Dar es Salaam. Mtandao wa Instagram umekuja na mfumo mpya wa mtumiaji kudhibiti maudhui ikiwemo picha na video unazotaka kuona ijulikanayo kama ‘algorithm’.
Instagram algorithm ni mfumo unaotumia kanuni na akili unde (AI) kuamua ni maudhui gani yaonyeshwe kwa mtumiaji fulani, kwa wakati fulani na kwa mpangilio gani.
Kwa lugha rahisi, ni akili ya nyuma ya pazia inayochagua, ni picha au video gani zitaonekana juu kwenye Feed yako, ni Reels zipi utaletewa, ni machapisho gani yataonekana, na ni nani ataonekana juu kwenye Stories.
Ili kukuletea maudhui mtandao wa Instagram unatumia kigezo cha tabia zako juu ya mambo gani unapenda ku-like, unapopenda kutoa maoni, video unazotazama hadi mwisho, akaunti ulizo-follow pamoja na maudhui unayo-share au kuhifadhi.
Kupitia hivyo, mfumo wa Instagram hutabiri kwamba mtu huyo huenda anapenda aina hii ya maudhui, hivyo huanza kukuletea zaidi ya hayo.
Hivi karibuni mtandao huo umekuja na mfumo wa namna ya kudhibiti algorithm ambapo hatua hiyo inakuja wakati baadhi ya watumiaji hulalamika kuona video (reels) na picha wasizotaka na bila ya kuelewa kwa nini.
Kufuatia hilo, kampuni ya Meta, inayomiliki Instagram, imetangaza kupitia tovuti yake rasmi, kuhusu kipengele kipya kinachoitwa “Your Algorithm”, kinachokupa udhibiti wa moja kwa moja juu ya kile unachokiona kwenye sehemu ya Reels.
Meta imesema hiyo ni hatua kubwa kwa watumiaji wake, hasa kwa wale wanaotumia kila siku kutazama video na kugundua mambo mapya ambapo sasa unaweza kuamua wewe mwenyewe kile unachotaka kuona mara kwa mara badala ya kukaa tu ukisubiri iamue kwa niaba yako.
Kwanza, fungua sehemu ya Reels, kisha juu kulia utaona alama mpya yenye mistari miwili yenye vimoyo ambayo ndiyo sehemu ya ‘Your Algorithm’. Ukifungua utaona muhtasari wa mada ambazo Instagram inadhani unazipenda kidogo au zaidi.
Kisha unaweza kubadilisha kwa kuongeza mada unayotaka kuona zaidi, ondoa mada usiyotaka tena, au andika mada mpya ambayo haionekani, kama vile michezo, sanaa, au mada yoyote unayopenda zaidi.
Baada ya hapo, Instagram itarekebisha mapendekezo yako ya Reels kwa wakati halisi kulingana na machaguo yako kwa mujibu wa Social Media Today.
Hata hivyo, kwa mujibu wa ripoti mbalimbali za taasisi huru za utafiti wa teknolojia barani Ulaya na Marekani, uwazi wa algorithm umeainishwa kama moja ya maeneo yanayohitaji marekebisho ili kulinda watumiaji dhidi ya taarifa potofu na maudhui hatarishi.
Sheria kama ile ya Huduma za Kidijitali (Digital Services Act) katika Umoja wa Ulaya zimeanza kuzitaka kampuni kubwa za teknolojia kuweka wazi zaidi namna mifumo yao ya mapendekezo inavyofanya kazi na kuwapa watumiaji chaguo la kubadilisha au kuondoa maudhui yanayoletwa kupitia ‘algorithm’.
Algorithm ya Instagram ilikuwa ikifanya kazi kwa siri, ikikusanya taarifa za tabia yako ya mtandaoni kama vile video uliyotazama, kupenda kisha ikatumia hizo data kutabiri unachotaka kuona.
Hii ilimaanisha mara nyingi watumiaji waliishia kuona video ambazo walikuwa hawana shauku nazo au ambayo haikuwa sawa na masilahi yao.
Sasa, kwa kutumia kipengele hiki, utakuwa na uwezo wa kupunguza mlolongo wa video zisizofaa au zisizokupendeza. Kuongeza mada unayopenda ili kuona zaidi video zinazokupa furaha au faida badala ya kubaki chini ya hatua za ‘algorithm’ ya awali.
Kwa sasa, ‘Your Algorithm’ ilianzia kwa watumiaji wa Marekani na sasa imeenea kwa watumiaji wote duniani.
Pia, Instagram imeahidi kupanua huduma hii zaidi sio tu kwenye Reels tu, bali pia sehemu nyingine kama ‘Explore’ na ‘Home feed’, siku za hivi karibuni.