Ni dawa, sumu au biashara? Mlipuko wa maduka ya tiba asili

Dar es Salaam. Kuna jambo lisilo la kawaida linaloendelea katika miji mikuu ya Tanzania. Ongezeko la kasi la maduka ya dawa za asili.

Hali hii inajitokeza wakati ambapo nchi imekuwa ikipiga hatua kubwa, katika huduma za afya za kisasa.

Katika muongo mmoja uliopita, Tanzania imepanua uwezo wa kutoa matibabu maalumu, yakiwemo huduma za saratani, upandikizaji wa figo, upasuaji wa moyo, upasuaji wa neva, upandikizaji wa uboho na huduma za upandikizaji wa viinitete (IVF), miongoni mwa nyinginezo.

Maendeleo haya, yaliyoambatana na mkakati wa kuitangaza Tanzania kama kitovu cha utalii wa tiba katika ukanda huu, yalitarajiwa kupunguza utegemezi wa tiba mbadala. Hata hivyo, hali inaonekana kuwa kinyume.

Dawa za asili si tu kwamba bado zinatumika kwa kiwango kikubwa, bali katika baadhi ya maeneo zinashamiri kwa kasi isiyoweza kupuuzwa.

Katika kitovu cha biashara cha Soko Kuu la Kariakoo, barabara moja iliyokuwa na maduka ya bidhaa za kawaida sasa imegeuka kuwa soko la tiba asili. Takribani maduka 40 yanayouza bidhaa za mitishamba yamepanga mstari katika eneo hilo.

Mwenendo kama huo unaonekana pia katika maeneo ya Mbagala, Buguruni na Manzese jijini Dar es Salaam ambako dawa za asili zinazozalishwa ndani na zinazoagizwa kutoka nje zinazidi kuwa sehemu ya kawaida katika kaya nyingi.

Wafanyabiashara wa Kariakoo wanasema kodi ya pango la kibanda kimoja inaweza kuanzia Sh800,000 hadi zaidi ya Sh2 milioni kwa mwezi. Uwezo wa wauzaji wa dawa hizo kulipa gharama hiyo, unaashiria kuwa si tu maarufu bali pia ina faida.

Mkazo wa maduka haya katika maeneo yenye pilika nyingi unaelezwa kuchangiwa na tabia ya wateja na urahisi wa upatikanaji.

Mmiliki wa Herbal Care Supplies, Abdallah Rashid, amesema eneo hilo ni nguzo ya mkakati wao wa biashara.

“Tupo hapa kwa sababu watu wengi huja Kariakoo kutoka maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam,” amesema. “Wateja hutafuta dawa za asili katika maeneo yanayofikika kirahisi. Ukikaribia barabara kuu na masoko ni rahisi zaidi kuonekana na kuwafikia wateja.”

Buguruni, muuzaji mwingine, Faudhia Salum, ametaja msongamano wa wakazi kama kichocheo cha biashara hiyo.

“Buguruni ina wakazi wengi, na wengi hutegemea tiba za asili. Kufungua duka eneo lenye pilika nyingi hurahisisha wateja kutufikia,” amesema. “Usajili hujenga imani kwa wateja, lakini si maduka yote yamesajiliwa rasmi. Wapo wanaofanya kazi bila uthibitisho, na hilo ni hatari kwa umma.”

Mbagala, mmiliki wa Ndola Herbal Centre, Hamisi Ndola, amesema kuhamisha biashara kutoka Kivule hadi barabara yenye pilika nyingi ilikuwa uamuzi wa kimkakati.

“Wateja hupendelea maduka yanayoonekana na kufikika kirahisi. Kuwa katika duka lililosajiliwa huwapa uhakika kuwa bidhaa zinakidhi viwango vinavyotakiwa,” amesema.

Muhudumu mwingine katika eneo hilo, Jongo Omary wa Afya Asili Centre, amehusisha ongezeko la maduka na gharama nafuu na urahisi wa huduma.

“Wateja wengi huja kwetu kwa sababu huduma ni za haraka na gharama ni nafuu. Mahitaji hayo yanachochea maduka zaidi kufunguliwa,” amesema.

Manzese, mmiliki wa Uhai Herbal Solutions, Rehema Mkinga, amesema ushindani miongoni mwa maduka yaliyodhibitiwa umeongeza presha kwa wauzaji.

“Sasa maduka ni mengi, hivyo wateja wana chaguo. Usipowaelekeza vizuri, wanaenda kwingine,” amesema. “Kuwepo hapa pia hutupa nafasi ya kuwaelimisha kwamba dawa za asili zinapaswa kutumika kwa uangalifu na kwa usahihi.”

