Moshi. Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Moshi Vijijini, Mkoani Kilimanjaro, kimesema hakitamvumilia kiongozi yeyote ndani ya chama hicho atakayeleta mpasuko.
Hayo yamesemwa leo Februari 15,2026 na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Moshi Vijijini, Sirili Mushi, wakati akizungumza na wajumbe wa mkutano wa Halmashauri kuu wa chama hicho, katika uwasilishwaji wa taarifa ya utekelezaji wa ilani ya CCM kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2025.
Mushi amesema kuwa, jukumu la chama hicho ni kujenga umoja na mshikamano miongoni mwa wanachama wake, na kwamba hawataruhusu mpasuko kwenye wilaya, kata au matawi ya chama hicho.
Mwenyekiti wa chama cha Mapinduzi (CCM) Moshi vijijini, Sirili Mushi, akizungumza na wajumbe wa mkutano wa Halmashauri kuu ya Chama hicho, wakati wa uwasilishwaji wa taarifa ya utekelezaji wa ilani ya chama hicho. Picha na Janeth Joseph
Amesema; “Kama Mwenyekiti wenu nawahakikishia atakayeleta mpasuko kwenye ngazi yoyote ile ya chama, yeye ndiye atapasuka, hatutaruhusu yoyote yule atuyumbishe.”
Aidha, amesema ili kuimarisha zaidi utendaji wa chama hicho, wataunda umoja wa wenyeviti wa CCM wa kata zote 32 za wilaya hiyo, ambao watakuwa wakijadili masuala mbalimbali yanayohusu chama hicho.
Naye, Katibu wa chama hicho, Wilaya ya Moshi Vijijini, Ramadhan Mahanyu, amesema Serikali imefanikisha mambo makubwa katika wilaya hiyo, huku akiwataka wanachama kufanya kazi kwa umoja, mshikamano, na kuacha makundi.
Aidha, amewataka kuelewa kuwa uchaguzi umekwisha, na hivyo ni wakati wa kuendelea na kazi ya kujenga na kuimarisha chama hicho.
“Tathmini tunayoifanya mojawapo ni kuheshimiana, unakuta wewe ni diwani lazima ushirikiane na mbunge wako, wewe ni diwani au mbunge lazima ushirikiane na chama chako, tufanyeni kazi kwa umoja,” amesema Mahanyu.
Baadhi ya wajumbe wa Mkutano wa Halmashauri Kuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wakiwa pamoja wakati wa uwasilishwaji wa taarifa ya utekelezaji wa ilani ya chama hicho. Picha na Janeth Joseph
Akizungumza wakati wa uwasilishwaji wa taarifa ya utekelezaji wa ilani ya chama hicho, Mkuu wa wilaya hiyo, Godfrey Mnzava amesema kwa kipindi cha Julai hadi Desemba mwaka 2025, fedha zilizopokelewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo na halmashauri ya wilaya hiyo ni Sh47.9 bilioni.
“Katika kipindi hiki cha Julai hadi Desemba 2025 halmashauri ilikuwa tayari imeshapokea jumla ya Sh47.9 bilioni ikiwa Sh2.4 bilioni ni mapato ya ndani na Sh44.6 bilioni ikiwa ni fedha kutoka Serikali Kuu,” amesema DC Mnzava.
Amesema, katika sekta ya afya halmashauri imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo ya afya ambapo jumla ya Sh1.9 bilioni zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wilaya, zahanati nne pamoja na ukarabati wa zahanati moja.
Aidha, amesema katika usambazaji wa umeme vijijini jumla ya Sh6.1 bilioni zimetumika na Wakala wa Nishati ya Umeme Vijijini (Rea) ambapo tayari wamesambaza umeme katika vitongoji 25 kati ya 45 vilivyokuwa vimesalia.