KAMATI YA BUNGE YA MIUNDOMBINU YAISIFU DMI KWA KUZALISHA WATAALAMU WA SEKTA YA BAHARI

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu tarehe 14 Februari 2026 imetembelea Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) kwa ziara ya kikazi yenye lengo la kujua shughuli zinazofanywa na Chuo katika utekelezaji wa majukumu yake ya kitaifa.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Mwenyekiti wa Kamati Mhe. Moshi Kakoso aliipongeza menejimenti na watumishi wa DMI kwa juhudi kubwa katika kuzalisha wataalamu wanaochangia katika sekta ya bahari na usafiri wa majini. Aliahidi kuchukua hatua kuhusu changamoto na maoni yaliyotolewa na wajumbe wa Kamati na wabunge wengine ili kuhakikisha chuo kinaendelea kustawi na kufikia malengo yake ya kimkakati.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Uchukuzi Mhe. David Kihenzile alibainisha kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imejikita katika kuboresha sekta ya usafiri wa majini kupitia ujenzi, ukarabati, na upanuzi wa bandari. Amesema jitihada hizo zinategemea nguvu kazi yenye ujuzi mkubwa, na kwamba DMI ni kitovu cha kuzalisha wataalamu watakaoiwezesha sekta hiyo kukua kwa kasi.

Akizungumzia kuhusu Uchumi wa Buluu, Naibu Waziri alisema Serikali inaendeleza matumizi endelevu ya rasilimali za bahari na maziwa makuu kwa ajili ya kukuza uchumi wa taifa. Alisisitiza kuwa DMI ina wajibu wa kuzalisha wataalamu, kufanya tafiti, na kutoa ushauri wa kitaalamu utakaosaidia nchi kunufaika zaidi na rasilimali hizo. Aidha, aliongeza kuwa mafanikio ya sekta ya bahari na rasilimali za majini yanategemea kwa kiasi kikubwa wataalamu wanaotoka DMI.

Mkuu wa Chuo, Prof. Tumaini Gurumo, katika taarifa yake alieleza kuwa licha ya mafanikio yaliyopatikana, bado kuna uhitaji wa kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia, pamoja na kuendelea kuwasomesha waalimu nje ya nchi.

Aliongeza kuwa chuo katika kuliona hilo kimeanza kutekeleza mpango wa upanuzi wa huduma zake katika Mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Lindi, Mwanza, Simiyu na Pemba ili kukidhi mahitaji ya elimu na mafunzo ya bahari.

Alibainisha kuwa DMI inaendelea kunufaika kupitia ushirikiano na taasisi mbalimbali za kimataifa na sekta binafsi, ambao huchukua wanafunzi na kuwapa mafunzo kwa vitendo kwa kutumia meli zao na kubadilishana uzoefu wa kitaaluma.

Prof. Gurumo vilevile aliishukuru Serikali kwa kuendelea kukiwezesha chuo kutimiza majuku yake ikiwa ni pamoja na kukipatia vifaa vya kisasa vya kufundishia kama vile mitambo ya kisasa ya mafunzo kwa vitendo (simulators), ambavyo vimeongeza ubora wa mafunzo unaoendana na maendeleo ya teknolojia ya usafiri wa majini.

Wajumbe wa Kamati walikipongeza chuo kwa mchango wake katika kukuza sekta ya bahari na kusema kuwa wameona umuhimu wa chuo hicho kuwezeshwa kwa miundombinu bora, meli ya mafunzo na vifaa vya kisasa ili kuimarisha uzalishaji wa wataalamu kwa maendeleo ya Uchumi wa Buluu.