhihakiwa, kutukanwa na baadhi ya vijana waliodhani mwanamke hafai kuwa dereva wa bajaji nilipambana mpaka sasa nimekomaa barabarani.”

“Unakuta kijana anakwambia ‘mama, si ukae nyumbani upike?’ Lakini nilijua napigania maisha ya watoto wangu.”

Wakati mwingine, anasema alilazimika kwenda Kituo cha Polisi baada ya kunyanyaswa au kunyang’anywa wateja.

Zuwena anasema kuna kipindi aliingia kwenye kijiwe cha madereva na kulia kwa sababu ya manyanyaso na ugumu wa kazi. Lakini msaada wa dereva mmoja mwema ulimpa nafasi ya kukubalika.

“Nilikuwa mwanamke peke yangu pale, leo hii tuko wengi wamezoea kuniona.”

Anasema ana zaidi ya miaka sita sasa barabarani, heshima imeanza kurudi na vijana waliokuwa wakimcheka leo wanamuita mama.

Zuwena ni mama wa watoto watatu, mmoja yupo chuoni akisomea masomo ya Tehama (IT), mwingine yupo sekondari mkoani Dodoma na mdogo yupo darasa la sita.

Zuwena Mnemo akiondoka katika kijiwe cha External kwa ajili ya kupeleka abiria.



“Niliamua kuingia barabarani kwa sababu nilijua watoto wangu lazima wasome leo mmoja yuko chuo, namshukuru Mungu.”

Anasema mtoto wake mkubwa amemwambia akimaliza kusoma watafungua duka la vifaa vya ofisini na shuleni, hilo ndilo linalompa nguvu kila siku kuamka alfajiri na kushika usukani.

Licha ya mafanikio hayo, ndoto yake haijaishia kwenye bajaji, anasema anatamani siku moja awe na gari kubwa hata yale ya abiria aina ya Coaster ili afanye safari za mikoani na kuajiri wengine.

Anasema hata kama watoto wake watamaliza shule na kupata ajira, ataendelea kupambana kwa sababu amezoea kujitegemea.

Hata hivyo, ametoa wito kwa wanawake wanaodharau kazi ngumu au kuogopa mitazamo ya jamii, wapambane wasione aibu.