Ukosefu wa vyoo kuwang’oa wakurugenzi, ma-DAS

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Mwigulu Nchemba, amewabana mawaziri wanne na manaibu wao kujibu hoja zilizotolewa na Mbunge wa Mkinga, Twaha Mwakioja, huku akiwaagiza wakuu wa mikoa, wakurugenzi kuhakikisha shule, vituo vya afya vinakuwa na matundu ya vyoo kabla ya tathmini ya utekelezaji wa bajeti 2026/27.

Hatua hiyo ilikuja baada ya mbunge huyo kuibua masuala ya barabara, maji, wanyama wakali na matumizi ya rasilimali za bahari, akitaka ufafanuzi wa kina kuhusu utekelezaji wa miradi hiyo katika jimbo lake.

Dk Mwigulu amewabana mawaziri hao leo Februari 15, 2026 wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa miundombinu ya Chuo Kikuu Mzumbe kampasi ya Tanga ambayo hadi kukamilika kwake kutagharimu zaidi cha Sh12 bilioni.

Kuhusu barabara ya Mabokweni kwenda Maramba hadi Hombomtini, Kwa Mndolwa hadi Old Korogwe yenye urefu wa kilomita 127, Waziri Mkuu amemwelekeza Naibu Waziri wa Ujenzi, Godfrey Kasekenya, kueleza ni lini ujenzi utaanza.

Akijibu, Kasekenya amesema Serikali ilikubaliana kuanza na kipande cha kilomita 20, ambapo kilomita 10 ni kutoka Mtakwa kwenda Maramba na nyingine kutoka Kwa Mndolwa kwenda Korogwe.

Kasekenya amesema zabuni kwa awamu ya kwanza iliwahi kutangazwa, lakini bei za makandarasi zilikuwa juu, hivyo mchakato ukarudiwa na kwa sasa kilomita 10 zimetangazwa tena ili kumpata mkandarasi.


Baada ya maelezo hayo, Dk Mwigulu amemtaka Naibu Waziri kuhakikisha kila hatua inawasilishwa kwa mbunge ili naye awape mrejesho wananchi.

Awali, Mwakioja amesema kukamilika kwa barabara hiyo kutaleta ukombozi wa kiuchumi kwa wakazi wa Mkinga kutokana na kurahisisha shughuli za kijamii na biashara, akisisitiza kuwa licha ya kuwepo kwenye bajeti ya mwaka wa fedha huu, bado hajaona utekelezaji wa kuridhisha.

Kuhusu changamoto ya maji, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amesema Serikali imeshaanza utekelezaji wa mradi wa zaidi ya Sh35 bilioni wa kupeleka maji kutoka Tanga Mjini hadi Mkinga na Holoholo.


Amesema mradi huo umefikia asilimia 70 na vijiji 37 vinatarajiwa kunufaika na huduma ya maji safi na salama.

Aweso amesema Rais Samia amesisitiza kutatua adha ya maji hususan kwa wanawake, akibainisha kuwa maeneo mengi ya Mkinga yana changamoto ya maji ya chumvi kutokana na ukaribu na bahari.

Kwa upande wake, Mwakioja alitaka Mkinga iunganishwe kwenye gridi ya Taifa ya maji, akieleza kuwa mabadiliko ya tabianchi yamechangia kukauka kwa baadhi ya vyanzo vya maji.

Akijibu hoja ya wanyama wakali na ombi la kuanzishwa kituo cha Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (Tawa), Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji, amesema katika bajeti ya 2025/26 wizara ilitengewa vituo 20, ambapo 14 tayari vimepatikana na sita vimebaki.

Amesema kituo kimoja kitajengwa Mwanyumba pamoja na lango la Umba, hatua inayotarajiwa kusaidia kudhibiti changamoto ya wanyama wakali katika eneo hilo kwa kushirikiana na mamlaka za uhifadhi wa misitu.

Kuhusu matumizi bora ya rasilimali za bahari na ombi la kuanzishwa ndaki, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dk Bashiru Ally, amesema Serikali ina mpango wa kujenga bandari ya tatu ya uvuvi katika Wilaya ya Pangani.

Amesema kwa sasa ujenzi wa bandari ya uvuvi ya Lindi unaendelea na usanifu wa bandari ya Bagamoyo unafanyika, huku mradi wa Pangani ukiwa katika mpango wa muda ujao.

Ameongeza kuwa bandari hizo zitapanua uwezo wa kuchakata mazao ya samaki na kuchochea uwekezaji wa viwanda, akizitaka taasisi za elimu ya juu kuandaa wataalamu watakaokidhi mahitaji ya sekta ya uvuvi wa kisasa.

