KOCHA wa Dodoma Jiji, Amani Josiah, amefurahishwa na mwenendo wa timu hiyo hadi sasa katika mechi za Ligi Kuu ilizocheza msimu huu, huku akisifu usajili wa kiungo wa kikosi hicho, Khleffin Hamdoun, aliyesajiliwa katika dirisha dogo la Januari 2026.
Akizungumza na Mwanaspoti, Josiah, amesema wachezaji wote waliosajiliwa katika dirisha dogo wameonyesha ushindani na nyota wengine waliopo kikosini tangu mwanzoni, ingawa usajili wa Khleffin, umetengeneza balansi nzuri ya kikosi hicho.
“Ni mchezaji anayekupa machaguo mazuri wakati timu inazuia na inaposhambulia, tulisajili kutokana na upungufu ambao sisi benchi la ufundi tuliuona mwanzoni, lengo kubwa ni kutengeneza kikosi bora cha kuendana na ushindani,” amesema Josiah.
Akizungumzia mwenendo wa timu hiyo kiujumla, Josiah amesema mwanzoni haikuwa rahisi kwenda kwenye viwanja vya ugenini na kupata pointi hata moja kwa urahisi, ingawa kwa sasa jambo hilo linawezekana na kutokana na ubora wa wachezaji wa kikosi hicho.
Khleffin amejiunga na Dodoma Jiji katika dirisha dogo lililofungwa Januari 30, 2026, baada ya kuachana na kikosi cha Coastal Union ‘Wagosi wa Kaya’, alichojiunga nacho mwanzo wa msimu huu, kufuatia kuachana na Klabu ya Muscat ya Oman.
Kiungo huyo aliyechangia bao moja la Ligi Kuu katika ushindi wa Dodoma Jiji wa mabao 3-0, dhidi ya TRA United, Februari 12, 2026, alicheza Azam chini ya kocha, Mromania Aristica Cioaba, aliyojiunga nayo Januari 8, 2020, akitokea Mlandege ya Zanzibar.