IKIWA zimesalia saa tatu kabla ya kuanza mtanange wa mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika, Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar wanaoutumia Yanga na JS Kablyie bado mambo hayajachangamka.
Yanga ni mwenyeji katika mechi hiyo ya mwisho ya kundi B ikiikaribisha JS Kablyie ambayo hadi sasa inakamilisha ratiba ikiwa tayari imeondolewa michuanoni.
Mechi nyingine ya kundi hilo ni kati ya Al Ahly dhidi ya AS Far Rabat inayopigwa Cairo, Misri.
Sasa zikiwa zimesalia saa chache kabla ya mtanange huo, bado hakuna mashabiki wengi nje ya uwanja na hata idadi ya wanaonunua tiketi sio kubwa.
Kuna idadi ndogo ya mashabiki waliojikusanya uwanjani hapo na wengi wanatoka sehemu mbalimbali nje ya Zanzibar.
Akizungumza na Mwanaspoti, mmoja wa wahudumu wa kukata tiketi, Ally Faki alisema hakuna watu wengi kutokana na muda wenyewe wa mechi kuchezwa usiku.
“Baadae ndio utaona watu, hata hawa ambao unawaona wengi wametoka Bara ndio wananunua, hapa Zanzibar saa 12 jioni ndio kunaanza kuchangamka,” amesema Faki.
Hadi sasa mageti yote bado hayajaruhusiwa kuingiza mashabiki na inaelezwa kuanzia saa 11 na nusu yatakuwa wazi.
Kwa muda huu geti moja tu ndio limeruhusu kuingiza watu ‘Gate B’ ambalo wanaingia maafisa wanaosimamia uwanja, Waandishi wa Habari na wageni maalumu.