Wakurugenzi kupimwa kwa vyoo

Aidha, Dk Mwigulu, ametoa onyo kali kwa wakurugenzi wa halmashauri nchini akisisitiza kuwa ndani ya miezi sita ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2025/26 hataki kusikia shule yoyote haina matundu ya vyoo.


Akimuelekeza  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Profesa Riziki Shemdoe kuwaandikia maofisa tawala wa mikoa na wakurugenzi wote wa halmashauri, Dk Mwigulu amesema maandalizi ya bajeti yanaendelea na hakuna sababu ya kuingia mwaka mpya wa fedha huku shule za msingi na sekondari zikiwa na upungufu wa miundombinu ya vyoo.

“Tunaelekea kukamilisha maandalizi ya mwaka wa fedha 2025/26. Tukishaanza utekelezaji wa bajeti mpya, ndani ya miezi sita sitaki kusikia habari ya shule haina matundu ya vyoo. Haya ni mambo yanayoturudisha nyuma na yanatia aibu,” amesema.

Amesema haikubaliki kwa nchi inayopanda hadhi kiuchumi kuendelea kuwa na shule zenye wanafunzi 200 hadi 300 bila vyoo vya kutosha, huku wakati huohuo Serikali ikitekeleza miradi mikubwa ya maendeleo ikiwamo ya vyuo na taasisi nyingine.

“Hatuwezi kuwa na miradi mikubwa kama hii halafu tuna shule hazina matundu ya vyoo. Huu ni uzembe wa watu wasiotembelea maeneo yao ya kazi,” amesema.

Waziri Mkuu amesisitiza kuwa katika ziara za tathmini ya utekelezaji wa bajeti, halmashauri itakayobainika kuwa na shule, kituo cha afya au zahanati isiyo na vyoo vya kutosha, mkurugenzi wake atawajibika.

“Nikiona halmashauri ina shule ya msingi, sekondari, kituo cha afya au zahanati haina matundu ya vyoo au ina upungufu mkubwa, mkurugenzi utakuwa umeshapoteza kazi yako. Utatufaa nini kama huwezi kusimamia jambo la msingi kama hilo?” amehoji.

Amesema ujenzi wa vyoo si jambo la kuhitaji mijadala mikubwa, akieleza kuwa hata kwa rasilimali zilizopo halmashauri zinaweza kupanga na kutekeleza ujenzi huo bila kusubiri maelekezo ya ziada.

“Gari moja linaweza kujenga matundu ya vyoo ya halmashauri nzima. Mnaombaje fedha za mambo mengine, hamuombi za matundu ya vyoo?” amesema.

Ameagiza barua ya maelekezo itolewe kwa wakurugenzi wote na nakala ziwasilishwe kwa wakuu wa mikoa ili kuhakikisha suala hilo linasimamiwa kwa karibu kabla ya kukamilika kwa miezi sita ya kwanza ya utekelezaji wa bajeti mpya.

Awali akizungumza katika mkutano huo, Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wanu Hafidh Ameir amesema kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, Serikali inalenga kusogeza huduma za elimu ya juu karibu na wananchi na kuboresha ubora wa mafunzo.

Amesema wizara imejipanga kusimamia utekelezaji wa mradi huo kwa kuzingatia thamani ya fedha, ubora na muda uliopangwa ili kuhakikisha malengo yanatimia.

Amesema chuo hicho kinachojengwa katika kata ya Gombero, Halmashauri ya Wilaya ya Mkinga mkoani Tanga, unatekelezwa kupitia mradi wa HEET.

Miradi inayoendelea kutekelezwa kupitia mpango huo ni Ujenzi wa Jengo la Taaluma lenye jumla ya madarasa sita, maktaba ndogo, ukumbi wa mihadhara, maabara mbili zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 80 kila moja, pamoja na ofisi 36 zitakazohudumia wafanyakazi 72.

Aidha, majengo mengine ni hosteli mbili za wanafunzi, bwalo la chakula, kituo cha afya kitakachohudumia wanafunzi, wafanyakazi na wananchi wa vijiji vilivyopo jirani na chuo, nyumba nne za wafanyakazi, mfumo ya majitaka na dampo la kuhifadhia taka ngumu pamoja na tenki la kuhifadhi Maji Safi la ujazo wa lita 400,000.

Hadi kufikia Februari 13, 2026 ujenzi wa kampasi hiyo ulikuwa umefikia asilimia 82.

Ziara hiyo imeibua mjadala mpana kuhusu kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo Mkinga, huku Waziri Mkuu akisisitiza uwajibikaji na mawasiliano ya karibu kati ya mawaziri na wabunge ili wananchi wapate mrejesho wa wakati.