Aliyemlawiti mtoto wa miaka mitano akwaa kisiki Mahakama Kuu

Arusha. Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, imebariki adhabu ya kifungo cha maisha jela kwa mkazi wa Arusha, Nasibu Kilalo aliyohukumiwa kwa kosa la kumlawiti mtoto wa kiume aliyekuwa na umri wa miaka mitano wakati huo.

Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo katika hukumu iliyotolewa na Jaji Frank Mahimbali, Februari 9, 2026 baada ya kutupilia mbali rufaa ya Nasibu aliyoikata kupinga hukumu ya Mahakama ya Wilaya ya Arusha.

Jaji amefikia uamuzi huo baada ya kupitia hoja za pande zote na kuwa kesi ya mashtaka ilithibitishwa bila kuacha shaka, hivyo rufaa hiyo haina mashiko na kuitupilia mbali.

Mahakama ya Wilaya ya Arusha ilimtia hatiani Nasibu katika kesi ya jinai namba 24697/2024, baada ya kushawishika na ushahidi wa upande wa mashtaka kuwa mrufani huyo alitenda kosa hilo kinyume na Kifungu cha 154(1)(a) na (2) cha Kanuni ya Adhabu.

Ilidaiwa Agosti 4, 2024 katika Mtaa wa Shuma, Elerai, Arusha, Nasibu alitenda kosa hilo.

Katika kesi ya msingi, mwathirika wa tukio hilo (shahidi wa pili) aliripoti kwa mama yake (shahidi wa kwanza) kwamba Nasibu amemlawiti.

Shahidi wa kwanza aliieleza mahakama kuwa baada ya taarifa hizo aliwashirikisha viongozi wa eneo hilo ambapo pia mwathirika wa tukio hilo alieleza kuwa Nasibu alimwita ofisini kwa Babuu na akamfanyia kitendo hicho.

Shahidi wa tatu, Petro Stephano, ambaye ni mmiliki wa ofisi hiyo, alithibitisha kwamba mshtakiwa alikuwa ndani ya ofisi yake, alimwona mwathirika wa tukio hilo akiondoka na suruali iliyolegea.

Shahidi wa tano ambaye ni Ofisa Kliniki wa Kituo cha Afya Kaloleni, aliyemchunguza mtoto huyo, alithibitisha sehemu za siri za nyuma za mtoto huyo zilikuwa na michubuko na misuli ilikuwa imelegea, hivyo kuashiria kupenya kitu butu.

Katika utetezi wake, Nasibu alikana kutenda kosa hilo na kudai kesi hiyo ni ya uzushi kutokana na ugomvi na Joseph kuhusu deni ambalo halijalipwa.

Mahakama hiyo ya chini  baada ya kuchunguza vipengele vya kosa linaloshtakiwa, ushahidi uliotolewa na upeo wa mfumo wa kisheria unaoanzisha kosa hilo ambao ni kifungu cha 154(1)(a) na (2) cha Kanuni ya Adhabu, ilimtia hatiani mrufani na ipasavyo ikamuhukumu kifungo cha maisha jela.

Kutokana na kutoridhishwa na hukumu hiyo, Nasibu alikata rufaa akiwa na sababu sita ikiwemo kesi hiyo haikuthibitishwa bila shaka yoyote, mahakama ilifanya makosa kuamini ushahidi wa shahidi wa pili, tatu na nne ambao hawakuwa mashahidi wa kuaminika.

Nyingine ni mahakama ilishindwa kutatua utata katika ushahidi wa upande wa mashtaka, mahakama ya mwanzo ilishindwa kutathmini ipasavyo ushahidi wa utetezi.

Wakati wa kusikilizwa kwa rufaa, mrufani alikubali misingi yake ya rufaa na kuomba Mahakama ifute hukumu hiyo na kuibatilisha.

Kimsingi, mrufani anasema kwamba ushahidi wa upande wa mashtaka ulikuwa dhaifu, umejaa utata, na haukufikia kikomo cha ushahidi bila shaka yoyote.

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote na kupitia mwenendo, Jaji amesema Mahakama itaamua kama ushahidi uliotolewa ulithibitisha kosa dhidi ya mshtakiwa bila shaka yoyote.

Amesema Mahakama hiyo itaangalia na kutathmini ushahidi uliotolewa.

Kuhusu uaminifu wa mashahidi, Jaji amesema kifungu cha 127(6) cha Sheria ya Ushahidi kinaruhusu hatia kulingana na ushahidi wa mwathirika unaoaminika.

Amesema ushahidi wa shahidi wa pili ulikuwa wa kuaminika na uliothibitishwa na shahidi wa tatu na nne ambao waliunga mkono mfuatano wa matukio.

Jaji amesema hoja ya utata kuhusu ushahidi wa upande wa mashtaka, utata unaodaiwa ulikuwa mdogo na haukuathiri kiini cha kesi na kuhusu utetezi wa mrufani kuhusu uzushi haukuzingatiwa, amesema haukuonekana kuridhisha kwani mwathirika wa tukio aliripoti kwa mama yake siyo Joseph na ushahidi wa kimatibabu ulithibitisha.

“Baada ya kuzingatia misingi yote ya rufaa, Mahakama hii inaona kwamba upande wa mashtaka ulithibitisha kesi hiyo bila shaka yoyote. Mahakama ya mwanzo ilimuhukumu mrufani huyo kwa ipasavyo chini ya Kifungu cha 154(1)(a) na (2) cha Kanuni ya Adhabu (juu),”amesema Jaji

 Mahakama hiyo ilitupilia mbali rufaa hiyo na kuthibitisha hukumu na adhabu ya kifungo cha maisha jela iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Arusha.