Ameongeza kuwa maeneo yenye watu wengi huwapa fursa ya kujibu maswali na kuondoa dhana potofu.

“Watu huja na maswali kuhusu usalama na ufanisi. Hapa tunapata jukwaa la kuwaelimisha kuhusu matumizi sahihi,” amesema.

Hata hivyo, wataalamu wa afya wanaonya kuwa ongezeko la maduka, hasa yanayofanya kazi bila usajili sahihi, linaweza kuhatarisha afya za wagonjwa.

Daktari katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Temeke, Dk Agnes Kweka, amesema tiba asili ni sehemu ya urithi wa kitamaduni, lakini kutoweka wazi kwa wagonjwa kunachanganya matibabu.

“Tunaheshimu tiba asili kama sehemu ya utamaduni wetu, lakini wagonjwa mara nyingi hawawaambii madaktari wanachotumia,” amesema. “Baadhi ya dawa, zikichanganywa na zile za hospitali, zinaweza kuingiliana na matibabu au kusababisha madhara makubwa. Elimu kwa umma na udhibiti ni muhimu.”

Mfamasia na mtafiti wa tiba, Dk Clemence Mushi, amesema umma hudhani kuwa maduka yote ya mitishamba yamesajiliwa na ni salama, jambo ambalo si sahihi kila wakati.

“Baadhi ya dawa zinaweza kuwa na viambato hatari, dozi zisizo sahihi au uchafuzi,” amesema. “Watumiaji wanapaswa kuwa waangalifu, na watoa huduma kufuata miongozo ya usalama kwa ukamilifu.”

Daktari katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Mwalimu Nyerere mkoani Mara, Dk Neema Mtatiro, amesisitiza hatari ya kuchanganya dawa bila usimamizi.

“Mchanganyiko wa dawa za asili na za kisasa bila ushauri wa kitaalamu unaweza kuwa hatari,” amesema. “Uelewa na uwajibikaji ni muhimu kuzuia madhara.”

Wizara ya Afya imesema inaunga mkono tiba asili iliyo ndani ya mfumo wa udhibiti unaolinda usalama wa wananchi.

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi katika Idara ya Tiba, Dk Winifrida Kidima, amesema dawa za asili husajiliwa tu baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kisayansi.

“Kupitia Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala, tunasajili dawa baada ya kupimwa ubora, usalama na dozi sahihi kabla ya kutumika kwa binadamu,” amesema.

Ameongeza kuwa wizara hufanya ufuatiliaji wa bidhaa zilizo sokoni, zilizosajiliwa na zisizosajiliwa.

“Katika mwaka wa fedha 2024/25, tulifanya ufuatiliaji mara tatu na kutoa taarifa rasmi kwa umma. Dawa yoyote isiyokidhi viwango huondolewa kwenye daftari la usajili na umma huarifiwa,” amesema.

Katika Taasisi ya Tiba Asili ya Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), watafiti wamesisitiza kuwa ukuaji wa kibiashara lazima uendane na uthibitisho wa kisayansi.

Dk Benson Mugaka amesema dawa yoyote inayokusudiwa kwa matumizi ya binadamu lazima ipitie mchakato mkali.

“Mchakato huo unahusisha utambuzi wa mmea katika botania, uchambuzi wa kemikali katika kemia, na upimaji wa usalama na dozi katika famakolojia,” amesema. “Hakuna mmea unaopaswa kuingia sokoni bila kupitia idara zote tatu.”

Ameonya kuwa upanuzi wa kibiashara bila kufuata taratibu unaweza kuhatarisha afya za watumiaji.

“Bidhaa zisizodhibitiwa zinaweza kuwa na sumu za kuvu, metali nzito au uchafu mwingine, na baadhi zinaweza kuathiri ini au figo,” amesema. “Motisha ya kibiashara inaweza kusababisha kukwepa taratibu, na hapo ndipo hatari ilipo.”

Kadri idadi ya maduka ya dawa za asili inavyoendelea kuongezeka, mjadala kuhusu nafasi yake katika afya ya umma utaendelea kushika kasi.

Kwa baadhi ya wananchi, ni mbadala nafuu na unaofikika kirahisi. Kwa wengine, ni chanzo cha wasiwasi kuhusu usalama, udhibiti na uwezekano wa unyonyaji katika soko linalokua kwa kasi lakini lisilosimamiwa kikamilifu.

Swali linabaki je, ni dawa, sumu au biashara tu?